Monday 11 November 2013

Wingu jeusi chadema: Zitto amlima barua Dk Slaa


“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” Zitto 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Novemba11  2013  saa 8:21 AM
Kwa ufupi
  • Zitto amlima barua Dk Slaa akimtaka atolee maelezo ripoti ya kumchafua mitandaoni, Dk Mkumbo aishutumu idara ya Mnyika, mwenyewe atoa ufafanuzi


Dar es Salaam. Mgogoro ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), umeingia katika sura mpya baada ya viongozi wake wawili waandamizi, Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo kuuandikia uongozi wa chama hicho wakitaka uikane taarifa inayowachafua mitandaoni.
Zitto na Dk Mkumbo wanatuhumiwa kupokea fedha na kushirikiana na viongozi wa Idara ya Usalama wa Taifa na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa nia ya kuivuruga Chadema.
Taarifa hiyo yenye kichwa cha habari `Ripoti ya siri juu ya Zitto Kabwe’, ambayo imesambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii katika siku za karibuni inadaiwa kuwa iliandaliwa na Kitengo cha Upelelezi cha Chadema baada ya uchunguzi wa mwenendo wa Zitto ndani na nje ya nchi kuanzia mwaka 2008.
Sehemu ya taarifa hiyo ya mtandaoni inadai kuwa Zitto alipelekewa kiasi cha Dola za Marekani 266,000 (Sh416 milioni) huko Ujerumani na maofisa wa Usalama wa Tanzania, Desemba 16, 2009.
Ripoti hiyo inadai kuwa fedha hizo zilipitishwa katika Benki ya Berliner ya Ujerumani kwenye akaunti ya raia wa nchi hiyo, Andrea Cordes, ambaye anadaiwa kumpelelekea Zitto.
Taarifa zaidi zinadai kuwa fedha hizo ziligawiwa kwa wafuasi mbalimbali wa chama hicho na miongoni mwao ni Dk Mkumbo.
Zitto amlima barua Dk Slaa
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema amemwandikia barua Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa kumwomba athibitishe ‘Taarifa ya Siri ya Chadema’ kama ni ya kweli au chama hicho kiikanushe ili aweze kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waandishi wa kile alichokiita ‘hekaya.’
“Taarifa ya Chadema inasema kwamba chama hicho (chama changu), kilikuwa kimechunguza mwenendo wangu tangu mwaka 2008 hadi 2010 na kubaini kuwa mimi ninapokea fedha kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuivuruga Chadema,” alisema Zitto kwenye taarifa yake.
Zitto alisema taarifa hiyo ni ya kutunga na iliyojaa uongo wa kiwango cha kutisha, imemfedhehesha, imemsikitisha na kumkasirisha.
Alisema taarifa hiyo iliibuliwa katika kipindi ambacho alikuwa ziarani barani Ulaya katika nchi za Uswisi na Uingereza ambako alikuwa anafuatilia fedha zilizofichwa na Watanzania katika nchi hizo.
“Pengine lengo la ripoti hiyo lilikuwa ni kutaka kunipoteza kutoka katika nia na dhamira yangu ya dhati ya kutaka Watanzania wafaidike na utajiri wao. Muda ambao watunzi wa ripoti hiyo waliamua kutoa taarifa yao unazua maswali mengi kuliko majibu,” alieleza Zitto katika taarifa yake.

SOURCE: MWANANCHI

READ MORE THIS STORY : mwananchi