Monday 11 November 2013

Ofisa Uhamiaji Kia atuhumiwa kumtukana Rais

Rais Jakaya Kikwete. 
Na Daniel Mjema, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Novemba11  2013  saa 9:54 AM
Kwa ufupi
  • Tukio hilo ambalo limefanywa siri kubwa, lilitokea Oktoba Mosi mwaka huu 10:00 alasiri katika Baa ya G5 iliyopo Bomang’ombe wilayani Hai na jalada la uchunguzi namba  BNG/IR/3498/2013 limeshafunguliwa.

Bosi wake katika Mkoa wa Kilimanjaro, amekiri  kuwa na taarifa kuhusu tukio hilo lililotokea kwenye baa.
Moshi. Ofisa Uhamiaji wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia), mwenye cheo cha Sajenti ameingia matatani baada ya kutuhumiwa kumtukana matusi ya nguoni Rais Jakaya Kikwete.
Kutokana na kashfa hiyo, Polisi mkoani Kilimanjaro, wamependekeza ofisa huyo achukuliwe hatua za kinidhamu kwa kukiuka kiapo cha utii kwa Rais wakati akihitimu mafunzo yake.
Tukio hilo ambalo limefanywa siri kubwa, lilitokea Oktoba Mosi mwaka huu 10:00 alasiri katika Baa ya G5 iliyopo Bomang’ombe wilayani Hai na jalada la uchunguzi namba  BNG/IR/3498/2013 limeshafunguliwa.
Mkuu wa Uhamiaji wa Mkoa wa Kilimanjaro, Johannes Msumule, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba wanalifanyia kazi.
Msumule alisema ofisi yake inafahamu tukio hilo lakini akataka lisiandikwe magazetini kwanza kwa maelezo kuwa watalitolea taarifa baadaye.
Alisema juzi alikuwa jijini Dar kushughulikia suala hilo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo.
Habari kutoka polisi zilisema ofisa huyo alitoa matusi ambayo hayaandikiki dhidi ya Rais.
Inasemekana alifanya hivyo baada ya kutakiwa kulipa ankara ya  vinywaji alivyokuwa amehudumiwa katika baa hiyo.
“Alimtolea matusi mhudumu aliyempelekea bili na baadaye  Rais kwa kumtolea matusi ya nguoni,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Inasemekana baada ya kutoa matusi hayo, wananchi waliokuwa katika eneo hilo walichukizwa na kupiga simu polisi na kwa mkuu wa upelelezi wa wilaya hiyo.

Read more: mwananchi