Wednesday 13 November 2013

MKUU WA WILAYA AFIA NDANI YA DALADALA DAR

DC Samizi afariki akiwa kwenye daladala
Na Joseph Zablon na Pamela Chilongola, Mwananchi

Posted  Jumatano,Novemba13  2013  saa 9:7 AM
Kwa ufupi
Akizungumza kwa niaba ya familia ya Samizi nyumbani kwake, Tegeta Dar es Salaam, Katibu Mkuu msataafu wa CCM, Yusuf Makamba alisema maziko yatafanyika leo baada ya swala ya adhuhuri.

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuongoza maziko ya Mkuu wa zamani wa Wilaya mbalimbali nchini, Mussa Samizi aliyefariki Dar es Salaam, juzi.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Samizi nyumbani kwake, Tegeta Dar es Salaam, Katibu Mkuu msataafu wa CCM, Yusuf Makamba alisema maziko yatafanyika leo baada ya swala ya adhuhuri.
Makamba alisema, “Nilizungumza na Samizi muda mfupi,  baadaye nilipata simu kuwa mtu huyu amefariki... Wale mabwana walipiga baada ya kuchukua simu yake na kuangalia mtu wa mwisho kuzungumza naye.
“Baadaye ya kunieleza kuwa amefariki kwenye daladala, nikawaambia wampeleke Hospitali ya Lugalo kwa ajili ya taratibu nyingine... Kimsingi alikuwa anakwenda ofisi za TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania).”
Enzi ya uhai wake, Samizi aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya za Kasulu, Kigoma Mjini, Tabora, Handeni na Moshi mkoani Kilimanjaro ambako alistaafu.
Nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Habari Tanzania (Shihata) na Shirika la Ujenzi wa Barabara (Mecco).
Kamanda wa Mkoa wa Kinondoni, Camilus Wambura alisema taarifa za msiba huo alipewa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana baada ya kutaka apewe ulinzi kwa ajili ya msiba huo.
“Mimi sina taarifa ya aliyekuwa mkuu wa wilaya kufariki akiwa kwenye daladala, ninachojua alikuja Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni leo  (jana)  asubuhi ili nimpatie walinzi kwa ajili ya kwenda nao kwenye msiba,” alisema Wambura.
Ilielezwa kwamba alikuwa anasumbuliwa na kisukari. Samizi ameacha mjane na watoto watatu.
 CHANZO: MWANANCHI