Saturday 9 November 2013

Mkakati wa serikali kuziba midomo wanahabari wakwama Bungeni

“Mheshimiwa Spika, nimesimama kuona hata wa upande wangu wamenisaliti, duh, basi naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina mmoja, mmoja ili tujiridhishe,” alisema AG Werema jana. PICHA | EDWIN MJWAHUZI 
Na Habel Chidawali, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Novemba8  2013  saa 23:26 PM
Kwa ufupi
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.

Dodoma. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema jana ameangukia pua baada ya Bunge kukataa mapendekezo ya Serikali ya kubadili baadhi ya vipengele vya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya makosa ya uchochezi.
Kadhalika Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliungana na wabunge wengine kukataa mapendekezo hayo na kudai kuwa wakati umefika kwa Serikali kupeleka bungeni muswada wa sheria ya vyombo vya habari, badala ya kutoa ahadi zisizo na majibu kila wakati.
Kukataliwa kwa mapendekezo hayo ni pigo kwa Serikali na Jaji Werema ambaye juzi wakati akijibu hoja za wabunge alijigamba kwamba yeye anasimamia amani ya nchi kwa hiyo vifungu hivyo haviwezi kuondolewa, kwani anafanya kazi kwa masilahi ya taifa na hategemei magazeti kwa ajili ya kuwa mbunge.
“Sitegemei magazeti kuwa mbunge nafanya kazi ya taifa. Walio wangu watanikataa na wasiokuwa wangu watanikataa. Nipo kwa ajili ya taifa sitamwangukia mtu yeyote miguuni,” alisema Werema, kauli ambayo iliwachefua wabunge.
Hata hivyo, jana baada ya Spika kuwahoji wabunge na kukataa mapendekezo ya Serikali, Jaji Werema alionekana kukereka hivyo alisimama na kutaka Spika aruhusu kura zihesabiwe katika kifungu hicho.
“Mheshimiwa Spika, nimesimama kuona hata wa upande wangu wamenisaliti, duh, basi naomba kura zihesabiwe kwa kuita majina mmoja, mmoja ili tujiridhishe,” alisema Werema.
Hata hivyo, Spika alikataa na kusema: “Kama kuna eneo ambalo tumefanyia utani Serikali ni katika eneo hili, naomba Serikali mtuletee muswada bungeni siyo porojo za maneno.”
Katika marekebisho hayo, Serikali ilikuwa ikipendekeza katika sheria hiyo mabadiliko ya kuongeza adhabu kwa waandishi wa habari watakaopatikana na hatia ya kuandika habari za uchochezi, kutoka faini ya Sh15,000 hadi kiasi kisichozidi Sh5 milioni.
Hata hivyo, wakati Bunge lilipoketi kama kamati wabunge walikataa kupitisha marekebisho hayo ambayo yalikuwa sehemu ya Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa mwaka 2013, wakisisitiza kwamba Serikali ipeleke bungeni muswada wa sheria ya habari.
Moto wa wabunge
Moto wa wabunge hao uliwashwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), ambaye alipendekeza sehemu ya nane ya muswada iliyokuwa na vipengele vya 39, 40 na 41 iondolewe ili kuishinikiza Serikali kupeleka bungeni sheria nzima inayohusu vyombo vya habari.
Mbunge huyo alisema kuwa sehemu hiyo na vipengele vyake kama vingepitishwa vingeifanya Serikali kuwa kimya na kushindwa kupeleka bungeni Muswada wa Sheria ya Vyombo vya Habari kama ilivyoahidi kwa muda mrefu.

“Mimi nimekuwa mbunge hapa huu mwaka wa nane, lakini kila siku Serikali imekuwa na kigugumizi cha kuleta muswada huo. Kila mara tunaambiwa kuwa utaletwa, lakini hauletwi sasa mpango wa kuleta vitu nusu-nusu haufai,” alisema Selukamba.
Mbunge huyo alilalamika kuwa baadhi ya viongozi walishapendekeza kuwa watu wote wanaopigia kelele sheria hiyo waangaliwe hati zao za kusafiria kwa madai kuwa zinatia shaka jambo alilosema kuwa yuko tayari kufanya hivyo ilimradi ahakikishe anasimamia kweli.
Jenista Mhagama
Baada ya Serukamba kutoa hoja hiyo, wabunge wengi walisimama kumuunga mkono ndipo akapewa nafasi ya kuchangia Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama ambaye pia alisisitiza kwamba lazima sheria ya vyombo vya habari ifikishwe bungeni.
Mhagama alisema kutokana na kigugumizi cha Serikali, tayari kuna gharama ambazo zimekuwa zikijitokeza ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kutumwa India kwa ajili kujifunza mambo mbalimbali yanayoendana na sheria hiyo, lakini bado hata hivyo haijasaidia kitu.
Mhagama na Serukamba tangu wakati mjadala wa  sheria ulipoanza juzi walisisitiza kuunga mkono kuletwa kwa sheria ya vyombo vya habari. Serukamba alisema akichangia muswada huo alihoji: “Kuna nini hapa? Maana hii tabia ya kuchomoa vipande vipande na kutuletea hapa haina tija.”
“Tukatae vipengele hivi, nawaomba wabunge wenzangu mniunge mkono katika hili na ikiwa tutavikataa vipengele hivi Serikali italeta sheria nzima hapa, mimi sina tatizo na adhabu hata ingekuwa mara tatu, lakini tuleteeni sheria nzima, mnaogopa nini?” alihoji Serukamba.
Mhagama yeye alisema kwa muda mrefu wadau wa vyombo vya habari wamelalamikia kuwapo kwa sheria hiyo itakayolinda tasnia ya habari, lakini Serikali mara zote imekuwa ikipiga danadana.
“Kwa nini Serikali inachelewa kuwasilisha muswada wa sheria bungeni? Hebu sasa tukae na wadau tukubaliane mambo ya msingi, tuwe na sheria ili kuinusuru tasnia ya habari, sheria itasaidia kuwadhibiti makanjanja, wapo watu wanaoidhalilisha tasnia ya habari bila sababu za msingi,” alisema.
Taarifa ya Serikali iliyotolewa bungeni jana ilisema Muswada wa Vyombo vya Habari uko tayari na kwamba wakati wowote unaweza kupelekwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa kuwa sheria.
Wabunge wengine
Vipengele hivyo vilipingwa na wabunge wengi tangu mwanzo, akianza Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) pamoja na Wabunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya na Martha Mlata (CCM).

Tundu Lissu
Katika maoni ya Kambi ya Upinzani, Lissu alisema mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Magazeti hayana msingi kwa sababu; hakuna ushahidi wowote kwamba adhabu zilizoko katika vifungu vya 36(1) na 37(1)(b) zinazopendekezwa kuongezwa zimeshindwa kudhibiti makosa ya uchochezi.
“Tangu sheria hiyo ilipotungwa miaka zaidi ya 37 iliyopita, hakuna mwandishi wa habari au mchapishaji wa gazeti lolote ambaye amewahi kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia ya makosa hayo. Badala ya kuwapeleka wakosaji mahakamani,  Serikali imejenga utamaduni wa kufungia magazeti na kutisha waandishi habari,” alisema Lissu na kuongeza:
“Hii peke yake inathibitisha hoja kwamba sheria ilitungwa kwa malengo ya kisiasa ya kudhibiti wakosoaji na wapinzani wa Serikali na watawala na si kuzuia makosa ya jinai”.
Bulaya
Bulaya kwa upande wake alisema, Serikali inafanya makosa makubwa kwa kutaka kuwaadhibu waandishi wa habari, pasipo kujenga msingi imara wa uandishi wenyewe kama taaluma katika nchi.
“Kwa nini Serikali inawaza adhabu kali tu? Kuongeza faini kutoka Sh15,000 hadi Sh5 milioni, hapo kuna nini, lazima tujiulize maana kwa kufanya hivi tunawaumiza waandishi wa habari ambao wengi wao hawana uwezo wa kulipa hizo fedha,”alisema Bulaya na kuongeza:
“Sheria nzima ikiletwa hapa, tutakuwa na uwezo wa kuangalia mambo mengi yakiwamo masilahi ya waandishi wa habari, lakini pia kuwabana watu ambao hawataki kutoa habari ila wanasubiri waandikwe ndipo wajitokeze kulalamika.”
Mlata
Naye Martha Mlata katika mchango wake alisema wanasiasa ndio wamekuwa wakiwatumia waandishi wa habari na kwamba faini iliyowekwa na Serikali ni mbaya kwani ni mzigo kwa waandishi wa habari.
“Na sisi wanasiasa tuache kuwatumia waandishi wa habari na ninyi waandishi wa habari msikubali kutumiwa na wanasiasa, tukitaka kuwatumia mkatae na mfanye kazi kwa kumwogopa Mungu kila mtu kwa dini yake,” alisema Mlata.
Walioishabikia sheria

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) walishabikia kuwapo kwa adhabu kali kwa waandishi wa habari, kwa maelezo kwamba wamekuwa wakitumiwa kuwachafua watu.
Chana alisema: “Katika malengo ya Serikali ilipoleta marekebisho haya wametuambia kwamba malengo yake ni kuongeza adhabu ili kulinda matumizi ya lugha ya matusi, makosa haya yanajumuisha matumizi ya lugha za uchochezi zinazoweza kusababisha machafuko katika jamii.
“Ni ukweli kila Mtanzania anafahamu kuwa magazeti yetu kuna wakati yanatumika na kikundi fulani, kuwabeba kikundi fulani au mtu fulani na kuangamiza mtu fulani au kikundi fulani.
Aliliomba Bunge litoe majibu pale magazeti yanapomdhalilisha mtu kwa kuandika jambo ambalo halina ushahidi wa kimahakama. “Nawauliza wahariri, pale magazeti yanapotumika kuchochea ndivyo sivyo tufanyaje? Je, huo ndio uhuru wa habari?” alihoji.
Nchemba kwa upande wake alisema hakuna haja ya kusubiri sheria mpya na
 kwamba kusubiri kunaweza kutoa mwanya kwa vyombo vya habari kuitumbukiza nchi kwenye machafuko.

SOURCE: MWANANCHI