Wednesday 20 November 2013

Mauaji Dar; Mtu mmoja aua,ajeruhi na kujiua kwa risasi


Polisi wakikagua gari walilokuwa wakisafiria watu wanne kabla ya kushambuliwa kwa risasi na mtu alitajwa kuwa jina la Gabriel Munisi aliyedaiwa kuua watu wawili na yeye kujiua baada ya kujeruhi wengine jana asubuhi jirani na Club ya Wazee, Ilala, jijini Dar es Salaam. Picha ndogo polisi wakikagua silaha iliyotumika.Picha na Silvan Kiwale 
Na Pamela Chilongola, Mwananchi

Posted  Jumatano,Novemba20  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi

Mfanyabiashara aua, ajeruhi na kisha kujiua kwa risasi kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi


Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa magari, Gabriel Munisi (35), jana alijiua baada ya kumuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watatu jijini Dar es Salaam katika tukio linalohusishwa na wivu wa mapenzi.
Munisi, ambaye alikuwa mkazi wa Mwanza, aliwapiga risasi watu watatu akiwamo mchumba wake, Christina Alfred katika Mtaa wa Bungoni Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam.
Baada ya kumpiga risasi mchumba wake huyo na kudhania kwamba amemuua, inadaiwa kwamba Munisi aliendelea kuwamiminia risasi watu wengine na kumuua mdogo wake Christina, Alpha (22).
Katika tukio hilo, Christina na mtu anayedaiwa kuwa mchumba wake mpya, Francis Shumila wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kujeruhiwa. Mama yake Christina, Helen Alfred amelazwa katika Hospitali ya Amana baada ya kujeruhiwa pia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marieta Minangi alisema Munisi alikutwa na bastola moja, magazini mbili na yalikutwa maganda 14 ya risasi zilizotumika na risasi mbili ambazo zilikuwa hazijatumika.
Tukio hili limetokea mwezi mmoja baada ya mwandishi wa habari wa ITV, Ufoo Saro kujeruhiwa kwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi.
Katika tukio hilo, Mushi alijiua baada ya kumuua mama mzazi wa Ufoo na inaaminika pia tukio hilo lilisababishwa na masuala ya mapenzi.
Lilivyotokea
Mashuhuda waliokuwapo katika tukio hilo walisema mauaji hayo yalitokea saa 1.15 asubuhi baada ya Munisi kufika Ilala Bungoni na kwenda katika Klabu ya Wazee iliyo jirani na eneo yalipotokea mauaji na kunywa supu kabla ya kusogea karibu na lango la nyumba anakoishi mchumba wake.
Mmoja wa majirani, Noel Gerald alisema alimuona Munisi akiwa amesimama karibu na lango la nyumbani kwa kina Christina.
Alisema baadaye waliona gari aina ya Toyota Hilux, Surf, likitoka katika lango la nyumba hiyo na mara walimuona Munisi akimwamuru dereva ashushe kioo lakini alikataa na kudai kwamba ndipo alipoamua kuwapiga risasi waliokuwamo kwenye gari hilo.

SOMA ZAIDI: Mauaji