Wednesday 20 November 2013

Hatari: Dawa, kemikali zinavyosababisha watoto kuzaliwa na viungo visivyokamilika

Mtoto mwenye matatizo katika ubongo ambayo wakati mwingine huhusishwa na matumizi ya dawa na kemikali hatari anazotumia mjamzito. Picha na Maktaba.  
Na Herieth Makwetta, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Novemba15  2013  saa 14:16 PM
Kwa ufupi
  • Dawa zinazoleta madhara si zile zinazotumika mara kwa mara, lakini kwa bahati mbaya wapo wanawake wanajigundua kwamba wamebeba ujauzito na hawa wanajikuta wakitumia dawa hizo ambazo mwishowe zinawaletea madhara katika ujauzito na hawezi kugundua mpaka atakapojifungua japokuwa wapo ambao mimba zao huharibika,” anasema Dk Masawe.

Hili ni tatizo kubwa na ambalo linazidi kujitokeza, lakini ambalo kama litaachwa liendelee lilivyo litaiangamiza jamii
Kujifungua mtoto asiyetimia viungo vyake vyote, mwenye matatizo ya viungo au viungo visivyo vya kawaida hutokana na vitendo au matukio hatarishi yaliyofanyika katika mwili wa mama, kuanzia siku moja hadi miezi mitatu tangu mimba kutungwa.
Kitu chochote ambacho ni sumu, dawa, kemikali, mionzi na mgawanyiko wa seli wakati wa uumbaji  wa mtoto zimetajwa kuwa sababu kuu za tatizo hilo.
Madaktari mbalimbali waliozungumza na gazeti hili wametoa sababu mbalimbali huku wakisisitiza kuwa mpaka sasa dunia bado haijapata sababu maalumu inayosababisha matukio kama hayo kutokea, lakini zipo sababu  zinazoaminika kuwa chanzo cha hayo.
Dk Cyriel Massawe Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Afya ya Uzazi  wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anasema mwanamke mjamzito hashauriwi kunywa dawa ya aina yoyote ile kama hajapata ushauri kutoka kwa daktari ni kutokana na baadhi ya dawa kuainishwa kwamba huenda yanaweza kuchangia kuvuruga uumbaji siku za mwanzo za ujauzito.
Anaongeza: “Hali hiyo husababisha seli kushindwa kugawanyika vizuri kila moja kwenda kufanya kazi ile inayokusudiwa katika uumbaji wa mtoto hapo ndipo tatizo huanza kutokea.”
Anatoa mfano kuwa kuwa tatizo kubwa linalowapata watoto walioungana pia linaweza kusababishwa na kutogawanyika vizuri kwa seli wakati wa utungwaji wa pacha.
“Mfano mzuri ni watoto walioungana, hawa ni wale wa mfuko mmoja. Yai moja linapogawanyika mara mbili ni nadra kutokea kosa, lakini katika uumbaji seli zikishindwa kugawanyika vizuri na kufanya uumbaji uliotimifu hapo pacha wataungana matumbo, migongo, vichwa na sehemu zingine za mwili au mmoja asitimie kama ilivyotokea hivi karibuni,” anasema.
Anasema iwapo mama hakutumia vidonge au dawa za aina yoyote basi yawezekana tatizo ni la kiasili na hali hii hutokea katika hatua za mwanzo wa ujauzito na hata mwanamke akienda hospitali huambiwa kwamba atajifungua watoto mapacha lakini hali huwa ndivyo sivyo.
Anakiri kwamba kuna idadi kubwa ya wanawake ambao hutumia dawa miezi ya mwanzo kabla ya kujigundua kwamba ameshika mimba  huathirika zaidi.
“Dawa zinazoleta madhara si zile zinazotumika mara kwa mara, lakini kwa bahati mbaya wapo wanawake wanajigundua kwamba wamebeba ujauzito na hawa wanajikuta wakitumia dawa hizo ambazo mwishowe zinawaletea madhara katika ujauzito na hawezi kugundua mpaka atakapojifungua japokuwa wapo ambao mimba zao huharibika,” anasema Dk Masawe.
Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto katika Hospitali ya Muhimbili, Dk Zaitun Bokhary anasema mama mjamzito hutakiwa kutumia dawa za ‘folic acid’ kabla na baada ya ujauzito ili kuepuka kujifungua mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa (Hydrocephalus) na Mgongo wazi (spina bifida).

SOMA ZAIDI: Dawa--kemikalI