Tuesday 19 November 2013

CUF yakiri Dk Shein ndiye msemaji wa Serikali Z’bar

Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Masoud Hamad PICHA|MAKTABA 
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi

Posted  Jumanne,Novemba19  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Yakiri pia kuwa, yaliyosemwa na Maalim Seif Sharif Hamad ni mtazamo wake binafsi kama kiongozi wa kisiasa.


Zanzibar. Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kinaunga mkono kauli ya Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kuwa yeye ndiye msemaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na yaliyosemwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad ni mtazamo wake binafsi kama kiongozi wa kisiasa.
Msimamo huo umewekwa wazi na Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Hamad Masoud Hamad katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mtendeni mjini Unguja jana.
Hatua hiyo ya Hamad imekuja siku chache baada ya Rais wa Zanzibar, Dk Shein kuwaambia waandishi wa habari kuwa hakuna mwenye mamlaka ya kuizungumzia Zanzibar isipokuwa yeye.
Hamad alisema, Makamu wa Kwanza wa Rais anapozungumza na kutoa msimamo wake juu ya mambo ya muungano na siasa, hufanya hivyo kama kiongozi wa CUF ndiyo maana hutumia jukwaa la kisiasa kuzungumza na wafuasi pamoja na wanachama wake.
“Rais wa Zanzibar ndiye msemaji wa Serikali na kiongozi mkuu, lakini Makamu wa Kwanza anapozungumza katika jukwaa na wafuasi wake, hutoa msimamo wa chama chake kama kiongozi wa juu,” alisema Hamad.
Maelezo hayo ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, yamekuja kufuatia tofauti ya kimtazamo na kimsimamo iliyojitokeza kuhusu ni nani mwenye mamlaka ya kuizungumzia Zanzibar.
Akizungumzia tathmini yake ya miaka mitatu ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), Hamad alisema kimsingi imefanikiwa kudumisha amani na kuondoa mivutano ya kisiasa na malumbano yaliyochangia kurudisha nyuma maendeleo ya Zanzibar.
Hata hivyo, alisema muundo wa SUK unahitaji kuangaliwa upya kwa ngazi ya watendaji na viongozi wa kisiasa ili kuleta taswira ya umoja wa kitaifa.
Mawaziri na manaibu wake wanafanya kazi kwa ushirikiano, lakini watendaji wakuu wa SUK bado wameshindwa kutekeleza majukumu yao na kuendeleza baadhi ya vitendo vinavyowanyima haki wananchi.
Alisema haikuwa mwafaka muundo SUK kuhusisha mawaziri na manaibu wake bila ya kuangalia nafasi nyingine za watendaji wakuu wa Serikali wakati wa marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Alisema pamoja na rais kuzungumzia mwelekeo wa kuimarika na kukua kwa
uchumi wa Zanzibar bado hali ya vipato kwa wananchi wa kawaida ni duni kutokana na kuanguka kwa sekta ya viwanda na kuzorota kwa uzalishaji wa ndani.

Hamad alisema sekta za uwekezaji, viwanda, mifugo na uvuvi lazima zipewe kipaumbele ili lengo la kuwapatia maisha bora wananchi lifanikiwe.

SOURCE: MWANANCHI