Saturday 9 November 2013

Bosi wa zamani TBS kizimbani kwa ufisadi

8th November 2013
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege
Aliyekuwa  Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege, jana alifikishwa  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka mawili ikiwamo matumizi mabaya ya madaraka kwa kutoa asilimia 50 ya punguzo la ada ya utawala kwa Kampuni mbili na kulisababishia shirika hilo hasara ya Dola 42,543 za Marekani (Sh. 68,068,800).

Kampuni hizo ni, Jaffar Mohamed Ali Garage na Quality Motors za jijini Dar es Salaam.

mshtakiwa huyo  alifikishwa mahakamani hapo juzi   na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Ausustina Mmbando.

Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Janeth Machuya, alidai kwamba kati ya Machi 28 mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, katika ofisi za TBS iliyopo wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu Ekerege alitumia madaraka yake vibaya.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo alitumia madaraka yake vibaya kwa kutoa punguzo la asilimia 50 ya ada ya utawala kwa kampuni hizo bila idhini ya baraza la utendaji la TBS kinyume cha sheria namba 2 kifungu kidogo cha (3) ya TBS ya mwaka 2005.

Ilidaiwa kuwa kitendo hicho kiliziongezea kampuni hizo faida ya Dola 42,543 za Kimarekani sawa na (kwa wakati huo) Sh. Milioni 68,068,800.

 Upande huo wa Jamhuri ulidai katika shitaka la pili kuwa katika tarehe na mahali pa tukio la kwanza, mshtakiwa alilisababishia shirika kupata hasara ya fedha hizo.

Mshtakiwa huyo alikana mashitaka hayo na upande wa Jamhuri kudai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na haukuwa pingamizi la kutoa dhamana dhidi ya mshtakiwa.

Hakimu Mmbando alimtaka mshtakiwa huyo kuwa na wadhamini wawili wanaotoka kwenye taasisi za kuaminika watakaosaini hati ya Sh. milioni 35 kila mmoja.

Mshtakiwa alitimiza masharti hayo ya dhamana na yuko nje hadi Desemba 12, mwaka huu atakaposomewa maelezo ya awali.

Mei 18, mwaka 2012, Ekerege alisimamishwa kazi kutokana na tuhuma za utendaji kazi mbaya wa shirika hilo na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 30.

Uamuzi huo ulifikiwa baada ya taarifa ya CAG ya ukaguzi wa hesabu za shirika hilo na kujadiliwa katika Bunge kisha kubainika kuwa ukaguzi uliofanywa na wakala wa TBS uliisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 30.
CHANZO: NIPASHE