Friday 25 October 2013

Wananchi waasi

25th October 2013
 Waua mgambo, wapiga risasi kigogo wa polisi 
Ni kupinga kulipa ushuru wa mazao yao

Mkuu wa Kituo cha Polisi Kilindi, Inspekta wa Polisi Lusekelo Edward, akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo baada ya kupigwa risasi mkono wa kulia na tumboni na kundi la watu wasiofahamika katika vurugu zilizotokea wilayani humo juzi.
Askari mgambo wa kijiji cha Lwande Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, Salum Mgonje, ameuawa kwa kucharangwa mapanga na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha wilayani hapa, Inspekta Lusekelo Edward, kujeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi baada ya kuibuka vurugu kubwa kijijini hapo.

Vurugu hizo zinadaiwa kusababishwa na kundi la watu ambao walikuwa wakipinga kitendo cha mwenzao kulipishwa ushuru wa ununuzi wa hiliki na serikali ya kijiji.
Kufuatia vurugu hizo, askari kadhaa wakiongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kilindi, Inspekta Edward, walikwenda katika kijiji hicho kwa lengo la kuwakamata watu waliohusika na mauaji ya askari mgambo, na ndipo alipopigwa risasi tumboni na mkononi.

Inspekta Edward akizungumza na NIPASHE  jana katika Hospitali ya Mkoa wa Tanga, Bombo, alikolazwa kwa matibabu, alisema alipigwa risasi alipofika katika Msikiti wa Answaar Suna uliopo kwenye eneo la Kibirashi wilayani Kilindi muda mfupi baada ya kuwatangazia watu hao ambao baadhi yao wanadaiwa kuwa waumini wa msikiti huo kuwa wako chini ya ulinzi.

Alisema chanzo cha tukio hilo ni kutokana na vurugu zilizotokea Oktoba 22, mwaka huu saa 6:00 mchana, baada ya waumini hao kutakiwa kulipa ushuru wa mazao waliyonunua, lakini waligoma na kusema kuwa ni kinyume cha sheria za dini yao.

Alisema kutokana na hali hiyo, watu hao walianzisha vurugu na kusababisha kifo cha mgambo huyo kwa kumshambulia kwa mapanga.
Hali hiyo iliwalazimisha polisi kuwakamata viongozi wao wawili na kusababisha wengine kuandamana kupinga hatua hiyo.

“Baada ya vurugu hizo ambazo zilisababisha kifo cha mgambo, ndipo tulipoamua kuwafuata waumini hawa kwenye msikiti wao, tulipofika pale walikuwa wakitoka na ndipo tulipowatangazia kuwa wapo chini ya ulinzi. Cha kushangaza walirudi na bunduki mkononi na kuanza kuwafyatulia askari risasi ovyo,” alisema Edward.

Alisema pamoja na kushambuliwa na waumini hao, hadi kufikia juzi watu watatu walikuwa wamekamatwa na kwamba msako unaendelea.

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Selemani Liwowa, alisema chanzo cha mapigano hayo ni mfanyabiashara mmoja ambaye jina lake halijafahamika, mkazi wa kijiji cha Lulago, Kata ya Lwande alipokwenda kijiji cha Lwande kununua hiliki na kukaidi kulipa ushuru wa mazao.

Alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo baada ya kukataa kulipa ushuru huo, ndipo askari mgambo (marehemu), alipokwenda kumtia msukosuko ili alipe kama taratibu na sheria za kijiji zinavyoelekeza.

Liwowa alisema baada ya kutokea mabishano makubwa baina ya mgambo na wafanyabiashara, ndipo wenzake walipoingilia suala hilo kwa kuanza kumshambulia kwa mapanga mgambo huyo hadi kusababisha kifo chake.

Aliongeza kuwa taarifa za mauaji ya mgambo zilipofika kituo cha polisi, ilimlazimu Mkuu wa Kituo kuongoza kikosi cha askari kilichokwenda kijiji cha Lwande kwa ajili ya kuwasaka waliohusika na mauaji hayo na ndipo lilipojitokeza kundi la watu wenye silaha na kuanzisha mapigano dhidi ya askari hao.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Juma Ndaki, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha vurugu hizo.

Kamanda Ndaki alisema kundi hilo lilianzisha vurugu baada ya kuona wenzao wamekamatwa na kukimbilia msituni na kwamba msako mkali unaendelea ili kuwatia nguvuni.

“Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constatine Massawe, yupo eneo la tukio kwa ajili ya kuona hali halisi ilivyo na operesheni maalum ya kuwasaka watu hao imeanza kutekelezwa,” alisema Kamanda Ndaki.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo, Dk. Jumanne Karia, alisema majeruhi huyo, Mkuu wa Kituo cha Polisi alipokelewa hospitalini hapo juzi saa 10:30 usiku akitokea wilayani Kilindi.

Dk. Kariya alisema hali yake kwa sasa inaanza kuimarika na kwamba utaratibu wa kumwondoa risasi moja iliyopo tumboni unaendelea.

Tukio hilo limetokea Kilindi wakati kukiwa na taarifa za tukio linalofanana na hilo kutokea katika Wilaya ya Lushoto ambako Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai wilayani humo (OCCID), Ufoo Maanga, alicharangwa mapanga na wananchi baada ya askari kwenda kumkamata mtuhumiwa wa mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Viti, Kata ya Shume wilayani Lushoto.
CHANZO: NIPASHE