Sunday 13 October 2013

Tanzania kamwe isikurupuke kujitoa ICC

Rais Jakaya Kikwete PHOTO|MAKTABA 


Posted  Jumapili,Oktoba13  2013  saa 12:15 PM
Kwa ufupi
Akitoa mhadhara nchini Afrika Kusini, kiongozi huyo mstaafu aliyeiongoza UN kati ya 1996 na 2006 na ambaye ni raia wa Ghana alisema ni viongozi wachache tu wanaoipiga vita ICC na kuonya kuwa, kujiondoa katika mahakama hiyo watakuwa wanalinda masilahi yao binafsi na si ya Waafrika wote.


Katika nyakati tofauti wiki hii zimesikika sauti za watu wawili mashuhuri barani Afrika zikiwahadharisha viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), kuhusu dhamira yao ya kuzitoa nchi zao katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), iliyoko The Hague, Uholanzi kwa madai kwamba mahakama hiyo inawadhalilisha na kuwalenga tu viongozi wa bara hilo.
Sauti hizo zimekuja wakati mwafaka, kwani wakati zikitoka, mawaziri wa nchi za nje wa nchi wanachama wa AU walikuwa wakikutana mjini Addis Ababa, Ethiopia kutayarisha ajenda za kikao cha wakuu wa nchi hizo kilichofanyika nchini humo jana. Ajenda maalumu ya kikao cha wakuu hao wa nchi ilikuwa kujadili uwezekano wa nchi hizo kujitoa ICC iwapo kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na makamu wake, William Ruto wanaokabiliwa na mashtaka ya uhalifu dhidi ya binadamu katika mahakama hiyo zisingefutwa au kuhamishiwa katika mahakama za Kenya.
Sauti ya kwanza kusikika ikiwaonya wakuu hao wa nchi wanachama wa AU dhidi ya kujitoa ICC, ilikuwa ya Katibu Mkuu mstaafu wa Umoja wa Mataifa (UN), Kofi Annan ambaye alisema itakuwa alama ya aibu kwa Bara la Afrika iwapo nchi hizo zitajitoa katika Mkataba wa Roma ambao uliunda mahakama hiyo mwaka 2002 na kusema iwapo watachukua hatua hiyo watakuwa wanajilinda wenyewe, huku waathirika wa uhalifu dhidi ya binadamu wakikosa wa kuwatetea.
Akitoa mhadhara nchini Afrika Kusini, kiongozi huyo mstaafu aliyeiongoza UN kati ya 1996 na 2006 na ambaye ni raia wa Ghana alisema ni viongozi wachache tu wanaoipiga vita ICC na kuonya kuwa, kujiondoa katika mahakama hiyo watakuwa wanalinda masilahi yao binafsi na si ya Waafrika wote.
Alisema njama za viongozi hao kutaka kujiondoa ICC ni ishara dhahiri kwamba Waafrika wana desturi ya kutoheshimu sheria, huku akisema viongozi wanaokabiliwa na mashtaka katika ICC walipelekwa huko kama watu binafsi na si Bara zima la Afrika kama inavyopotoshwa makusudi.
Sauti ya pili iliyosikika ilikuwa ya Jaji Stephen Bwana, raia wa Tanzania ambaye ameteuliwa majuzi kuwa jaji wa ICC, ambaye amesema viongozi wa nchi za Afrika wanaotaka kujitoa kwenye mahakama hiyo wana lengo la kuficha uovu uliopo katika nchi zao, kwani baadhi yao wanajifanya miungu watu. Jaji huyo alisema hayo juzi baada ya kuapishwa kuwa jaji wa ICC atakayesimamia kesi za uhalifu dhidi ya binadamu nchini Cambodia. Kabla ya kuteuliwa na UN, Jaji Bwana alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani hapa nchini.
Jaji huyo alisema nchi za Afrika zikijiondoa ICC ni kukubali udhaifu wetu na kuficha madudu yetu. Aliwashauri viongozi makini wa Afrika wasijiondoe, kwani sababu zilizowafanya wajiunge na ICC, ambayo alisema inatimiza wajibu wake bado zipo. Alikanusha vikali madai kwamba mahakama hiyo inawalenga viongozi wa Afrika pekee.
Tumetumia muda mrefu makusudi ili Serikali ya Rais Jakaya Kikwete iweze kupata ujumbe kutoka katika sauti za Waafrika hao wawili wenye utumishi uliotukuka. Sauti hizo zinashauri nchi za Afrika ziendelee kushirikiana na ICC na kuheshimu Mkataba wa Roma. Tunadhani kuwa, pengine kitu ambacho sauti hizo zinasita kusema ni kwamba nchi zitakazojitoa zitatengwa na jumuiya ya kimataifa.

SOURCE: BBC