Sunday 13 October 2013

Sinema ya mtandao wa biashara ya ukahaba-2


Picha ya kuchorwa ikionyesha jinsi biashara ya ukahaba inavyofanyika 
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Kwa ufupi
Nilishuhudia wasichana zaidi ya 35 wakitiwa mbaroni usiku wa Septemba 27 karibu na Baa ya Kimboka, lakini nusu saa baadaye kundi la wasichana wengine nikaliona likiwa limejipanga kuendelea na kazi.



Sehemu ya kwanza tuliona jinsi biashara inavyoendeshwa katika madanguro, leo simulizi inaendelea kuuelezea mtandao wake na jinsi watu wengine wanavyoitumia kama fursa ya kujinufaisha.
Katika sehemu ya kwanza nilisimulia wanaume ambao huonekana nje katika nyumba hizo wakinywa pombe za aina mbalimbali mchana kutwa.
Swali la kwanza nililojiuliza inakuaje mwanamume mzima anakaa katika vibanda na kunywa pombe mchana kutwa. Je anapata wapi pesa za kunununulia pombe au kuitunza familia yake?
Jibu nililopata ni kuwa wanaume hawa wengi ni madalali, ambao huwatafutia wasichana wateja pia huwatafutia wasichana wazuri wateja wa kiume.
Yaani hawa wanaume wanaweza kuingia mkataba na wanawake au wasichana wa kuwatafutia wanaume, na wao hupata kitu kidogo na hapa ndiyo hupata pesa za kunywa pombe.
Pia mwanamume anapokuja na kutaka mwanamke mzuri na mwenye usalama huwatumia madalali hawa. Wanasema hufanya hivi kujihakikishia usalama kwa kuwa wanawake wengine huwaibia wateja wao na ikitokea hivyo basi mteja humfuata dalali ambaye humsaidia kuvipata vitu vyake, kwa kuwa wao wanawajua wasichana wote wanaofanya biashara hiyo.
Mwanamke mmoja anayejiuza katika maeneo ya Buguruni Madenge, anasema wanaume hawa ni kiungo muhimu katika biashara hiyo hasa wakati wa mchana.
“Wanaume wengi huwa wanahitaji usalama zaidi wakati wa mchana kwa sababu ni lazima muingie ndani, sasa huwa wanaogopa labda tunaweza kuwabadilikia ndiyo maana huwa wanawatumia hawa ili wawe na uhakika,” anasema mwanamke huyo.
Anasema madalali wameingia katika biashara hiyo baada ya kukithiri vitendo vya kuwasingizia wateja, ambavyo hufanywa na makahaba kama vile kuwasingizia hawajawalipa hata kabla ya kufanya tendo lenyewe.
Anaongeza kuwa wakati wa usiku biashara hiyo inaweza kufanyika ‘chapchap’ hata katika vichochoro au kwenye gari lakini mchana ni lazima watafute faragha.
Aidha, anasema usipokuwa na uhusiano mzuri nao wanaweza kukuharibia kwa mteja wako, pale watakapokukuta naye kwa kumwambia maneno mabaya ili akuache amchukue mtu wanayemtaka wao.
Buguruni usiku

Mitaa hii hasa karibu na Barabara ya Mandela na Uhuru, wanawake hawa wanaonekana pembeni wakiwa wamejipanga kila mmoja kwa ‘pozi’ lake.
Tofauti na wale wanaojiuza katika ‘Club za Usiku’ na makasino ambao huvalia nadhifu na nusu utupu, hawa huvalia kawaida, wengine chini wamejifunga vitenge au khanga.
Wasichana wa chini ya miaka 15 na wanawake wenye zaidi ya miaka 35 wakiwa na nywele zisizo na matunzo na mavazi yasiyovutia, wanaonekana katika barabara hizi wakijiuza.
Nyumba za kulala wageni katika mitaa hii ambazo zipo mpaka zenye vyumba vitatu zinafurika, siyo wageni wa kulala bali wale wa ‘chapchap’ na wengine wanaonekana kwenye foleni wakisubiri wengine watoke ili na wao waingie.
Wamiliki wa nyumba hizo za kulala wageni huwatoza kiasi cha Sh2,000 kwa muda wa dakika kumi, zikiisha mgeni hugongewa atoke au aongoze pesa nyingine ili aendelee kwa dakika kumi zaidi.
Pia simulizi ya leo inaelezea upande mwingine wa biashara hii, kwa wale ambao wanajitegemea kwa kupanga katika makazi ya kawaida au nyumba za kulala wageni.
Siyo kuwa wanawake wote wanaojiuza Buguruni wanaishi kwenye madanguro, wengine wamepanga katika makazi ya kawaida na wengine wanaishi katika nyumba za kulala wageni.
Wenye nyumba wanasema siyo rahisi kujua anayekuja kupanga kama anafanya biashara hiyo au la, lakini pia wanasema si rahisi kuthibitsha hilo kwa kuwa hawawaleti wateja wao katika nyumba walizopanga.
Mmiliki mmoja wa nyumba maeneo ya Buguruni kwa Mnyamani (Jina tunalihifadhi), anasema siyo rahisi kujua kazi anayofanya mpangaji wako na hata hivyo anachoangalia ni pesa yake ya pango tu.
“Kama mtu anafanya biashara hiyo na hawaleti wateja wake nyumbani kwangu, mimi nina sababu gani ya kukataa kodi yake wakati mimi ninachotaka ni mpangaji tu,” anasema mwanamke huyo.
Hata hivyo, wapo wanaokerwa na tabia za wenzao wanaowapangisha wanawake wanaojiuza, wakisema kuwa wanashusha hadhi ya maeneo wanayoishi.
Wengine wanaichukulia biashara hii kama fursa ya kujinufaisha kwa kuwapangisha huku wakiwapa sharti la kulipa kodi kwa siku, kitu ambacho wanasema kinalipa tofauti na yule anayelipia pango kwa mwezi.

“Wasichana hawa kwa kuwa wengi hawana uhakika wa maisha yao, hupendelea nyumba za kulipia pango kila siku, huwa tunawatoza Sh3,000 mpaka Sh4,000 kwa siku, hii inatulipa kuliko mpangaji anayetaka akulipe kodi ya mwezi ambayo haizidi elfu ishirini,” anasema mwanamume mmoja anayemiliki nyumba katika eneo la Buguruni Madenge.
Aidha, anasema hii inawaondolea adha ya kusumbuana na wapangaji wanaolipia kodi ya mwezi, kwani huwa hawana uhakika ukilinganisha na wapangaji wa aina hii.
Zainab Zubeir anasema kukithiri kwa wanawake wanaojiuza katika maeneo wanayoishi, kumeshusha na kuwatia doa wanawake wote wa eneo hilo.
“Mimi leo hii ninaona aibu kumwambia mtu ninatokea Buguruni kwa sababu ukimtajia mtu hivyo moja kwa moja anakuhusisha na biashara ya ukahaba, natamani ningekuwa na uwezo wa kuwaondoa watu hawa huku,” anasema Zainab.
Hata hivyo mara kwa mara serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuwakamata na kuwaondoa wanawake hawa katika eneo hili, kutokana na kuwa na mtandao mkubwa juhudi hizo zimeshindwa kuzaa matunda.
Nilishuhudia wasichana zaidi ya 35 wakitiwa mbaroni usiku wa Septemba 27 karibu na Baa ya Kimboka, lakini nusu saa baadaye kundi la wasichana wengine nikaliona likiwa limejipanga kuendelea na kazi.

CHANZO: MWANANCHI