Sunday, 13 October 2013

MAISHA KAMILI YA MWAL. NYERERE KISIASA, KIIMANI NA KIFAMILIA

Mwalimu Nyerere alianza safari ya maisha Magomeni

Nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Magomeni ambayo kwa sasa ni makumbusho ya Taifa 
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi

Posted  Oktoba12  2013  saa 14:40 PM
Kwa ufupi
Enzi hizo Magomeni ndiyo ilikuwa kama Masaki. Mwalimu Nyerere alimwomba rafiki yake Mustafa Songambele amtafutie kiwanja katika maeneo hayo, naye akampatia hicho ambacho sasa ipo nyumba ambayo imegeuzwa Makumbusho ya Taifa.


Dar es Salaam. Wakati Taifa linaadhimisha miaka 13 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, pia anakumbukwa kwa namna alivyoona umuhimu wa kununua kiwanja na kujenga nyumba yake mwenyewe, eneo la Magomeni mkoani Dar es Salaam.
Enzi hizo Magomeni ndiyo ilikuwa kama Masaki. Mwalimu Nyerere alimwomba rafiki yake Mustafa Songambele amtafutie kiwanja katika maeneo hayo, naye akampatia hicho ambacho sasa ipo nyumba ambayo imegeuzwa Makumbusho ya Taifa.
Mhifadhi Malikale anayesimamia nyumba hiyo, Emmanuel Katoroki anasema si serikali iliyoamua kuifanya nyumba hii kuwa makumbusho bali Mwalimu Nyerere mwenyewe, ambaye alitaka Watanzania wajue ilipotoka historia yake kisiasa.
Katoroki anasimulia kuwa Mwalimu Nyerere baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, alitafuta sehemu ya usalama na ndipo rafiki yake alipomtafutia kiwanja hicho kilichopo Magomeni, Mtaa wa Ifunda.
“Mwalimu alikinunua kiwanja hiki mwaka 1957. Hii ilikuwa ni baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuwa Waziri Mkuu na wakati ule alihitaji ulinzi kwa kuishi katika mazingira salama, kwa kuwa Magomeni enzi zile ndiyo ilikuwa kama Masaki sasa hivi, akanunua na kuanza ujenzi,” anasema Katoroki.
Ulinzi wake
Katoroki anasema kwa wakati ule ulinzi ulikuwa mdogo hivyo kwa mtu anayeanza kuchipukia kisiasa tena anayetajwa kuweza kushika nafasi kubwa katika nchi, alihitaji kujilinda kwa kuwa lolote lingeweza kutokea.
Aidha, Katoroki anasema historia ya kisiasa ya Mwalimu ilianza wakati akiishi katika nyumba hii na baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwani baada ya hapo alikwenda kuishi katika nyumba ya serikali Sea View na baadaye Ikulu.
“Pia ni nyumba ya kihistoria kwani aliijenga kwa kiinua mgongo chake baada ya kuacha ualimu pale Shule ya Sekondari ya Pugu. Baada ya kuwepo tetesi na pengine mwenyewe alikuwa na taarifa kamili, aliamua kuachana na ualimu, “ anasema Katoroki.
“Ninasema historia yake kisiasa ilianzia katika nyumba hii kwani aliamkia katika nyumba hii kwenda kuapishwa kuwa Waziri Mkuu na kuanza rasmi shughuli za kisiasa na ukombozi wa bara la Afrika,” anasema.
Kingine ambacho kinaifanya nyumba hii kuwa ya kihistoria ni pamoja na kuwa alijinyima wakati akijenga, aliishi kwa muda wa miezi minane tu kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika Januari 1, 1960.
Katoroki anasema pamoja na nyumba hiyo kuwa ya pekee, Mwalimu aliwahi kuiuza baada ya kutokea mgogoro katika familia yake iliyokuwa ikiiogombea.


“Inavyoonekana Mwalimu baada ya kuwa Waziri Mkuu aliitelekeza nyumba hii na ndugu wakaanza kuigombania. Mwenyewe baada ya kupata taarifa hizo aliamua kuumaliza ugomvi wa ndugu kwa kuiuza,” anasema Katoroki.
Hata hivyo historia nyingine iliandikwa mwaka 1973 wakati Jumuiya ya Wafanyakazi (JUWATA), ikitimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ambayo Mwalimu Nyerere alialikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo na Jumuiya hiyo iliamzawadia nyumba.
“Juwata walimwambia Mwalimu tunataka kukupa zawadi, alipoifungua alikuta ni hati ya nyumba yake ambayo aliwahi kumuuzia mtu mwingine,” anasema Katoroki.
Viongozi wa Juwata walimnunulia Mwalimu Nyumba hiyo kutoka kwa mtu aliyemuuzia kwa Sh 35,000 na kumrudishia mwenyewe kwa njia ya zawadi.
Aliwashukuru kwa kuirudisha mikononi mwake. Hata hivyo alisema asingependa ibaki kwenye mikono yake kwani inaweza kurudisha matatizo aliyoyakwepa na hivyo akaamua kuitoa kwa serikali ili iifanye kuwa Nyumba ya Makumbusho.
Serikali kwa muda mrefu iliitelekeza nyumba hii na hivyo kuanza kuharibika na vyombo kuanza kupotea. Hata hivyo, Wizara ya Utamaduni ilipewa jukumu la kuisimamia nyumba hii chini ya Idara ya Mambo ya Kale na mwaka 2002 ilikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Idara ya Mambo ya Kale.
Vitu vyake
Pamoja na kuwa vitu vingi vya Mwalimu vilipotea baada ya Mwalimu Nyerere na familia yake, ndani ya nyumba hiyo vipo vitanda vya familia kikiwamo kile alichokilalia mwalimu mwenyewe kabla ya kuhama.
Vitu vingine vilivyopo ni kabati la jikoni, kabati la kuhifadhia fedha (kibubu), pasi ya mkaa, mtungi wa kuhifadhia maji, redio ya mbao, makochi, cherehani na vyombo vya jikoni.
Pamoja na vyombo ndani ya nyumba hiyo, kuna noti za pesa zilizokuwa zikitumika enzi za utawala wake. Pia vipo vitabu alivyowahi kuandika kama vile; Ujamaa ni Imani, Maendeleo ni Kazi, ‘Education to Self Relience’, Tujisahihishe, Tanu na Raia, ‘Our Leadership and Destiny of Tanzania’ na vingine vingi.
Vitu vingi vilivyopo ndani ya nyumba hiyo vilipatikana kutoka kwa Mzee Omary (Aliyekuwa baba mlezi wa Mwalimu Nyerere), ambaye inadaiwa kuwa baada ya kuona nyumba haina mwelekeo alivichukua na kwenda navyo Dodoma ambako anaishi mpaka sasa.
“Mzee huyu ametunza vitu vingi vya Mwalimu na kama unavyoona humu ndani, hivi vyote tumevipata kwake, tunasikia kuna vingine walichukua ndugu na sasa wameviuza kwa watu wa makumbusho binafsi,” anasema Katoroki.

 “Nia yetu ni kupata kila kitu ambacho kilikuwamo humu ndani, vingi viliuzwa kwenye makumbusho binafsi na wao wanaviuza kwa bei za juu hivyo si rahisi kuvipata,” anasema Katoroki.


Nyerere alikuwa Mkatoliki haswaSanamu ya Bikira Maria na Rozali vilivyokuwa vikitumiwa na Mwalimu Nyerere wakati wa salama. picha na Maktaba 
Na Maimuna Kubegeya, Mwananchi

Kwa ufupi

“Tangu atimize miaka 51 babu amekuwa akifanya ibada za asubuhi na jioni hadi alipokutwa na umauti” anasema Julius Makongoro Nyerere mjukuu wa Mwalimu Nyerere.


Dar es Salaam. Moja ya urithi mkuu aliouacha Mwalimu Nyerere kwenye familia yake ni kumcha Mungu, ambapo watu wake wa karibu wanasema alikuwa Mkristo wa kweli ambaye alikuwa akiishi maisha ya kumcha Mungu.
“Tangu atimize miaka 51 babu amekuwa akifanya ibada za asubuhi na jioni hadi alipokutwa na umauti” anasema Julius Makongoro Nyerere mjukuu wa Mwalimu Nyerere.
Anasema wakati wa uhai wake, alikuwa yuko tayari kukupa adhabu yeyote ile ikiwa tu utakosa kufanya ibada.
“Ilifikia kipindi tulikuwa tukipewa adhabu ya kunyimwa chakula kwa kosa la kushindwa kusali,” anasema.
Kwenye familia yao ilikuwa ni kawaida kusali novena ambayo kwa kawaida husaliwa kila baada ya saa nane.
“Hivyo ikitokea sala hiyo ikaangukia usiku wa manane, babu alikuwa akituamsha nyumba nzima kwa ajili ya kusali,” anasema Julius.
Monsinyori Deogratias Mbiku mlezi na paroko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni miongoni mwa watu wanaomfahamu Mwalimu Nyerere.
“Kwa mara ya kwanza nilikutana na Mwalimu mwaka 1963, pale Nyegezi, Mwanza, alipokuja kumtembelea Fideric Mula aliyesoma naye huko nchini Scotland.
“Nyerere hakuwa na makuu vaa yake, ongea yake hata ushiriki wake katika masuala mbalimbali ya kijamii, ulikuwa ni wa kawaida kabisa”.
Kila mahali alipokwenda alikuwa akiomba apelekwe kanisani na hakusita kuwaambia walinzi wake; “Nipelekeni kanisani mimi ni Mkristu.” Alikuwa hafichi hilo.
Mbiku anasema ratiba ya Nyerere siku zote ilianza kwa sala. “Na siyo tu alikuwa akisali, bali alikuwa pia akitoa “comments” zake kuhusiana na ibada,” anasema Mbiku.
Anasema pia alikuwa muwazi katika kueleza kama ameridhishwa au hakuridhishwa, kwa kuwa sehemu nyingi kuna namna mbalimbali za kufanya ibada.

“Alikuwa akifuatilia ibada na siyo tu kusali kwa kutimiza wajibu,” anasema na kuongeza:
“Kwa mfano alienda kanisa moja, akakuta wanaimba sana, yaani wanatumia muda mwingi kuimba na kwa muda mfupi wanasali, Mwalimu hakusita kuwaambia kinachotakiwa ni kusali muda mrefu kila mtu apate muda wa kufanya toba na siyo kuimba kama kwenye tamasha.
“Halafu hii baba yetu kama kuna ‘tune’ ambayo watu wanaweza kudaka sawa, lakini hii ni sala ya bwana, tusali wote” alisisitiza na kuongeza kuwa kutoa huduma za kiroho katika Kanisa la Mtakatifu Petro kuanzia mwaka 1972 alikokuwa akisali Mwalimu.
Mbiku anasema Nyerere alikuwa ni zaidi ya muumini, kwani siku zote alikuwa mshauri mzuri wa masuala yanayohusiana na ibada, akilenga kuweka mazingira mazuri ya kumwabudu Mungu.
“Nilikuwa nikimshuhudia Mwalimu akija kusali kila siku kabla ya kwenda kazini kwake,” anasema.
Sababu hizi na nyingine nyingi zilifanya kiongozi huyu kuingia kwenye mchakato wa kutangazwa mwenye heri mara baada ya kifo chake.
Mbiku anasema mchakato huo si wa muda mfupi kwani una hatua kadha wa kadha. Hivyo katika hatua za awali uchunguzi hufanyika juu ya maisha yake.
Anasema hatua hiyo ya kwanza inaitwa mtumishi wa Mungu, halafu hatua pili ni kuangalia miujiza inayomhusisha huyo mtumishi wa Mungu. Hatua ya mwisho ni kumtangaza mwenye heri. Kwa kawaida mchakato huo huanza miaka mitano baada ya mhusika kufariki dunia.
Mbiku anasema mchango wa Mwalimu Nyerere umekuwa ukitambuliwa na watu wengi, hususani waliokuwepo katika Kanisa Katoliki.
“Kwa mfano mwaka 1994 nilikuwa Makamu Mkuu wa Chuo katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki huko nchini Kenya, kilichokuwa kikihudumia nchi nane za Afrika ya Mashariki.”
“Wakuu wa chuo kile walipendekeza Mwalimu Nyerere apewe shahada ya heshima ya Kanisa Katoliki, hivyo nikaagizwa kwenda kumpelekea taarifa.”
“Nilirudi nyumbani na nikamsubiri kule kanisani, baada ya kanisa nilimwambia kuwa nahitaji kuongea naye na hivyo akanikaribisha nyumbani kwake,” anasema.

Alipofika nyumbani kwake siku ya pili yake, alikaribishwa chai na kufanya maongezi.
“Nilimfikishia ujumbe nikimwambia kuwa, viongozi wa chuo wamemteua yeye kupokea shahada ya heshima,” anasema na kuongeza kuwa majibu ya Mwalimu Nyerere yalikuwa; “Asante sana kwa kunipa nafasi hiyo, lakini kwa sasa sitoweza kuhudhuria kwani kwa sasa hali ya nchi siyo nzuri, kuna matatizo fulani yanayohusiana na masuala ya muungano yameingia hivyo ninaumiza kichwa katika kuyatafutia ufumbuzi.
“Lengo langu hasa ni kuhakikisha muungano unasimama, nisingependa kuona muungano unakufa mimi nikiwa hai.”
Mbiku anasema baada ya Mwalimu Nyerere kuacha kupokea shahada hiyo, Kadinari Rugambwa alichaguliwa badala yake.
Jambo hili lilinifanya niwe naamka mapema kumuwahi na huo ndiyo ukawa utaratibu wa maisha yangu.

Nyerere alivyoishi na wajukuu

Wajukuu wa Mwalimu Nyerere wakiwa na baba yao mdogo, John Nyerere (katikati). Kulia ni Moringe Magige na kushoto ni Julius Makongoro. Picha na Julieth Kulangwa NyereNyerere(katikati) , Picha na Julieth Kulangwa.  

Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Kwa ufupi
Unapofika katika nyumba yake iliyopo jijini Dar es Salaam maeneo ya Msasani maarufu kwa Mwalimu Nyerere, kinachoyatofautisha maisha ndani ya nyumba hiyo na zile za Magomeni na Ilala ni mazingira nadhifu.


Si urithi wa mali, isipokuwa ni mapenzi kwa binadamu wenzake na hekima ambavyo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ameviacha katika vitabu, maandiko mbalimbali na kwa familia yake, tangu afariki dunia miaka 14 iliyopita.
Unapofika katika nyumba yake iliyopo jijini Dar es Salaam maeneo ya Msasani maarufu kwa Mwalimu Nyerere, kinachoyatofautisha maisha ndani ya nyumba hiyo na zile za Magomeni na Ilala ni mazingira nadhifu.
Wenyeji ndani ya nyumba hii kwa mwonekano na mazungumzo hawana tofauti na Watanzania wa kawaida, hawana majivuno na wanamkaribisha mgeni kama ndugu au jamaa waliyemfahamu miaka mingi.
Pamoja na kuwa nyumba ni kubwa na wenyeji ni wengi, lakini kwenye maegesho ya magari lipo gari moja tu. Mwonekano wa nje wa nyumba hii unaweza kukufanya ufikiri ndani kuna magari zaidi ya matatu tena ya kifahari.
Wanafamilia ni wakarimu sana, kwa kawaida ungetarajia kusikia wenyeji wakitumia maneno kama “Yes, No” na maneno mengine ya Kiingereza kwa kuwa hiki ni kitambulisho cha vijana waliopata elimu angalau ya sekondari, lakini hapa ni tofauti, wote wanazungumza Kiswahili na bahati mbaya wakichanganya huwa ni lugha ya Kizanaki.
Wajukuu wa Baba wa Taifa, Moringe Magige na Julius Makongoro wanasema huu ndiyo urithi ambao Baba wa Taifa aliwaachia ndugu zake wakisema kuwa walilelewa kuamini kuwa mali siyo kitu kuliko utu na ndivyo walivyo.
Maisha ya Mwalimu Nyerere kama babu
Wengi tunafahamu historia ya Baba wa Taifa hasa katika majukumu yake ya uongozi wa Tanzania na ukombozi wa bara la Afrika, lakini Moringe na Julius wanaturudisha nyumbani wakisimulia walivyomfahamu babu yao.
Moringe anasimulia akisema; “Kwanza mimi sikufahamu kwa jinsi gani babu alikuwa mtu muhimu katika nchi hii na bara la Afrika kwa ujumla, nilijua baada ya kufariki dunia na kuanza kusoma historia yake na kugundua vitu vingi alivyofanya,”
“Sikuiona tofauti yake na mababu wengine kwani shuleni nilisikia watu wakisimulia jinsi walivyoishi na babu zao na sikuona tofauti na babu yangu,” anasema Moringe.
Anasema Mwalimu Nyerere aliwapenda wajukuu zake, alipenda kufanya shughuli za shamba akiwa na wajukuu zake, hakutaka hata mmoja azembee kwenda shambani.
“Babu aliipenda familia yake, tumeishi na ndugu wengi kwa sababu hakutaka kukaa mbali na ndugu zake na kila mmoja alihakikisha anapata wasaa wa kukaa naye na kuzungumza naye, mfano alikuwa na utaratibu wa kula chakula cha jioni na sisi wajukuu zake,” anasema Moringe.

Aidha anasema kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akiwahimiza kuongeza juhudi shuleni hasa katika masomo ya Kiingereza na Hisabati.
“Babu alikuwa akifuatilia maendeleo yetu shuleni, kila mwisho wa muhula alikagua matokeo ya kila mmoja wetu na alikuwa akisisitiza zaidi masomo ya Kiingereza na Hesabu akisema hayo ndiyo ya msingi,” anasema Moringe.
Alikuwa anapenda kupiga makonzi
Kila mtu anakumbuka adhabu gani alikuwa anapewa na bibi au babu yake pale anapokosea, lakini Julius anatuambia kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akiwapiga makonzi wajukuu zake pale wanapokosea.
Julius anasema adhabu kubwa waliyokuwa wakipewa na babu yao ni kupigwa makonzi hata hivyo utaokoka tu kwa juhudi zako za kutoka mbio kwani ukisimama anaendelea kukupiga. “Babu alikuwa na tabia ya kutupiga makonzi hasa ukiwa mtundu au ukimpitia karibu wakati anacheza bao lazima atakupiga japo konzi moja,” anasema.
Pia anasema kamwe hatasahau siku moja alipomuomba babu yake akaangalie mkanda wa video mchana;” Nilimwambia babu tunaomba kuangalia mkanda kwa sababu Tv ilikuwa inakaa Maktaba, alinikubalia na kuniambia nenda ukawaite na wenzako unaotaka kuangalia nao. Basi nikaenda kuwaita tulivyofika alitufungia na kuanza kutupiga makonzi ,” anasema Julius.
Aidha anasema babu yao aliwapangia muda maalumu wa kuangalia televisheni pia aliwachagulia mikanda ya kutazama kwa kuwa alipenda wawe na maadili mema.
Vituko,utani wa babu na wajukuu zake
Pamoja na kuwapiga makonzi wajukuu zake lakini kuna wakati alikuwa akiketi chini na kufanya utani na kushuhudia vituko vya wajukuu zake.
Moringe anasema moja kati ya maswali ya utani waliokuwa wakimuuliza babu yao ni iwapo enzi za ujana wake alikuwa akifanya starehe za aina mbalimbali.
“Tulikuwa tunamuuliza babu hivi unajua kuogelea au kucheza muziki kwa sababu hatujawahi kukuona hata siku moja ukicheza, alijibu ‘siwezi’, tukawa tunamuuliza sasa wewe ujana wako ulikuwa unafanya nini, alisema ‘kusoma tu’, anasema Moringe.
Aidha wanasema utani mwingine kwa babu yao ilikuwa ni kuwa hajui kuendesha gari. Julius anasema “Tangu nimepata akili sijawahi kumuona akiendesha gari, nina wasiwasi alikuwa hajui kuendesha”.

Julius pia anasema hajawahi kumuona babu yake akiwa amevaa suti au kuchomekea huku akisema inawezekana zamani alikuwa analazimishwa kuvaa hivyo. “Sijawahi kumuona babu amevaa suti au amechomekea shati, hata hakupenda ndugu wavae suti hasa tukiwa Butiama, alipenda kuvaa ‘simple’.
Alisisitiza maadili
Moringe na Julius wanasema wanaamini babu yao alikuwa akilinda maadili kwa kutowaachia watazame televisheni ovyo na kuwahimiza kushiriki kanisani.
“Babu hakuwa na mchezo linapokuja suala la kanisani, yaani usipoenda kanisani ni ugomvi mkubwa anaweza hata kukufukuza usile naye chakula cha jioni,” anasema Moringe.
Wakizungumzia iwapo Baba wa Taifa angekuwa hai leo angebariki matumizi ya mitandao ya kijamii kama ‘facebook’ na ‘twitter’ kwa pamoja walisema asingepinga kwani alikuwa mpenda maendeleo.
“Watu wengi huwa wanazungumza wakisema kuwa babu alikuwa hataki watu waendelee kwa kutumia teknolojia, sio kweli, babu alikuwa anapenda maendeleo lakini aliheshimu utamaduni,” anasema Julius.
Akitolea mfano wa dada yao mmoja aliyekuwa akiishi Ulaya walisema, babu yao hakuwa na tatizo na mavazi yake lakini alimwonya kuwa ni lazima aangalie anavaa wapi.
“Mfano tukiwa hapa Msasani babu hakumkataza kuvaa nguo zake anazopenda, lakini tulipoenda Butiama alikuwa akimrudisha pale anapovaa nguo anazoona haziendani na utamaduni wa watu wa kule,” anasema Julius.
Anaongeza kuwa Mwalimu asingekuwa na tabu na mitandao hiyo au teknolojia yoyote isipokuwa pale itakapotumikwa visivyo kama wafanyavyo wengi.
“Ukiukwaji wa maadili unaotokana na teknolojia unawakwaza watu wengi, watu wanatumia ndivyo sivyo na hiki pengine kingemkera babu,” anasema Julius.
Siri ya kifimbo cha babu yao
Moringe na Julius wanasema wamesikia hadithi nyingi kuhusu kifimbo cha Mwalimu Nyerere alichokuwa akipenda kukibeba, wengine wamediriki kusema alizikwa nacho.

Julius anasema kwanza wanavyofahamu wao babu yao alikuwa nazo zaidi ya nne, nyingine alinunua mwenyewe na nyingine alipewa zawadi.
“Babu alikuwa na fimbo nyingi, alibeba yoyote anapotoka nyumbani, wakati mwingine aliweza kuisahau na kutuagiza tumpelekee nje kama ameshatoka,” anasema Julius.
Aidha Moringe anasema amewahi kusikia kuwa asili ya babu yao kutembea na fimbo hiyo ilitokana na nia yake ya kuacha kuvuta sigara. “Niliwahi kusikia babu alikuwa akivuta sigara, sasa alipotaka kuacha alipewa fimbo kama njia mbadala ya kushika kitu mkononi ili aweze kuacha,” anasema Moringe.
Wasifu wa Julius na Moringe
Julius Kambarage (28) ni mtoto wa Makongoro ambaye ni mtoto wa tano wa Mwalimu Nyerere na Moringe ni mtoto wa Magige ambaye ni mtoto wa tatu.
Hivi sasa Julius anafanya kazi katika Kampuni ya Uingizaji na Utoaji wa Mizigo (Clearing and Forwading) iitwayo Tesna Quality wakati Moringe ni Ofisa Uwekezaji katika Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF).


Mwalimu Nyerere alimfanya kila mmoja ajione muhimu

Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na mke wake.Picha na Maktaba 
Na Julieth Kulangwa, Mwananchi
Kwa ufupi
Mimi siku zote alikuwa akiniita ‘rafiki yangu’ kwa kuwa alinipa jina la rafiki yake kipenzi, hakuwahi kuniita kwa jina langu la Moringe hata siku moja


Oktoba 14 ya kila mwaka Watanzania hukumbuka siku ya huzuni, ambapo walimpoteza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia tarehe na mwezi huo, mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas nchini Uingereza alipokwenda kwa matibabu.
Madaktari walieleza kuwa kifo cha baba wa taifa kilitokana na ugonjwa wa saratani ya damu. Julius Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika huru na baadaye alikuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.
Mwalimu alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ambapo alikaa madarakani akiiongoza Tanzania kwa miaka zaidi ya 20.
Oktoba 14 ya kila mwaka imefanywa kuwa ya kitaifa ikitoa nafasi ya kumbuka, kutafakari aliyolitendea taifa, lakini zaidi kuenzi yote mema na mazuri kwa Tanzania aliyoipenda.
Tangu kufariki kwake mengi yamekuwa yakikumbukwa na kutajwa kama mfano na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo viongozi.
Ni wazi na hakuna anayeweza kupinga kuwa Mwalimu Nyerere ameacha mambo mengi mazuri ya kujivunia na mfano wa kuigwa na jamii ya Watanzania.
Historia hiyo ipo katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, elimu, uchumi hata utamaduni katika taifa la Tanzania linaloelezwa kuwa na makabila zaidi ya 120, hivyo pia kuwa na tamaduni tofauti kati ya kabila moja na nyingine, ingawa baadhi ya makabila hufanana mila na utamaduni wao kwenye baadhi ya mambo.
Katika makala haya leo, tunaangalia namna Mwalimu Julius Kambarage alivyoacha historia ya kipekee katika kuenzi utamaduni wa kabila lake na kuheshimu uhusiano katika familia na urafiki wake na watu wengine.
Ukweli wa hilo unadhihirishwa na jinsi Mwalimu alivyokuwa akitoa majina kwa watoto wake, wajukuu na jinsi alivyokuwa akiwaita kila mmoja kwa namna yake, akizingatia uasili na heshima kati yake na watu wengine.
Ndivyo ilivyo, Mwalimu aliwapa majina watoto wake akitaka kila mmoja awe na jina lenye maana kama siyo kwa familia, basi kwake binafsi.
Hapa mfano wa karibu ni namna alivyowapa majina watoto wake kwa kuwapa majina ya pili ambayo ni ya kiasili na kwa namna tofauti, huku kila jina likiwa na maana kwa familia na kwake.
Katika uhai wake, Mwalimu Nyerere alibahatika kupata watoto saba ambapo mbali na majina yaliyotokana na imani yake ya dini ya Kikristo, kila mmoja alimpa pia jina la kiasili ya Kizanaki, kabila alilotokea, ukoo wake au wa mkewe mama Maria Nyerere.

Akionyesha mfano wa kuthamini uafrika na asili yake Nyerere alimwita mtoto wake wa kwanza kwa jina la Burito au Andrew, mwingine alimwita Watiku (Anna), Magige(Emily), Nyerere (John), Makongoro (Charles) na Madaraka ambaye ni Godfrey.
Mmoja wa wajukuu zake aliyempa jina la Moringe anasema kuwa anaamini kila mtu katika familia ya mwalimu alipewa jina kwa sababu maalumu, kwani pamoja na kuwa majina mbalimbali, bado babu yao aliwaita kwa maana ya jina la kiasili.
Anatoa mfano wa baba yake yeye, (Mzee Magige) ambaye alipewa jina la baba wa Mama Maria Nyerere, hivyo Mwalimu alikuwa akimwita Magige ‘mkwe’.
“Babu alikuwa akimwita baba yangu kwa lugha ya Kizanaki ‘Tata Kyara’ akimaanisha baba mkwe, nimemsikia akimwita hivyo siku zote na hakuwahi kutumia jina lake la Magige au Emily.
Anasema hata yeye alipewa jina la Moringe ambalo ni la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Moringe Sokoine kwa sasa ni marehemu, ambaye alikuwa ni rafiki mkubwa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Mimi siku zote alikuwa akiniita ‘rafiki yangu’ kwa kuwa alinipa jina la rafiki yake kipenzi, hakuwahi kuniita kwa jina langu la Moringe hata siku moja,” anasema.
Anaongeza kuwa alifanya vivyo hivyo kwa ndugu wote akiwaita kutokana na asili ya majina yao na kwa kuwa wengi walikuwa na majina ya Kizanaki aliwaita kutokana na uhusiano au tafsiri ya majina hayo.
Moringe anasema kuwa Nyerere aliwalea watoto na wajukuu zake katika maisha yaliyolenga kuwaonyesha Watanzania kuwa kila mtu ni sawa kwa kuwa pamoja na kuwa na madaraka, hakuyatofautisha maisha yake na ya Watanzania wengi.
“Nchi hii matajiri ni wachache kuliko maskini, alitaka familia yake iishi maisha ya kawaida, yanayofanana na ya Watanzania wengi ingawa alikuwa na uwezo wa kuwafanya waishi kama wako peponi.
Hii ililenga kuonyesha kwamba alijali usawa na kutaka kila mmoja ajione muhimu katika nchi yake,” anasema Moringe.
Anabainisha kuwa Mwalimu hakutaka Watanzania wajione wanyonge kwa tabaka na walionacho na wasionacho na yeye alipinga hali hiyo kwa kuonyesha mfano.
“Isingekuwa na maana kwa babu kufanya mambo ambayo kwa Watanzania ni mageni, kama angefanya hivi pengine leo hii sisi kama familia au kama Watanzania tusingejivunia kupata mtu kama yeye,” anasema Moringe.

Anaongeza kuwa unapotaka kusisitiza jambo fulani lifanyike, mwenyewe unatakiwa kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano na hiki ndicho alichokuwa akifanya Baba wa Taifa.
“Kama angejihusisha na biashara nyingine wakati akiwa kiongozi wa nchi, maana yake angetengeneza mwanya kwa viongozi wengine kufuata nyayo zake na hii ingeweza kutengeneza mianya ya rushwa na ukiukwaji wa maadili,” anasema Moringe. Akizungumzia yeye kutaka kujiingiza katika siasa anasema atafuata nyayo za babu yake ambaye kabla alitumikia taaluma yake na baadaye ndipo akajiingiza huko.
“Ninapenda kufuata nyayo za babu, alisoma, akawa mwalimu na baadaye ndiyo akajiingiza katika siasa, nami nitafanya hivyo, sasa hivi ni wakati wangu wa kuitumikia taaluma yangu mpaka pale nitakaporidhika ndipo nitaingia kwenye siasa,” anasema Moringe.
CHANZO: MWANANCHI