Thursday 31 October 2013

‘Luteni Rajab aliniomba nimwombee’


 
Na Aidan Mhando, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Oktoba31  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni kauli ya aliyekuwa mchumba wa marehemu Luteni Rajabu, aliyeuawa nchini DRC .


Dar es Salaam. Mchumba wa askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliyeuawa kwa kupigwa risasi akiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Luteni Asia Hussein aliyekuwa naye kabla ya kuuawa mchumba wake amesema, marehemu alimwomba amwombee arudi salama kutoka kwenye mapigano.

Pia, alisema kauli hiyo ndiyo ya mwisho kuisikia kutoka kinywani mwa mchumba wake huyo aliitoa baada ya kutolewa amri ya kijeshi kwamba anatakiwa kwenda kuwasaidia wenzake waliokuwa kwenye mapigano na askari wa waasi wa M23.
Askari huyo wa(JWTZ), Luteni Rajab Ahmed Mlima, aliuawa akiwa kwenye uwanja wa mapambano na vikosi vya askari wa waasi wa M23 katika milima ya Gavana, karibu na Goma, DRC wakati akitekeleza jukumu la ulinzi wa amani.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili jana nyumbani kwake, Luteni Asia alisema, “Ninachokumbuka walitakiwa kwenda kuwasaidia wenzao waliokuwa kwenye mapigano kwa muda mrefu, tayari walikuwa wamezidiwa nguvu na askari wa waasi wa M23, ukweli hali ilikuwa mbaya na mimi nilimkataza asiende kwa kuhofia usalama wake,” alisema Luteni Asia huku akibubujikwa machozi.
Alisema wakati akimsihi asiende alimjibu kwamba ni lazima aende kuwasaidia wenzao, kwani kazi waliyotumwa kuifanya ni pamoja na hiyo hivyo asingeweza kuacha kwenda.
Aidha, Luteni Hussein alibainisha kuwa baada ya kwenda kutoa msaada na kufanikiwa kuwadhibiti waasi, muda mfupi baadaye alipata taarifa kuwa Luteni Mlima amefariki kwa kupigwa risasi jambo lililomshtua kiasi cha kuishiwa nguvu kabisa.
Alisema kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa, yeye anamwombea huko aliko apumzike kwa amani kwani amefariki akiwa anawatetea wananchi wa DRC na kuiwakilisha nchi yake.
Mipango ya harusi
Akielezea mipango yao ya harusi, Luteni Asia alisema Desemba 28, mwaka huu walipanga kufunga ndoa na kwamba taratibu zote zilikuwa zimekamilika ikiwa pamoja kutolewa mahari.
“Kwa kweli jambo linalo niuma sana na siwezi kusahau ni kwamba, tulikuwa tumebakiza muda mfupi tufunge ndoa na kila kitu kilikuwa kimeshakamilika hadi ukumbi wa kufanyia sherehe ya harusi yetu tulishaulipia,” alisema Luteni Hussein huku akibubujikwa na machozi.
Kaka wa marehemu
Akizungumza na gazeti hili, kaka wa marehemu Dk Aziz Mlima alisema ndugu yao atazikwa leo Alhamisi saa 10 kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

JWTZ yatoa tamko
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Erick Komba alisema mwili wa Luteni Rajab Ahmed Mlima ulitarajiwa kuingia jana saa moja jioni na kuhifadhiwa kwenye kambi ya Jeshi Lugalo. Alisema taratibu za kuuaga mwili huo zitafanyika kijeshi kwenye kambi hiyo kuanzia leo saa tatu asubuhi na mazishi yatafanyika kwenye makaburi ya Kisutu Dar es Salaam.

SOURCE: MWANANCHI