Tuesday 29 October 2013

Kinana azima mapinduzi UVCCM


Mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Hamisi Juma (katikati) Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (kulia) wakiimba nyimbo ya chama hicho kabla ya kuanza kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo kilichofanyika White House, mjini Dodoma jana. Kushoto ni Katibu wa UVCCM, Sixtus Mapunda. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumanne,Oktoba29  2013  saa 10:23 AM
Kwa ufupi
Hii ni mara ya pili kwa Katibu Mkuu huyo kumwokoa Sadifa, kwani Septemba mwaka huu, alilazimika kuingilia kati mgogoro ambao uliibuka katika kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo Visiwani Zanzibar baada ya wajumbe kutaka kumwajibisha kwa madai kwamba alikiuka kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM.
 

Mwenyekiti Sadifa acheza sakakasi kukwepa kung’olewa, amteua hasimu wake kisiasa, Makonda na wengine watatu kuongoza 
Dodoma. Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alilazimika kuzima mapinduzi yaliyokuwa yamepangwa kuwang’oa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (UVCCM), Sadifa Juma Khamis na makamu wake, Mboni Muhita.
Jana Kinana akifungua mkutano wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo, aliweka bayana kuwa mkutano huo haukuwa kwa ajili ya “kuibomoa UVCCM, bali kuijenga”, kauli ambayo inatajwa kuwa iliwavunja nguvu wajumbe waliokuwa wamepanga kuanzisha harakati za kuwatoa madarakani viongozi hao.
Habari zaidi kutoka Dodoma zilisema kauli ya Kinana iliongeza nguvu harakati za kujinasua za Sadifa ambaye usiku wa kuamkia jana, alikesha akifanya vikao vya kuwaomba radhi wenyeviti wa UVCCM wa mikoa na baadaye wajumbe wote wa Baraza Kuu.
“Hatua hiyo nadhani imemsaidia sana maana wenzake ndani ya umoja huo hawaridhiki na jinsi mambo yanavyokwenda, pamoja na uongozi wake. Wanaona kama hakidhi standards (viwango) zao,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya mkutano huo.
Hii ni mara ya pili kwa Katibu Mkuu huyo kumwokoa Sadifa, kwani Septemba mwaka huu, alilazimika kuingilia kati mgogoro ambao uliibuka katika kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo Visiwani Zanzibar baada ya wajumbe kutaka kumwajibisha kwa madai kwamba alikiuka kanuni za uteuzi wa wakuu wa idara za UVCCM.
Pamoja na kauli elekezi ya Kinana, Sadifa ambaye pia ni Mbunge  wa Donge, Zanzibar alilazimika kucheza sarakasi zilizomwezesha kuzima mapinduzi yaliyokuwa yameandaliwa dhidi yake. Mwenyekiti huyo aliongoza kikao cha Baraza Kuu kwa saa tatu na kukamilisha ajenda zilizokuwa zimepangwa, ikiwa ni pamoja na kuwaidhinisha wakuu wapya wa idara za jumuiya hiyo,  kisha aliahirisha mkutano huo mara tu baada ya kuibuliwa kwa hoja ya kutaka kumjadili.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana jioni zilisema, Mwenyekiti wa UVCCM, Mkoa wa Mbeya, Amani Kajuna ndiye aliyeibua hoja ya kutaka Sadifa ajadiliwe kutokana na kile alichosema kuwa kiongozi huyo ameifanya jumuiya hiyo kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
“Kama tunataka kusonga mbele katika jumuiya yetu, lazima tuhakikishe kwamba tunaisafisha nyumba yetu ili tukitoka hapa wote tuwe tunazungumza lugha moja. Kwa hiyo napendekeza mwenyekiti atoke nje ili tumjadili,” chanzo chetu kilimnukuu Kajuna.
Habari zaidi zilidai mapendekezo hayo ni kama yaliungwa mkono na baadhi ya wajumbe, akiwamo Mwenyekiti wa UVCCM wa Mkoa wa Dodoma, Henry Msunga ambaye alisimama na kusema: “Hiyo ni hoja ya msingi sana”.
Hata hivyo, wakati wajumbe wengine wengi wakiwa wameinua mikono yao juu wakitaka kuchangia pendekezo hilo, Sadifa alisimama na kuanza kuzungumza huku akiomba msamaha kwa upungufu wa kiuongozi unaojitokeza na katika hali isiyotarajiwa aliahirisha rasmi mkutano huo.
Kajuna na Msunga kwa nyakati tofauti jana, walilithibitishia gazeti hili kuwapo kwa matukio hayo, lakini walikataa kuyazungumzia kwa undani huku wakisema kuwa bado wana fursa katika vikao vijavyo kwa ajili ya kurekebisha mambo ndani ya jumuiya hiyo.

 Mimi bado nina imani na jumuiya yetu, maana watendaji ambao tumewapitisha leo (jana) ninaamini watafanya kazi nzuri. Sisi viongozi wa mikoa tuko vizuri na tuna wanachama wengi, kwa hiyo jumuiya itaendelea kuwa imara,” alisema Kajuna.
Kwa upande wake, Msunga alisema: “Baada ya hoja kuibuliwa kweli mimi niliiona ni ya msingi sana, ila nimeridhika na maelezo kwamba mkutano ulikuwa na ajenda maalumu kwa hiyo ninachoamini ni kwamba fursa bado ipo, tutakapokutana tena tutakuwa na nafasi ya kurekebisha kasoro zinazojitokeza”.
Jitihada za kumtafuta Sadifa hazikufanikiwa jana, baada ya gazeti hili kuambiwa kuwa alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya jumuiya hiyo, kilichokutana jana usiku.
Chimbuko la mapinduzi
Mpango huo wa mapinduzi ulikuwa ni mwendelezo wa fukuto lililoanzia katika Mkutano Maalumu wa Baraza Kuu lililofanyika Zanzibar mapema Septemba mwaka huu, wakati wajumbe walipowakataa wakuu wa idara za UVCCM kwamba hawakuwa halali kutokana na uteuzi wao kutofuata taratibu na kanuni za jumuiya hiyo.
Mapema jana kabla ya kuzuka kwa hoja za kutaka kumjadili Sadifa, baraza hilo liliwapitisha wakuu wa idara wapya watatu akiwamo hasimu wa kisiasa wa mwenyekiti huyo wa UVCCM, Paul Makonda ambaye sasa ataongoza Idara ya Chipukizi na Uhamasishaji.
Makonda mara baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa jumuiya hiyo mwishoni mwa mwaka jana alipokuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti, aliteuliwa kuwa mjumbe wa Baraza Kuu lakini aliikataa nafasi hiyo.
Hatua hiyo ilimgharimu katika kikao cha Baraza Kuu la UVCCM, Februari mwaka huu, wakati alipokwenda Dodoma kwa mwaliko wa kuhudhuria kikao hicho, lakini baada ya kuchukua posho, alitimuliwa kwa maelezo kwamba aliwahi kukataa nafasi hiyo.
Taarifa ambazo gazeti hili lilizipata na kuthibitishwa na Katibu Mkuu wa UVCCM, Sixtus Mapunda zilisema wengine walioteuliwa na kuidhinishwa na Kikao cha Baraza Kuu ni Zainabu Katimba atakayeongoza Idara ya Oganaizesheni na Omari Suleiman ambaye amepewa Idara ya Fedha na Uchumi.
Sadifa ambaye pia ni Mbunge wa Donge aliwahi kulalamika juu ya kuwapo kwa kundi la vijana ambao wamekuwa wakimpiga vita sambamba na kuingilia utendaji wa kazi zake za kila siku kinyume cha katiba ya jumuiya hiyo.
SOURCE: MWANANCHI