Wednesday 30 October 2013

JK atua London ziara ya kikazi


30th October 2013
Rais Jakaya Kikwete, akisalimiana na wafanyakazi wa Swissport katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, wakati akielekea kupanda ndege kwenda London, Uingereza, kwa ziara ya kikazi ya siku nne juzi jioni. Kulia kwake ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Meneja wa Shirika la Ndege la Emirates uwanjani hapo, Aboubakar Jumaa.
Rais Jakaya Kikwete, ameondoka nchini kwenda London, Uingereza kwa ziara ya kikazi ya siku nne.

Rais Kikwete aliondoka juzi jioni ambako akiwa London, atahudhuria Mkutano wa Kimataifa wa Serikali Uwazi (Open Government) uliotishwa na Serikali ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameroun.

Mkutano huo wa siku mbili, utafanyika leo na kesho kwenye Ukumbi wa Queen Elizabeth 2 mjini London.

Miongoni mwa mambo makuu ambayo mkutano huo utazungumzia ni Serikali Uwazi na Ajenda ya Maendeleo baada ya mwaka 2015 wakati muongo wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia unafikia mwisho.

Masuala mengine yatakayozungumzwa katika mkutano ambao Rais Kikwete anaambatana na Mawaziri wake watatu ni pamoja na uwazi katika manunuzi ya umma, uwazi katika mikataba, haki ya kupata habari, uwazi katika ukaguzi wa fedha za umma, uwazi wa Serikali na vyombo vya habari, uwazi katika mikataba ya maliasili, uwazi katika maendeleo ya nchi zinazoendelea.

Mawaziri wanaoambatana na Rais Kikwete katika ziara hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar Mwinyihaji Makame.

Rais Kikwete anatarajia kurejea nyumbani Jumamosi hii.
 
CHANZO: NIPASHE