Wednesday 30 October 2013

Chadema wajibu tuhuma za Mwigamba


Na Fidelis Butahe, Mwananchi

Posted  Jumatano,Oktoba30  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi

Mwigamba alisimamishwa katika Mkutano wa Baraza la Uongozi la chama hicho Kanda ya Kaskazini siku tatu zilizopita akituhumiwa kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii wa Jamii Forums.


Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeibuka na kujibu tuhuma zilizotolewa katika mitandao ya kijamii na Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba, zilizosababisha hadi kusimamishwa wadhifa wake kwa muda usiojulikana, kikieleza kuwa hazina ukweli wowote.
Katika andiko lake kwenye mtandao, Mwigamba anadaiwa kuwatuhumu viongozi wa juu wa Chadema akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Wilbrod Slaa kuwa wamechakachua katiba ya chama hicho kuhusu ukomo wa nafasi za uongozi ili kujinufaisha binafsi.
Mwigamba alisimamishwa katika Mkutano wa Baraza la Uongozi la chama hicho Kanda ya Kaskazini siku tatu zilizopita akituhumiwa kusema uongo, kupotosha taarifa za chama na kuchonganisha viongozi kupitia mtandao wa kijamii wa Jamii Forums.
Mbali na kujibu tuhuma hizo, chama hicho kimesema kauli zinazozidi kutolewa na Mwigamba katika vyombo vya habari ni kinyume na Katiba ya chama hicho ambayo inaeleza kuwa, kama mwanachama ana jambo au malalamiko anatakiwa kuwasilisha katika vikao vya ndani vya chama.
Taarifa iliyotolewa na chama hicho jana ilieleza kuwa, Mwigamba alitoa taarifa mbili zinazokinzana akiwa katika kikao cha chama hicho mkoani Arusha na wakati akiwa katika mkutano wa baraza hilo.
“Kwanza alikana kuwa hakuandika chochote katika mitandao ya kijamii, lakini juzi wakati akizungumza na wanahabari alikiri wazi kuwa, waraka aliouandika ulikuwa wake,” ilieleza taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa, hakuna kiongozi yeyote wa chama hicho aliyebadili vifungu vya katiba ya chama hicho na kwamba katiba hiyo iliandikwa upya mwaka 2006 na haikufanyiwa marekebisho kama ambavyo amedai Mwagimba.
Imeelezwa kuwa maoni yaliyotolewa na kiongozi huyo aliyesimamishwa kuhusu katiba kuvunjwa yana maswali mengi, kwa sababu yametolewa na mtu anayejua kila kinachoendelea ndani ya chama hicho.
Katika hatua nyingine, Diwani wa Kata ya Nyasura wilayani Bunda kwa tiketi ya Chadema, Zamberi Ngobayi (68) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando Mwanza alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya kiharusi uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

SOURCE: MWANANCHI