Tuesday 29 October 2013

Askari aliyeuawa DRC alikuwa mbioni kufunga ndoa Desemba



Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Oktoba28  2013  saa 21:57 PM
Kwa ufupi
Kauli hiyo ilitolewa jana na kaka wa marehemu, Dk Aziz Mlima

Dar es Salaam. Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliyeuawa kwa kupigwa risasi kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, (Monusco), Luteni Rajab Ahmed Mlima, alikuwa katika hatua za mwisho za kufunga ndoa.
Askari huyo aliuawa katika uwanja wa mapambano na vikosi vya wapiganaji wa Kundi la Waasi la M23, katika Milima ya Gavana, karibu na Goma, DRC- Congo wakati akitekeleza jukumu la ulinzi wa amani
Akizungumza na gazeti hili, kaka wa marehemu Dk Aziz Mlima, alisema kuwa ndugu yake alikuwa tayari amekamilisha mipango yote na kilichokuwa kikisubiriwa ni siku ya kufunga ndoa hiyo.
“ Alikuwa yuko mbioni kufunga ndoa, lakini kwa sasa sitapenda kutaja jina la mchumba wake kwa kuwahayupo hapa lakini naye ni askari,” alisema Dk Mlima.
Alisema mwili wa marehemu unatarajiwa kuwasili nchini leo ukitokea Entebbe, nchini Uganda, ulikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.
“ Utakapowasili utaendelea kuwa nchini ya jeshi na baadaye kupewa heshima za mwisho kesho na siku inayofuata yaani Alhamisi, tutakuwa na mazishi ya kifamilia” alisema Dk Mlima.
JWTZ yatoa tamko
Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Makao Makuu ya JWTZ, ilisema askari huyo alipigwa risasi wakati akiwalinda wananchi wasidhurike na mapigano kati ya Jeshi la Serikali ya DRC na wapiganaji wa Kundi la M23.
Taarifa hiyo ya JWTZ, ilisema Monusco inajipanga kuuleta mwili wa marehemu na wananchi watajulishwa taratibu za mapokezi, kuaga mwili na mazishi.
Ofisa huyo anakuwa wa pili wa JWTZ kuuawa katika mapigano nchini humo, baada ya hivi karibuni Meja Khatib Shaaban Mshindo, kuuawa kwa bomu katika mapigano makali yaliyotokea katika mji wa Goma, Agosti 28, mwaka huu.
Julai 13, askari saba wa Tanzania waliokuwa wakilinda amani katika mji wa Darfur nchini Sudan, waliokuwa katika mpango wa kulinda amani, waliuawa na kikundi cha Janjaweed.

SOURCE: MWANANCHI