Saturday 28 September 2013

Yaliyojiri Miss Tanzania 2013: Nyota ya Happinness iling’ara mapema

 
Na Herieth Makwetta, Mwananchi

Posted  Septemba28  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Warembo walilicheza kwa ubunifu licha ya wachache wao kukosea na kujichanganya. Katika shoo warembo hao walivalia mavazi tofauti huku wakiiga uchezaji wa Kundi la P Sqare wakichanganya na uchezaji wa wimbo wa Thriller ulioimbwa na hayati Michael Jackson.

Dar es Salaam. Suti nyeusi yenye shati nyeupe na tai nyekundu kwa wanaume na magauni marefu na mafupi kwa wanawake, ndiyo mavazi yaliyotawala usiku wa kumtafuta malkia mpya wa urembo nchini Tanzania Jumamosi iliyopita katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Kila mgeni aliyewasili kwa lengo la kuingia ukumbini humo alihitajika kupita katika zulia jekundu ‘red carpet’ kwa ajili ya mahojiano mafupi na mtangazaji Sauda Mwilima wa Star Tv pia kupiga picha, kabla ya kuingia kupitia milango miwili wa VIP na ule wa viti vya kawaida.
Onyesho lilianza saa 3 usiku likifunguliwa na shoo ya warembo wote 30 waliocheza dansi kupitia wimbo wa ‘Personally’ wa wasanii P Sqare, dansi walilofunzwa na msanii wa ngoma za asili Wanne Star.
Warembo walilicheza kwa ubunifu licha ya wachache wao kukosea na kujichanganya. Katika shoo warembo hao walivalia mavazi tofauti huku wakiiga uchezaji wa Kundi la P Sqare wakichanganya na uchezaji wa wimbo wa Thriller ulioimbwa na hayati Michael Jackson.
Kikundi cha ngoma za asili cha Mama Afrika ndicho kilichoendeleza burudani katika Jukwaa la Redds Miss Tanzania lililokuwa na upana na hadhi ya aina yake ambapo baadaye warembo waliingia na mavazi ya ubunifu yaliyobuniwa na wabunifu mbalimbali wa hapa nchini.
Wakati wa kuonyesha vazi la ubunifu warembo walitambulishwa kwa majina yao na hadhi zao kwa makundi, kisha kupanda jukwaani ikishuhudiwa jitihada za wabunifu zilizoonyesha uwezo wao kwa kubuni mavazi mapya machoni pa wengi.
Baada ya kuonyesha vazi la ubunifu, warembo walirejea jukwaani safari hii wakionyesha vazi la ufukweni, lililonakshiwa na kitenge cha Kiafrika ambalo ni  ubunifu wa Veronica Lugenzi. Jambo la kushangaza lililojitokeza ni vazi hilo kuvaliwa na viatu virefu, badala ya viatu vifupi vya wazi kama ilivyo uhalisia wa vazi la ufukweli, kosa linalojirudia kwa miaka kadhaa sasa. 
Kuhitimishwa kwa onyesho la vazi la ufukweni kulitoa fursa kwa jukwaa kupambwa na burudani ya muziki iliyotolewa na mwanamuziki Judith Wambura maarufu Lady JD aliyevaa vazi 
lililopendezeshwa na mchanganyiko wa rangi nyeusi, dhahabu na fedha. Akiongozwa na Dj Choka, Lady JD aliimba wimbo unaotambulika kwa jila la Wangu aliomshirikisha Mr Blue, kisha kuimba wimbo maarufu wa Joto Hasira kabla ya kushuka jukwaani na kuwapisha warembo, waliopanda na vazi la jioni.
Licha ya awali kutangazwa kwamba mwanamuzi huyo angekuwa na bendi yake, lakini hali ilikuwa tofauti kwani aliimba kwa ‘play back’ jambo lililowashangaza wengi.
Kimbwanga kiliibuka pale mrembo mmoja aliyekuwa amevalia nambari 6 kujikuta gauni alilovaa likizuiwa na kiatu kisha kujikwaa kwenye ngazi alipotaka kupanda jukwaani kutoka nyuma ya jukwaa. Mrembo huyo alijaribu kujinasua zaidi ya mara tatu na kushindwa hivyo kuamua kurudi nyuma ya jukwaa, kabla ya kupanda tena jukwaani na kundi lililofuata huku akionekana kukosa kujiamini tofauti na alivyokuwa awali.
Baada ya warembo kuonyesha mavazi hayo walichaguliwa walioinga 15 bora sanjari na warembo watano walioshinda mataji mbalimbali.
Mwanamuziki Mike Ross kutoka Uganda ndiye aliyepokea jukwaa na kutoa burudani kabla ya kumpisha Lady JD aliyepanda kwa mara ya pili na kuuinua umati wa mashabiki kwa kuimba wimbo wake unaotamba zaidi kwa sasa ‘Yahaya’ kabla ya kumpisha jaji kusoma majina ya warembo watano walioingia hatua ya fainali.

Jaji huyo, Dk Ramesh Shaa alisoma majina ya warembo walioingia hatua ya fainali ambao ni Lucy Tomeka, Isabel Petty, Clara Bayo, Latifa Mohamed na Happiness Watimanywa.
Warembo hao waliulizwa maswali mbalimbali waliyoyachagua, wa kwanza  kuchagua swali akiwa Happiness Watimanywa aliyechagua swali namba tano lilimhoji iwapo atachaguliwa kuwa Miss Tanzania atafanya kipi ambacho warembo waliotangulia walishindwa kufanya katika nyanja tofauti. Happyness alijibu swali hilo kwa ufasaha na umakini mkubwa hali iliyoufanya ukumbi ulipuke kwa shangwe.
Katika mashindano hayo ambayo kwa miaka miwili sasa yanadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s, Happiness Watimanywa, ndiye aliyeibuka kuwa malkia mpya wa urembo na kuvikwa taji la Redds Miss Tanzania, akiandika historia mpya katika miaka 21 ya mashindano hayo.
Happiness mwenye umri wa miaka 19, aliyeibukia kutoka mashindano ya urembo ngazi za vitongoji mkoani Dodoma, anakuwa mshindi wa kwanza aliyekubalika vilivyo na wapenzi wa fani ya urembo nchini sanjari na warembo wenzake 29 aliokuwa akichuana nao.
Nafasi ya pili ilikwenda kwa Latifa Mohamed huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Clara Bayo. Nafasi ya nne na tano zilikwenda kwa Isabel Petty na Lucy Tomeka.                           
Taji lililoongezeka usiku huo ni la Balozi wa Marie Stopes, ambalo lilikwenda kwa Marietha Boniphace.
Wasifu wa Happyness Watimanywa
Happiness Watimanywa, ndiye msichana pekee kutoka Tanzania aliyeweka historia ya kuongoza nchi zaidi ya 150 za mtandao wa IGCSE katika somo la Uhasibu kwenye mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2010.
Yeye ni mzaliwa wa familia ya Louis Roussos ya
Morogoro. Wadogo zake Angel na Romeo sasa wanasoma shule ya St Constantine ya mkoani Arusha ambayo pia alisoma malkia huyo. Happiness amewahi kusoma Laureatte International School ya Dar es Salaam, ambapo alikutana na mwalimu wa michezo anayemtaja kwa jina la Tchalewa Ndeki akimwelezea kuwa ndiye aliyemfungulia mipaka ya kimataifa.
Akiwa Laureatte, Happiness aliwahi kwenda China na South Korea pamoja na wanafunzi wenzake katika matamasha mbalimbali ya elimu na michezo. Baada ya kumaliza kidato cha nne, alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Strathclyde cha Uingereza anaposomea Shahada ya Biashara.
Kipindi Happiness alipokuwa kwenye likizo ndefu,  aliamua kujihusisha na masuala ya urembo na kufanikiwa kutwaa Taji la Miss Dodoma, Miss Kanda ya Kati na hatimaye kuingia kwenye Kambi ya Miss Tanzania.

Akiwa Miss Tanzania, Happiness alikuwa ni mshiriki wa kwanza kuingia nusu fainali ya mashindano hayo kwa kutwaa taji la Redds Miss Photogenic 2013.
Ndani ya Kambi ya Miss Tanzania, Happiness Watimanywa alikuwa mwiba kwa warembo wengine 29 wanaowania taji hilo kwani alikuwa akionyesha uwezo wa hali ya juu kuanzia kwenye kipaji hata michezo, mbali na upeo mkubwa alio nao.
Akizungumzia Redd’s Miss Tanzania, Happeness alisema kwa kifupi: “Nilipoingia kambini nilipata hofu kuona warembo wenzangu, wengi walikuwa wazuri pia wenye uwezo, nikajitahidi kuwa karibu nao kuondoa hofu na kujenga kujiamini zaidi kuwa naweza.”

SOURCE: MWANANCHI