Monday 23 September 2013

Unyama Kenya : Waliouawa na magaidi wafikia 69

 


Baadhi ya raia, waliokuwa ndani ya jengo hilo wakitoka nje kwa hofu kubwa jana, Picha na AFP 
Na Waandishi wetu, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Septemba23  2013  saa 8:19 AM
Kwa ufupi
Magaidi hao wanaodaiwa kuvalia vitambaa vyeusi vinavyofunika nyuso zao, wameteka eneo hilo kwa siku mbili, huku wakiwa wamezima taa zote za ili kujilinda na askari wa Kenya ambao waliingia kupambana nao.

Bado jengo hilo limezingirwa na wanajeshi, kuhakikisha magaidi hao hawatoki nje kuhatarisha usalama wa wananchi.
Nairobi. Magaidi wanaokadiriwa kuwa kati ya 10 na 15 wamelitikisa Jiji la Nairobi kwa siku mbili mfululizo baada ya kuteka jengo kubwa la biashara la Westgate lililopo Westlands na kuua watu wapatao 69 hadi leo asubuhi.
Magaidi hao walivamia jengo hilo juzi saa tano asubuhi na hadi jana, jitihada za kuwadhibiti zilikuwa hazijafanikiwa. Zaidi ya watu 1,000 wameokolewa na wengine zaidi ya 170 wamejeruhiwa.
Tukio hilo limesababisha shughuli mbalimbali katika Jiji la Nairobi kusimama na hata maduka mengine makubwa ya Nakumatt kufungwa, hivyo kusababisha upatikanaji wa bidhaa mbalimbali kuwa shida kwa wakazi wengi wa Nairobi.
Wakazi wengi wa eneo la Westlands jana walikwama kufika katika maeneo yao na watu wengi waliokuwa kwenye jengo hilo waliacha magari yao na kukimbia huku na huko ili kujiokoa huku vyombo vya usalama vikiwataka wananchi kukaa mbali na eneo hilo.
Magaidi hao wanaodaiwa kuvalia vitambaa vyeusi vinavyofunika nyuso zao, wameteka eneo hilo kwa siku mbili, huku wakiwa wamezima taa zote za ili kujilinda na askari wa Kenya ambao waliingia kupambana nao.
Risasi zimekuwa zikisikika usiku kucha na watu zaidi wameendelea kuuawa huku Serikali ikisema mateka wanaodaiwa kuwepo ndani ya jengo hilo wakiwa chini ya magaidi hao ni 30.
Jengo hilo limezingirwa na vyombo vya usalama vya ndani na nje ya Kenya vikiongozwa Mkuu wa Majeshi ya Kenya pamoja Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), David Kimaiyo, ambaye amekuwa akitoa taarifa mbalimbali za tukio hilo kupitia account yake ya Tweeter ili kuhakikisha vyombo vya habari na jamii vinajua kinachoendelea.
Pia Wizara ya Mambo ya Ndani imekuwa ikitoa taarifa kupitia mitandao yake, huku televisheni zote za Kenya zikirusha tukio hilo moja kwa moja tangu lilipotokea juzi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Joseph Ole Lenku akizungumza na vyombo vya habari alisema watu 69 waliouawa ni pamoja na raia wa kigeni kutoka nchi mbalimbali. Hata hivyo, alisema haijajulikana ni wangapi na wanatoka nchi gani haswa.
Canada imethibitisha kuwa raia wake wawili wameuawa kwenye tuko hilo, pia raia wawili wa Ufaransa nao wameuawa.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab limedai kuhusika na tukio hilo ambalo ni kubwa kutokea Kenya tangu ubalozi wa Marekani ulipolipuliwa mwaka 1998 jijini Nairobi.

READ MORE : mwananchi.co,tz