Sunday 29 September 2013

Tanzania yashtukia mtego jeshi la pamoja EAC

28th September 2013

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)
Siri za kutengwa kwa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinazidi kufichuka, baada ya kudaiwa kuwa nchi za Kenya, Uganda na Rwanda zilitumia ubabe kushinikiza ikubali kusaini itifaki ya kuunda jeshi la pamoja.

Habari za uhakika kutoka vyanzo vyetu vya habari, zilidai kuwa nchi hizo zilikuwa zikiishinikiza Tanzania ikubali kutia saini ripoti ya viongozi wakuu wa nchi hizo, ambapo ndani yake kuna itifaki inayojulikana kama Mutuar Defence Park (MDP) inayoruhusu majeshi ya nchi hizo kuingilia kati nchi mwanachama zinapopigana vita.

Hata hivyo, katika kikao hicho kilichofanyika jijini Bujumbura nchini Burundi, hali ilikuwa mbaya baada ya kuona wajumbe wa Tanzania wakipinga suala hilo, wakitoa sababu kwamba jambo hilo ni jipya, lazima yawepo kwanza majadiliano ya wazi.

Msimamo huo wa serikali, ulionyesha kuzikera nchi za Rwanda na Uganda ambazo kwa miaka mingi zinakabiliwa na mapigano dhidi ya vikundi vya waasi.

Nchi hizo zilikuwa zikiamini kuwa kama Tanzania itakubali kusaini itifaki hiyo, haitaweza kupeleka majeshi yake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kupambana na waasi wa M23.

Lengo la nchi hizo ni kusaidiwa katika vita vyao na waasi wa Rwanda wa Interahamwe (FDLR) kwa upande wa Rwanda na waasi wa Lord Resistance Army (LRA) wanaopigana na Serikali ya Uganda.

"Wajumbe wa Tanzania hawakukubaliana na jambo hilo, walisema suala hilo ni jipya na endapo litakubaliwa kuwa itifaki nchi itajiingiza kwenye mtego," kilisema chanzo hicho.

Pamoja na msimamo huo, nchi hizo zilishinikiza kusaini kwa ripoti hiyo haraka, hatua ambayo ilisababisha wajumbe kutoka Tanzania kususia kikao hicho.

"Wakati wa kusaini ripoti hiyo, kiti cha nchi yetu kilikuwa kitupu jambo ambalo lilileta hali ya wasiwasi kwa Watanzania," ilisema.

Chanzo hicho kilisema kuwa baada ya kuona hali imekuwa ngumu, nchi hizo zilikubaliana na maoni ya Tanzania na kuomba kuwepo na majadiliano ya namna ya kufikia muafaka wa jambo hilo.

SERIKALI YAZUNGUMZA
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Naibu Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dk. Abdullah Juma Sadallah, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema uamuzi huo ulikuwa kwa ajili ya maslahi ya Watanzania.

Hata hivyo, alisema tayari viongozi wa nchi zote wamelipatia ufumbuzi suala hilo na kutiliana saini ya uanzishwaji wa mazungumzo ya uwepo wa suala hilo.

"Ninasisitiza kwamba nchi yetu inafuata taratibu za kidemokrasia lazima kama kitu kipya wananchi wafahamishwe na waridhie kuliko kufanya makubaliano ya viongozi." alisema Dk. Sadallah.

Alipoulizwa kama nchi hizo zitakapoiweka Tanzania kando na kuanza suala hilo peke yao kama ilivyofanya hivi karibuni katika mambo mbalimbali ikiwamo miradi, viza ya pamoja na raia kuwa na uhuru wa kuingia kwenye nchi hizo bila kikwazo. Dk. Sadallah alisema hilo halitawashangaza.

"Ninachowaomba wananchi wasiwe na hofu hata kama wakiamua wao kuanza basi ruksa, lakini kwanza kuwepo na makubaliano ya nchi zote tano vinginevyo itakuwa nje ya EAC kama walivyofanya nyuma," alisema.

Alisisitiza kuwa wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Samuel Sitta ipo makini na inafanya kazi zake kulingana na maoni na matakwa ya wananchi na ndio maana bado maslahi ya nchi yanaendelea kulindwa. 
CHANZO: NIPASHE