Monday 16 September 2013

Tanzania yaihofia EAC

15th September 2013
Hatimaye serikali imeonyesha wasiwasi juu ya mwenendo wa nchi tatu zilizo miongoni mwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Imepinga dalili zinazoonekana kwa nchi za Kenya, Uganda na Rwanda, kutumia jina la EAC kuomba fedha au kugharamia miradi inayopaswa kuwa ya Jumuiya.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afrika Mashariki, Dk. Abdallah Abdallah, wakati akizungumza na NIPASHE Jumapili jijini Dar es Salaam juzi.
Alisema malalamiko hayo, yalishawasilishwa pia katika kikao cha baraza la mawaziri wa EAC, kilichofanyika hivi karibuni jijini Arusha.
Dk. Abdallah, alisema serikali imemtaka Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sezibera, kutoa maelezo juu ya gharama ya miradi kadhaa inayoaminika kuwa sehemu ya jumuiya hiyo.
Nchi hizo zimekuwa katika mchakato wa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo na kuonekana kuitenga Tanzania.
Marais wa nchi hizo, Uhuru Kenyata (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) na Paul Kagame (Rwanda), walikutana mara mbili bila kumualika Rais Jakaya Kikwete.
Kwenye vikao viwili vilivyofanyika Kampala na Nairobi, viongozi hao walikubaliana kutekeleza kwa haraka miradi ya ujenzi wa reli itakayounganisha nchi hizo na bomba la mafuta litakalojengwa kuanzia Sudan Kusini hadi Mombasa na jingine kutoka Kampala hadi Kigali.
Katika hatua nyingine, nchi hizo zimetangaza kuanzia Januari, Mosi mwakani, raia wao watembeleana bila kuwa na hati ya kusafiria, pia kuwa na viza moja kwa watalii.
Katika kuonyesha umoja huo unakuwa katika sura ya jumuiya, mkutano wa Kenya ulioambatana na ufunguzi wa gati katika bandari ya Mombasa, nchi za Burundi na Sudani Kusini zilialikwa na kuwakilishwa na mawaziri wao waandamizi. Tanzania haikualikwa.
Katika hatua nyingine, juzi vyombo vya habari viliwakariri baadhi ya mawaziri wa nchi hizo waliopewa jukumu la kusimamia makubaliano hayo, wakieleza makubaliano hayo ni ya Jumuiya nzima na endapo Tanzania ikipenda kuingia itakaribishwa.
Pia, Dk. Abdallah, alisema hatua zilizochukuliwa na nchi hizo kwa kukubali kuanzisha utaratibu wa matumizi ya viza moja na vitambulisho vya pamoja, ni mfano wa ubabe usiokidhi matakwa ya kidemokrasia.
"Tatizo linakuja kwamba Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, inafanya uamuzi wa kushirikisha wananchi wake, lakini wenzetu wanatumia ubabe ili kutulazimisha, kitu ambacho hakikubaliki," alisema Dk. Abdallah.
Alisema kimsingi suala hilo halikupelekwa na kukubaliwa na nchi tano za EAC zikiwamo Tanzania na Burundi, kama makubaliano ya jumuiya yanavyoeleza.
Alisema, kama nchi hizo zilikusudia kuwapo utaratibu huo, zingeitisha kikao na kupata baraka za nchi zote, ili kutoa uhuru kwa nchi zinazotaka kuanza zifanye hivyo.
"Utaratibu unaweka wazi kabisa, lazima nchi tano zikubaliane kwanza kwa jambo lolote, hata kama ikitokea nchi mbili au tatu zitaamua kuanza hakuna tatizo, lakini hilo halikufanyika sisi tunasikia kwenye vyombo vya habari," alisema.
Dk. Abdallah alisema Tanzania haipingi kwa nchi hizo kuanzisha miradi ya kimaendeleo kwa sababu ni jukumu lao kwa ajili ya kujijenga kiuchumi.
Hata hivyo, alisema lazima miradi hiyo iwe nje ya makubaliano ya kiuchumi na biashara ya EAC.
Alisema kama miradi hiyo itahusisha katika jumuiya na kutumia rasilimali zake itakuwa kinyume na makubaliano hayo.
"Tanzania ni mwanachama muanzilishi, inachangia jumuiya, ni makosa makubwa fedha au ufadhili ukatumika kupitia mgongo wa chombo hicho ikiwa mwanachama mmoja hajui chochote," alisisitiza.
Alitolea mfano kwamba Tanzania imetekeleza miradi kama hiyo kwa baadhi ya nchi wanachama, lakini ilifanya kama ya nchi na nchi na haikuhusisha umoja huo.
"Tulitumia fedha zetu kwa kujenga na kutekeleza miradi yetu, kama wenzetu wakiingiza kwenye Jumuiya itakuwa makosa, tunashauri waendelee kufanya kama ushirikiano wa nchi na nchi pekee," alisema.
Hata hivyo juhudi za kumpata Dk. Sezibera kuelezea juu ya hatua hiyo ya serikali ya Tanzania haikuweza kufanikiwa baada ya alipopigiwa simu kuonyesha kuzimwa.
Naibu Waziri aliwataka wananchi kutohamaki wala kuwa na wasiwasi na mwenendo uliokuwapo katika EAC, akisema viongozi wao waliopewa mamlaka wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa.
Alisema yeye na Waziri wake Samuel Sitta, wapo makini na kila kinachofanywa kinakuwa na umuhimu wa nchi.
"Tuna uhuru wa nchi kuona jambo hili linatufaa au halitufai, hatuwezi kuburuzwa kutokana na uharaka wa watu fulani, huo ndiyo msimamo wetu na wananchi wanatuelewa," alisema.  
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI