Sunday 29 September 2013

Serikali kukopesha wanafunzi 29,754 elimu ya juu


28th September 2013

Cosmas Mwaisobwa
Serikali itawakopesha wanafunzi 29,754 wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo wa 2013/14.
Aidha, Bodi ya mikopo ya elimu ya juu inatarajia kutoa mikopo ya Sh. bilioni 306 kwa ajili ya wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo.

Lengo la serikali ni kuwakopesha wanafunzi 31,647. Mkurugenzi wa Habari, Elimu na Mawasiliano, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Cosmas Mwaisobwa, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alipozungumzia utaratibu wa utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na elimu ya juu.

“Uchambuzi wa maombi ya mikopo kwa mwaka huu wa masomo umekamilika,” na lengo la serikali ni kuwawezesha wanafunzi wa elimu ya juu kwa muda muafaka.

Alisema kuwa mchanganuo wa utuoaji wa mikopo hiyo ulizingatia vigezo na masharti ya uombaji mikopo na ruzuku.
Alisema kuwa idadi ya waombaji wapya waliotuma maombi ya mikopo ni 53,239, waombaji wanaoendelea na masomo 43,032, waombaji waliokuwa na maombi yenye matatizo ni 6,364.

“Wengine ni waombaji waliorekebisha matatizo kwenye maombi yao 3,151 na waombaji ambao hawakurekebisha matatizo kwenye maombi yao 3,213,” alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu mchanganuo huo alisema waombaji wapya 53,630 watakaosoma ndani na nje ya nchi wamepata mikopo hiyo.

Alisema maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaoendelea 61,692 ambao wanasoma ndani na nje ya nchi wamepangiwa kupata mikopo hiyo.

Alisema mchakato wa upangaji wa mikopo unaendelea vizuri ambapo hadi sasa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90. “Matarajio ni kukamilisha mchakato huu kwa asilimia 100 ifikapo wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba kabla ya Vyuo vya Elimu ya Juu kufunguliwa, kwa mujibu wa Tume ya Vyuo Vikuu,” alisema.

Alisema orodha kamili ya waombaji wapya waliopangiwa mikopo inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz) ambapo mwombaji anaweza kutafuta jina lake kwa kutumia namba ya mtihani ya kidato cha nne. Alisema taratibu za kupeleka mikopo yao vyuoni zinaendelea na kwamba watalipwa baada ya kufanya usajili. Alisisitiza umuhimu wa kila mwombaji kuwa na akaunti ya benki kwa ajili ya kupitishia mikopo hiyo.

Alisema waombaji waliofanikiwa kupangiwa mikopo wanawajibika kurejesha mikopo hiyo baada ya kuhitimu masomo yao.
 
CHANZO: NIPASHE