Thursday 12 September 2013

Maoni na mapendekezo kwa kampuni za simu na vyombo vya usimamizi Tanzania


12/09/2013

Teknologia ya mawasiliano ya simu za mkononi ni kati ya ugunduzi mkubwa sana wa kisayansi ambao umewahi kutokea na kuathiri maisha ya wanadamu wengi kwa wakati mmoja. 

Ninadhani utakua ni ugunduzi unafuata baada ya ugunduzi wa kompyuta na mawasiliano ya intaneti. Ugunduzi wa mawasiliano ya simu za mkononi ni matokea ya utafiti wa kisayansi wa karibu karne moja ambao ulifanyika hatua kwa hatua hadi kufikia matokeo tunayoyaona sasa.

Mwanzo wa kizazi (generation) cha simu za mkononi tunazotumia sasa ni kazi mwanasayansi Martin Cooper aliyekua akifanya kazi na kampuni ya Motorola huko Marekani. Simu ya kwanza ya mkononi ambayo mwendelezo wake ndio simu tulizonazo sasa hivi, ilikua ni kubwa na yenye urefu wa kama sentimita 23 hivi na uzito wa kilo moja na gramu mia moja.

Ugunduzi huu ulifanyikwa takribani miaka 40 iliyopitika (1973) lakini hadi sasa mabadiliko makubwa sana ya kitechnologia yametokea sio tu katika kupunguza ukubwa na uzito wa simu ya mkoni, bali pia mfumo mzima wa mitandao ya mawasiliano, matumizi ya mitandao hii  na jinsi ilivyounganishwa na mifumo mingine ya
 kompyuta na intaneti. Kikubwa zaidi ku kupungua sana kwa gharama za kumiliki simu na tozo la kulipia muda wa mawasiliano.

Hapa kwetu Tanzania, tekonologia hii ilikubalika na kuanza kumumika miaka ya 1990, enzi hizo tukiwa na makampuni kama Traitel na Mobitel (Tigo ya sasa) na hadi sasa tuna makampuni mengi ya simu za mkononi (tunayajua) ambayo mengi yako chini ya sekta binafsi yakishindana katika soko kubwa lenye mamilioni ya wateja.

Ni ukweli ulio wazi kuwa, kama ambavyo imekua katika nchi nyingine nyingi duniani, makampuni  ya mawasiliano ya simu za mikononi yamekua na nafasi kubwa sana katika ujumla wa maisha ya watanzania katika nyanja zote za kimaisha. Matumizi ya simu za mkononi ni kati ya huduma za kijamii ambayo imepenya kwa nguvu na kwa sehemu kubwa sana katika maisha ya kila siku ya watu wengi bila kujali ngazi ya elimu waliyonayo, kipato au eneo wanaloishi. Ni ngumu sana kutenganisha huduma za makampuni haya na shughuli za kuichumi, kisiasa, kijamii, taaluma, biashara, kilimo, na nyingine nyingi. Sina haja ya kuelezea umuhim wa huduma za intaneti na fedha zinazotolewa na makampuni haya na jinsi ambavyo kila siku zimetumika kurahisha shughuli za kimaisha.

Kukubalika kwa huduma ya makampuni ya simu na kutumika na mamilioni ya watu, ni wazi kuwa biashara hii inalipa. Ukweli kwamba makampuni ya simu yamekua yakifanya biashara hii kwa miaka mingi sasa na mengine mengi bado yanajiingiza kwenye biashara hii, ni wazi kuwa wanajua wanachokifanya  na jamii inaona ni nini makampuni yanafanya. Makampuni haya yamekua wabunifu sana katika kujiendesha na kufanya matangazo ambayo yanamvutia kila mtu na kutamani kujaribisha huduma zinazotolewa; na hii ni afya kwa maelezo yoyote yale yanayoweza kutolewa.

Matatatizo yanayohitaji ufumbuzi

Pamoja na mengi tunayoweza kueleza kuhusu huduma za makampuni ya simu, bado ukweli unabaki kuwa mtumiaji wa huduma hizi au mteja amekua hapewi "hazi zote stahiki" kutokana na kile anachokinunua au kukistahili. Mojawapo kubwa ni mteja kukosa haki ya kujua undani na ukweli wa huduma anazopata pamoja na kuwa na uwezo wa kuhakikisha iwapo alichokilipia ndicho alichokitumia.

Ni kwa muda mrefu sasa kumekua na malalamiko mengi kwa wateja wa simu za mikononi kwa kile wanachokiona kama ni ama kutotendewa haki, kuonewa au kuibiwa na makampuni ambayo kwayo wanapata huduma. Ni mara nyingi tumesikia wabunge na wanasiasa wengine wakipiga kelele kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za wateja katika matumizi ya huduma za simu za mkononi. Mifano ni mingi ila nitataja michache tu ya kile ambacho kimekua kikillalamikiwa na wateja kwa muda mrefu sasa bila ufumbuzi wa kueleweka:

  1. Mteja kuingizwa kwenye huduma usizohitaji na kukatwa pesa bila kujua au kuambiwa, mfano kwenye milio ya simu 

  2. Mteja kutokuambia wazi ukweli kuhusu gharama ya baadhi ya huduma mteja anazoshawishiwa kuzitumia 

  3. Mteja kutumiwa wingi wa jumbe fupi za simu zilizojaa matangazo na habari zingine mteja asizohitaji

  4. Mteja kupotezewa muda mwingi wa hewani kwa kusikiliza matangazo wakati ambapo mteja anahitaji mawasiliano 

  5. Mteja anapopiga simu kulazimishwa kuingia kwenye mfumo wa ujumbe wa sauti pale simu anayoitafuta inapokua haiko hewani na kukatwa fedha nyingi wakati hakuomba kuingia kwenye huduma husika

  6. Mteja kukatwa kiwango kikubwa cha fedha kuliko huduma uliyotumia hasa unapopiga simu 

  7. Mteja kununua huduma (mfano vifurushi) na kukuta alichoahidiwa ni tofauti na anachopata

Ni jambo la kawaida kabisa kwa baadhi ya mitandao ya simu za mikononi kwamteja kuongeza muda wa maongezi kwenye simu yake na baada ya muda kujikuta salio limekwisha au limepungua sana bila kujua lilipotumika au lilivyotumika. Ni mara nyingi wateja wamejikuta wakishindwa kuelewa ni kwa  namna gani  wamelipia huduma ambazo hawajawahi kuziomba,  hawazihitaji wala kujua kuwa wanazo. Sina hakika sana hiki kinaweza kuelezwaje lakini kwa lugha nyepesi na isiyopiga kona nyingi, hiki chaweza kuitwa wizi wa wazi kwa mteja wa huduma za simu za mikononi.

Tatizo liko wapi?

  1. Ni watanzania wachache sana wanajua haki zao katika huduma wanazozipata au wanazostahili kuzipata baada ya kuzilipia. 

  2. Kibaya zaidi hata pale wanapojua na kufahamu kuwa mtoa huduma amewaonea, hawajui njia au taratibu za kufuata kutafuta haki yao.

  3. Hata kama wanajua taratibu za kufuata, wanapopima wanakuta gharama ya kufuatilia hiyo haki ni kubwa sana kuliko walichokipoteza na hivyo kuamua kujinyamazia. 

  4. Mwisho wa siku wateja wanajikuta wamezoea shida ya uonevu wa kihuduma wanaokutana nao na hivyo kuishi tu ili mradi yaende. Ni wateja wengi wanatumia mitandao ya simu hizi kwa uvumilivu kama vile uvumilivu wa kwenye ndoa kwani hawana "options". 

  5. Wanalazimika kutumia huku wakionewa kwani ukweli ni kuwa wanahitaji sana huduma husika.

  6. Mbaya zaidi, watoa huduma wanajua kuwa wateja wao hawana uwezo wa kufuatilia haki zao na huenda hakuna sheria nzuri za kuwalinda hata pale watakapozifuatilia

Nini kifanyike?

Pamoja na njia nyingi zinazoweza kutolewa kama suluhisho, kilio kikubwa ni kutaka kuona sheria na vyombo husika, vinachukua hatua za haraka, za makusudi na za uhakika katika kumlinda mtumiaji wa huduma za simu. Kama vile ambavyo vyombo na sheria husika za kibiashara zinatumika vema kulinda makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi, ni haki na wajibu wa vyombo husika kufanya hivyo pia kwa kumlinda mteja ili apate haki zake kwa kile anachokilipia. Wengi wa wateja wa simu  ni watu wasio na uwezo wa kifedha wala uelewa wa kutosha kuhusu haki, sheria na wajibu wa watoa huduma na hivyo ni wajibu wa vyombo na sheria husika kuwalinda kama sehemu ya haki zao za msingi za kiraia ndani ya nchi yao. Miongoni mwa mambo ninayoweza kushauri yafanyike ni pamoja na:

  1. Sheria itungwe au tararibu katika sheria husika ya kuyalazimisha makampuni ya simu za mkononi kuwa wazi vya kutosha kwa wateja wao kuhusu huduma wanazozitoa. Kuwe na adhabu stahiki kwa kampuni ambayo itagundulika kuwa haikua wazi kwa mteja wake kwa habari ya gharama za huduma walizompa au alizohitaji 

  2. Sheria hiyo hiyo itamke wazi haki za mteja wa huduma za simu za mkononi na njia stahiki za kisheria zisizo na usumbufu ambazo mteja ataweza kudai haki ya fidia kwa usumbufu na upotevu atakaokua kaupata toka kwa mtoa huduma 

  3. Sheria iwekwe au taratibu zitungwe katika sheria zilizoko na kusimamiwa vilivyo na vyombo husika yenye kuzilazimisha kampuni za simu za mikononi kumpa mteja uhuru wa kuhakiki matumizi yake na gharama aliyoitumia. Kama vile ambavyo mteja anaweza kuangalia mtiririko wake wa kuweka na kutoa fedha bank, hivyohivyo mteja aweze kuangalia mtiririko wa makato ya salio lake kwa kila simu aliyopiga na ujumbe mfupi aliotuma. Mara nyingi mteja anapokatwa fedha kinyume na taratibu na kuwasiliana na kitengo cha huduma kwa wateja, anajikuta napewa maelezo ambayo hawa uwezo ya kuyahakiki na kujikuta analazimika kukubaliana na asichoelewa huku akiwa na manung'uniko. Sheria iyalazimishe makampuni ya simu kumpa mteja njia rahisi ya kuhakiki muda na gharama ya huduma aliyoipata. Hili ni jambo linalowezekana kiufundi; mteja anaweza kufanya hivyo kwa kutumia simu yake kama aitumiavyo kuangalia huduma za fedha ama kuwa kupewa uwezo wa kuangali account yake kupitia tovuti ya kampuni husika baada ya kuingiza number yake ya simu na neno la siri.

  4. Sheria au taratibu ziwekwe kuzionya kampuni za simu kutopoteza muda wa mteja kwa kumsikizisha matangazo wakati anapohitaji kuwasiliana. Inasumbua pale ambapo mteja ana jambo la dharura na anahitaji kuwasiliana kwa haraka na badala yake anajikuta anasikilizishwa kwanza mtiririko wa  matangazo. Mbaya zaidi, unakuta matangazo anayopewa ni ya huduma ambayo tayari yeye ni mteja wa siku zote na hayana msaada kwake. taratibu hizohizo, ziyakataze makampuni ya simu za mkono kumtumia mteja wingi wa ujumbe mfupi wa simu bila ridhaa yake. 

Iwapo yatafanya hivyo yalazimishwe kumlipa kwa kila ujumbe wataomtumia kwani wanakua wamemfanya ubao wa matangazo.

---
Mathew Mndeme,
Dar es Salaam, Tanzania