Monday 16 September 2013

Kufa na kupona

Tido Mhando 


Posted  Jumapili,Septemba15  2013  saa 13:0 PM
Kwa ufupi
  • Wakati watu wakijipongeza kama vile sote tulikuwa kwenye mkabiliano ule yakaandikwa kwenye ubao mkubwa uwanjani pale maandishi makubwa yaliyokuwa yakimeremeta meremeta “A WORLD RECORD – 3.32.16”.


Kwenye makala zake hizi, Tido Mhando, ambaye amefanya kazi ya utangazaji kwa muda mrefu anasimulia baadhi tu ya mambo ya kusisimua aliyowahi kukutana nayo wakati wa hizo enzi zake. Wiki jana alielezea mwanzo wa mbio maarufu za mashindano ya riadha za mita 1,500, kwenye Michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola ya 1974, huko Christchurch, New Zealand, ambapo Filbert Bayi wa Tanzania alikuwa mshiriki nyota na yeye Tido akiwa mwandishi wa habari wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), kwenye michezo hiyo. SASA ENDELEA...
Naam, Filbert alikuwa amefyatuka kweli kweli tangu mwanzo tu wa mbio hizo, akiwa na dhamira ya wazi wazi kuwa hakuna ambaye angeweza kumkamata, hata miongoni mwa wale wapinzani wake wakuu wawili, John Walker wa New Zealand na Ben Jipcho wa Kenya.
Kinyang’anyiro hiki kilinitia kiwewe na kuniogopesha kupita kiasi, hadi kunifanya nikimbilie chooni. Nilidhani huko nitasalimika, nijifiche hadi mwisho, ili nikitoka iwe kazi imekamilika, nifahamishwe tu nani kashinda na nani kashindwa, kwani kwa hakika, hali yangu ya mwili ilikuwa mbaya mno!
Lakini kumbe hatua hiyo haikuweza kusaidia kitu, maana mlipuko wa kelele na mayowe yaliyokuwa yakivuma yalikuwa yakiingia hadi huko nilikokuwa. Na jinsi muda ulivyokuwa ukisonga mbele, ndivyo kelele hizo zilivyozidi kuvuma.
Wakati nikiwa natafakari hili na lile, akili zangu zikanirudia, na kukumbuka ya kuwa kazi kubwa na muhimu kuliko zote iliyonifanya nije New Zealand ilikuwa ni ya kutangaza mchezo huo, mbio za mita 1,500 uliokuwa ukifanyika wakati huo. Nikajiambia kwamba nilikuwa na wajibu mkubwa wa kuwafahamisha Watanzania hali halisi ya pambano hilo.
Nikatoka chooni humo mithili ya kifaru aliyejeruhiwa, nikikimbia kulingana na ongezeko la mayowe ya uwanjani yalivyokuwa yakiendelea kurindima. Nilijua sasa mambo yalikuwa yameiva zaidi na kwa kweli, yalikuwa yanakaribia nchani, kwenye mduara wa mwisho.
Lahaula! Macho yangu yalipoona tu mwanga yakakutana na kitimbi cha kutisha zaidi. Filbert Bayi bado alikuwa mbele lakini mahasimu wake Walker na Jipcho walikuwa kama wanaoruka wakiwa kwenye kasi ya mfano wa radi inayojirudiarudia. Zilikuwa zimebakia kama mita 300 tu!
Kila binadamu aliyekuwepo uwanjani pale alikuwa wima, halikuwa tukio la mtu kuweza kutulia kimya ama kuketi. Halikuwa jambo la hali ya mtu kulaza damu, hata kama hukuwa mshiriki pale kiwanjani. Sote tulitimbilika na jasho kututoka vilivyo.
Sasa mvuto wangu zaidi uliegemea kwa wale jamaa wawili Jipcho na John Walker, waliokuwa wamepania kutunyang’anya tonge mdomoni mwetu. Niliamua kuwafuatilia wao tu kwani nilijua endapo watamfikia Bayi, basi macho yangu yataweza kuiona hali hiyo vyema zaidi, hali ambayo sikuwa nataka kuiona hata kidogo.
La kutisha zaidi ni kwamba miamba hao walikuwa na uzoefu na ujuzi wa muda mrefu kwenye mbio hizi ukilinganisha na ule wa nyota wetu. Sasa zikiwa zimebakia mita 100 tu; Bayi bado alikuwa mbele na wala hakuonyesha dalili yoyote za kuchoka. Ilionekana alikuwa kwenye dhamira ya kufa na kupona, lakini wenzake nao walikuwa wanamkaribia zaidi na zaidi.
Kwa muda sasa nilikuwa pia nimewasha kinasa sauti changu, nikitangaza hatua hizo za mwisho za mbio hizi za kihistoria lakini hasa nikiendelea kukazia kuhusu mnyemeleo ule wa Jipcho na Walker kwa Bayi: “Hii ni patashika ya aina yake yenye asili ya ubingwa tena ubingwa wa dunia!”
“Zimesalia mita 50, Walker, Jipcho lakini bado Bayi anapepea mbele. Sasa mita ishirini hivi na bado jamani Bayi huyo yuko mbele tu mama yangu weeeeeee! Mambo bado hawa jamaa hawakati tamaa, lakini bado Bayi huyoooooooooo anavuka mstari, ameshindaaaaaaaaaa na tena ni rekodi mpya ya dunia,” nikapiga mayowe ya furaha.

Umati wote ulikuwa kwenye hali ya msisimko mkubwa sana. Tulikuwa tumeshuhudia jambo ambalo halijawahi kutokea mahali pengine popote duniani kwenye mashindano ya mbio hizi za mita 1,500. Sote tunaingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kama mashuhuda wakati Mtanzania wa kwanza anavunja rekodi ya dunia ya michezo ya riadha na si mwingine bali Filbert Bayi, akiwa kijana wa umri wa miaka 20 na ushei tu.
Wakati watu wakijipongeza kama vile sote tulikuwa kwenye mkabiliano ule yakaandikwa kwenye ubao mkubwa uwanjani pale maandishi makubwa yaliyokuwa yakimeremeta meremeta “A WORLD RECORD – 3.32.16”.
Naam, Filbert Bayi akawa ameivunja rekodi ya hapo nyuma ya dakika 3.33.1 iliyokuwa ikishikiliwa na Mmarekani Jim Ryun aliyoiweka miaka saba iliyopita kwenye mbio za masafa haya zilizofanyika Los Angeles, Marekani.
Nilijisikia fahari kubwa kuwepo uwanjani pale siku sike ile. Nilijisikia fahari kubwa kuwa Mtanzania na zaidi, nilijiona kuwa mtu mwenye bahati kweli kweli kuwa, ni mimi niliyekuwa nimepewa dhamana na umma wote wa taifa langu la Tanzania kuwafahamisha kuhusu tukio hili la kishujaa na kihistoria.
Wakati nikiwa bado natafakari hili na lile, nikiwa nafikiri jinsi Watanzania watakavyopokea habari hii njema, mara ghafla nikamwona Filbert Bayi mwenyewe huyu hapa, amekuja hadi pale juu nilipokuwepo mimi akiwa bado anatweta, anahema huku akiwa anavuja jasho na kunipa mimi Tido Mhando nafasi ya mwanzo kabisa ya kuelezea furaha yake isiyo kifani ya kulipatia taifa lake medali ya dhahabu kwenye michezo mikubwa ya kimataifa ya riadha. Alikuwa mzalendo wa kweli.
Waandishi wengine wote wa kimataifa walipigwa na butwaa na kupata mshangao. Nilimkumbatia Bayi na kumpongeza na kwa muda wa dakika kama tatu hivi huku viongozi wa michezo ile wakiwa wanamsubiri tulifanya mahojiano na bingwa huyu mpya wa dunia.
Haya yakibakia kuwa miongoni mwa mahojiano yangu muhimu sana kuwahi kuyafanya katika kipindi changu chote cha utangazaji, ikiwa ni pamoja na yale niliyofanya na Rais mstaafu Benjamin Mkapa dakika chache tu kabla ya kwenda kuapishwa kwake kuwa Rais wa tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mahojiano mengine niliyoyafanya na Laurent Kabila, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku chache kabla ya kupigwa risasi na kuuawa.
Kwenye mahojiano yale, Bayi alielezea jinsi alivyokuwa amepania kuipatia nchi yake medali ya dhahabu na kwamba ushindi ule haukuwa wa kwake, bali wa nchi yake. Ni kweli, kwani ushindi ule uliiwezesha Tanzania kushika nafasi ya 16 miongoni mwa nchi 32 zilizoshiriki, tukimaliza na medali hiyo moja ya dhahabu na nyingine ya shaba kwa ushindi wa tatu aliokuwa ameupata Clever Kamanya kwenye mbio za mita 400. Baada ya Bayi kuondoka, waandishi wengine wengi walinivamia mimi na kutaka kujua mengi kuhusu yale tuliyokuwa tukiongea tena kwa lugha yetu ya Kiswahili, na pia kumhusu yeye mwenyewe Bayi na wengine wakataka kujua mengi kuhusu nchi yangu Tanzania.
Muda mfupi baadaye tangazo muhimu lilitolewa kwenye vipaza sauti vya hapo uwanjani ya kwamba sherehe ya utoaji wa medali kwa washindi wa mbio zile za mita 1,500 zilizohitimisha patashika za michezo ile kwa kuwekwa rekodi mpya ya dunia zinakaribia kufanyika.
Ndipo Filbert Bayi akiwa katikati ya washindani wake wakuu, John Walker wa New Zealand aliyeshika nafasi ya pili kwa muda wa dakika 3.32.52 na Ben Jipcho wa Kenya aliyekuwa wa tatu kwa muda wa dakika 3.35.16 walipoingia uwanjani hapo kwa vifijo na hoi hoi kubwa.
Halafu ndipo ukafika muda wa fahari kubwa zaidi kwetu: mara baada tu ya kupokea medali yake ya dhahabu pale jukwaani, ukapigwa wimbo wa taifa la Tanzania na bendera ya taifa letu ikapandishwa. Nilisimama kimya na kujiimbia mwenyewe, “Mungu Ibariki Tanzania…”
Adhuhuri ile baadaye, zikafanyika sherehe za kusisimua za kufunga michezo hiyo ya Nchi za Jumuiya ya Madola, mgeni rasmi akiwa Malkia Elizabeth wa Uingereza mwenyewe. Wanamichezo na viongozi wao waliofikia kiasi cha 1,500 safari hii waliingia uwanjani pale wakiwa kwenye mavazi yao ya kawaida na kuchangamana kwa pamoja kuashiria urafiki walioujenga kwenye kipindi cha ushindani mkubwa viwanjani. Wengine hata walimdhihaki Malkia mwenyewe kwa kudandia nyuma ya gari lake la wazi. Kuliko wanamichezo wote, wale wa Tanzania walikuwa wakitamba sana.

Ilipofika saa mbili usiku, ikiwa ni sawa na saa tano mchana Tanzania, siku hiyo ya Jumamosi tarehe 2 Februari, 1974, kama ilivyokuwa kawaida, nilikwenda kutuma ripoti yangu ya michezo hii, lakini safari hii ilikuwa tofauti na siku zilizotangulia. Safari hii, nilikuwa nawapelekea Watanzania habari njema, habari za ushindi.

Nilianza ripoti yangu hiyo kwa kucheza kiashiria changu, ule wimbo wa kitamaduni wa ala tupu za mpigo wa kuonyesha ushindi vitani. Wimbo ulichezwa na kikosi cha JWTZ. Naam tulikuwa tumeshinda kwenye vita hivi vya kimichezo na tulikuwa tayari kurejea nyumbani tukiwa washindi.
Niliwafahamisha wasikilizaji wangu nyumbani Tanzania yale yote yaliyotokea kwenye uwanja huo wa QE11 Park siku hiyo na wengi wakamsikia Filbert Bayi mwenyewe akielezea furaha yake kuhusu ushindi ule. Ripoti hiyo ndiyo ilikuwa ripoti yangu ya mwisho kutoka Christchurch. Nilihakikisha ilikuwa ripoti iliyokuwa na bashasha chungu nzima, maana nilitaka kumaliza kwa kishindo na kwa kweli kwa kishindo nilimaliza.
Baadaye usiku ule nilikwenda kwenye ukumbi mkubwa jijini hapo kuungana na wanamichezo wengine katika tafrija maalumu iliyokuwa imeandaliwa na Meya wa Christchurch ya kuwaaga wote waliohudhuria michezo hiyo. Hapa napo Watanzania tulikuwa tunakwenda kifua mbele.
Wakati tukiwa hapo, ghafla nilikumbuka kwamba bado nilikuwa sijarejeshewa sanduku langu ambalo lilikuwa limepotea njiani wakati nilipokuja. Nikakumbuka pia kuwa maofisa wa Shirika la Ndege la Qantas walionisafirisha walikuwa wameahidi kunirejeshea sanduku hilo kabla sijaondoka kurejea nyumbani. Muda wa kuondoka ulikuwa umekaribia na bado kulikuwa hakuna dalili zozote za kupatikana kwake. Nikadhamiria kuonana nao siku ya pili yake.
INAENDELEA JUMAPILI IJAYO

SOURCE: MWANANCHI