Monday 30 September 2013

Hamad: Kikwete usisaini muswada

Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad 
Na Salim Mohammed

Posted  Jumatatu,Septemba30  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Hamad aliisifu Serikali ya Kikwete kwa kuwaachia wananchi wenyewe kuiandika katiba yao na kumwomba asikubali kutia saini muswada huo wa sheria.
 

Tanga. Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad amesema mgogoro wa Muungano uliopo unatokana na kufichwa kwa makubaliano yaliyowekwa na waasisi wa Muungano na kusema kero hizo hazitakwisha hadi kutakapoundwa Serikali tatu na Muungano wa mkataba.
Alisema hayo juzi wakati wa kongamano la Wazanzibar waishio Bara na kusema Muungano uliotiwa saini na waasisi wa Muungano huo umefichwa na kusema dawa yake ni Serikali tatu na  Muungano wa mkataba.
Hamad ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013 kwa maelezo kuwa una kasoro.
“Wazanzibari wenzangu na mimi pia ni mmoja wao ambao tunataka Muungano wa mkataba, nilipoulizwa na tume nilisema nataka Muungano wa mkataba nadhani nanyi pia mawazo yenu ni kama mimi,” alisema Hamad.
Hamad aliisifu Serikali ya Kikwete kwa kuwaachia wananchi wenyewe kuiandika katiba yao na kumwomba asikubali kutia saini muswada huo wa sheria.
Alisema Zanzibar ni nchi kamili yenye mamlaka kama ilivyo kwa nchi nyingine hivyo inahitaji kurejeshewa mamlaka yake na kuwa na uamuzi ikiwa na pamoja kurejeshewa kiti chake katika Baraza la Umoja wa Kimataifa.
“Zanzibar iko na haki ya kuingia mikataba na jumuiya za kimataifa kama ilivyo nchi nyingine, tunataka dola ya Zanzibar iliyo nchi kamili kama ilivyokuwa zamani, Muungano umeifuta Zanzibar katika ramani ya kimataifa,” alisema na kuongeza:
“Hivi sasa Zanzibar haina haki ya kusema inajiunga na jumuiya yoyote ya kimataifa, kikwazo hiki ni kufichika kwa makubaliano ya Muungano kutoka kwa waasisi wetu."

SOURCE: MWANANCHI