Tuesday 27 August 2013

Wajanja wanavyozidi kuneemeka mavuno Kivuko cha Kigamboni


 

Na Elias Msuya,  (email the author)

Posted  Jumatatu,Agosti26  2013  saa 22:24 PM
Kwa ufupi
  • Aliongeza kuwa magari yanayoruhusiwa kupita bure katika vivuko hivyo ni ya Serikali na wagonjwa.


Mchezo mchafu unaelezwa kuikosesha Serikali mamilioni ya fedha kwenye vivuko vya Magogoni na Kigamboni, Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili hivi karibuni, umegundua ukwepaji malipo unaofanywa na wenye magari.
Pia, kuna wizi wa tiketi unadaiwa kufanywa na wakata tiketi.
Hata hivyo, Kitengo cha Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), kinaonekana kutokuwa na habari ya wizi huo, huku kikificha taarifa za mapato ya vivuko hivyo.
Ofisa Habari wa Temesa, Theresia Mwami, alisema kanuni haziruhusu kuweka wazi mapato hayo na kwamba, kanuni zote zinafuatiliwa.
“Serikali inaendeshwa na kanuni na taratibu… kama Serikali inataka kujua hizo taarifa itazipata kwenye taasisi yake. Kama ni nauli zimebadikwa kwenye ubao wa matangazo na kila mwananchi anapaswa kulipa nauli kwa kiwango hicho, siyo nje ya hapo,” alisema Mwami.
Aliongeza kuwa magari yanayoruhusiwa kupita bure katika vivuko hivyo ni ya Serikali na wagonjwa.
“Kwa sasa tuna utaratibu wa tiketi za ku- scan, kwa hiyo kila gari linapopita linaangaliwa kama limelipa,” alisema.
Kwa mujibu wa Temesa, nauli za kivuko kwa watu wazima ni Sh200 na watoto hadi miaka 14 ni Sh50, huku wanafunzi wakipanda bure.
Kwa upande wa vyombo vya usafiri, baiskeli ni Sh300, pikipiki Sh500, mzigo chini ya kilo 50 Sh200, zaidi ya hapo ni Sh500. Mikokoteni inatozwa Sh1,500, pikipiki za magurudumu matatu Sh1,800, Bajaj Sh1,300.
Kwa magari aina ya saluni Sh1,500, madogo Sh2,000, mabasi madogo Sh3,500, magari ya tani 2.0 hadi 3.5 na trekta lisilo na tela Sh7,500. Kwa upande wa wanyama, ng’ombe anavushwa kwa Sh2,000, wanyama wengine wa kufugwa Sh1,000.
Jinsi mchezo unavyofanyika uchunguzi uliofanyika kwa wiki kadhaa umebaini kuhusika kwa polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao huruhusu baadhi ya magari kutofuata utaratibu.


“Utakuta tunalipia magari yetu na kupanga foleni ya kuingia kwenye vivuko, lakini wengine wanapitishwa bure kwenye geti la jeshi,” anasema Ramadhan Juma anayeishi Kigamboni.
Mwandishi wa habari hizi alipofika eneo la kivukoni Kigamboni kwenye geti hilo, alikuta foleni ya magari ya jeshi, Serikali na magari binafsi.
Kwa upande mwingine kuna foleni kubwa ya magari binafsi yanayolipia, ambayo pia hukaguliwa.
“Ni vigumu kusema magari mangapi yanayopita bure hapa, lakini tangu asubuhi hadi jioni yanapita mamia ya magari. Sasa kama kila gari linatakiwa kulipa Sh1,500 ni kiasi gani kinapotea kwa siku?” Alihoji Sadiki Madembwe, anayefanya biashara eneo hilo.
Hata hivyo, Msemaji Mkuu wa JWTZ, Meja Eric Komba, amekanusha madai ya geti la wanajeshi kutumika kupitisha bure magari binafsi.
“Unajua kuna wanajeshi wanaaoishi Kigamboni na kule pia tuna kambi yetu, kwa hiyo magari ya jeshi yanapita na magari binafsi ya wanajeshi pia yanapita bure. Sasa watu wakiona vile wanadhani kuna magari ya raia yanayopitishwa, siyo kweli,” alikanusha Meja Komba na kuongeza:
“Mimi nimefanya uchunguzi, hicho kitu hakipo na kama kuna mwanajeshi anafanya hivyo mlete ushahidi tu, tutamfukuza kazi. Isitoshe, sisi tuna ushirikiano mzuri na wananchi kwa hiyo hatuna tatizo pale.”
Mmoja wa waliowahi kufanya kazi ya kukatisha tiketi katika vivuko hivyo mwaka mmoja uliopita ambaye hakutaka kutajwa, alisema kuna wizi mkubwa katika uuzaji wa tiketi.
“Kwa sasa hivi ni tofauti kwa sababu tiketi zimetengenezwa kwa mfumo wa kompyuta na abiria akishanunua, inakaguliwa kwa ‘Scanner’. Lakini zamani wakaguzi walizikusanya zile tiketi na kuziuza upya,” alisema na kuongeza:
“Hata sasa, licha ya Scanner bado tiketi zinakusanywa na kurudishwa tena dirishani kuuzwa. Kwa sababu abiria akishanunua tiketi humkabidhi mkaguzi ambaye huikagua na kuitupa kwenye ndoo ya taka. Hapo abiria hafuatilii tena kama Scanner imelia au haijalia kwa sababu tiketi hairudishwi.”
Hadi sasa kuna vivuko viwili yaani Mv Magogoni kinachokadiriwa kubeba abiria 2,000 kwa wakati mmoja na magari madogo 20, pikipiki, baiskeli na mikokoteni.
Huku Kivuko cha Mv Kigamboni kinakadiriwa kubeba abiria 800 hadi 1,000 kwa wakati mmoja, magari, mikokoteni na baiskeli.
  liongeza kuwa baadhi ya watu hupita bure na magari na jamaa zao kwa kujuana na walinzi.
“Michezo huwa unafanyika zaidi muda wa jioni, utakuta mtu pale anaondoka hadi na Sh100,000 kwa siku,” alisema.
Akizungumzia hali hiyo, Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile, alisema ameshawaeleza Temesa lakini haoni hatua madhubuti zikichukuliwa.
“Nikiwa mbunge nimesikia malalamiko mengi pale kwenye vivuko, nimechukua hatua ya kukutana na maofisa wa Temesa kuwaeleza kero hizo,” alisema Dk Ndungulile na kuongeza:
“Pale kuna magari kama 10 ya kudumu yanayotakiwa kupita bure yaani ya wanajeshi, Serikali na magari ya wagonjwa. Lakini magari mengi mno yanapita bure.”
Akitaja baadhi ya hoja zake kwa Temesa, Dk Ndugulile alisema licha ya kuboreshwa kwa tiketi za sasa, aliwataka waanzishe tiketi za msimu kwa wavukaji wa kudumu jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.
“Ni kweli sasa wameboresha utoaji tiketi, lakini niliwataka waainishe tiketi za msimu. Kuna watu wanaovuka kila siku wanaweza kulipa kwa mwezi. Vilevile waboreshe mfumo wa kuingilia na kutoka,” alisema Dk Ndugulile.
source: Mwananchi