Friday 30 August 2013

Tusipokuwa makini tofauti hizi zitaiua EAC


                                                             Rais Kagame 

Na Tusipokuwa makini tofauti hizi zitaiua EAC  (email the author)

Posted  Alhamisi,Agosti29  2013  saa 22:4 PM
Kwa ufupi
  • Kiongozi huyo alitoa kauli zisizokubalika kidiplomasia dhidi ya Rais Kikwete ambaye aliamua kuzipuuza, ingawa baadhi ya vyombo vya habari nchini Rwanda vimeendeleza vita ya maneno.


Sasa ni bayana kwamba tofauti zilizopo miongoni mwa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimeanza kukuzwa, huku wachambuzi wa masuala ya kidiplomasia wakionya kwamba tofauti hizo zisipotatuliwa haraka jumuiya hiyo itasambaratika na kubaki historia.
Sote tunatambua kwamba tofauti hizo zilianza baada ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania kumshauri Rais Paul Kagame kuzungumza na FDLR ambao ni waasi wa nchi hiyo wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Rais Kikwete pia alimshauri Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuzungumza na waasi wa nchi hiyo ADF, akisema hatua hiyo italeta amani ya kudumu katika ukanda mzima wa Maziwa Makuu.
Kwa bahati mbaya Rais Kagame alikasirishwa na ushauri huo. Alisema ushauri wa Rais Kikwete yalikuwa matusi kwa Rwanda na kusema nchi hiyo haiwezi kamwe kuzungumza na watu waliofanya mauaji ya kimbari.
Kiongozi huyo alitoa kauli zisizokubalika kidiplomasia dhidi ya Rais Kikwete ambaye aliamua kuzipuuza, ingawa baadhi ya vyombo vya habari nchini Rwanda vimeendeleza vita ya maneno.
Tunashawishika kusema kwamba Rais Museveni kwa kukaa kimya aliukubali ushauri wa Rais Kikwete au alifanya hivyo tu ili kuepusha kukua kwa mgogoro huo. Wapo wanaosema Rais Kikwete alitoa ushauri huo kwa nia njema, lakini wakosoaji wake wanasema pamoja na nia yake hiyo kuwa ya dhati kabisa, angeutoa faragha kwa Rais Kagame au katika vikao mwafaka vya EAC badala ya kufanya hivyo katika kikao cha Umoja wa Afrika (AU), kilichofanyika Addis Ababa, wakisema huko hapakuwa pahala pake.
Hilo hakika ndilo chimbuko la mgogoro tunaoushuhudia hivi sasa ambao tunadhani umekuzwa kupita kiasi tukitilia maanani matukio ambayo yamekuwa yakitokea katika siku za hivi karibuni. Hata hivyo, zipo tetesi pia kwamba Rwanda haikufurahishwa na kitendo cha Tanzania kukubali kupeleka wanajeshi wake nchini DRC kuungana na kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN), kulinda amani nchini humo kwa lengo la kuwanyang’anya silaha waasi wa M23 wenye asili ya Rwanda.
Tumelazimika kuandika hayo yote ili kuweka kumbukumbu sahihi za mtiririko wa mgogoro huo ambao baadhi ya watu walidhani ungeziingiza nchi hizo mbili jirani katika vita.
Hivi sasa umefanyika mkakati wa kuitenga Tanzania kiuchumi ambapo juzi marais wa Kenya, Uganda na Rwanda waliungana kuzindua upanuzi wa Bandari ya Mombasa inayokusudiwa kutumiwa na nchi hizo kupakua na kusafirisha mizigo. Mkakati huo ulizinduliwa na marais wa nchi hizo mjini Entebbe hivi karibuni ambapo Tanzania haikualikwa kama ambavyo haikualikwa juzi wakati wa uzinduzi huo.
Tofauti zinazoendelea kujitokeza hakika sio ishara njema kwa mustakabali wa EAC. Siku chache zilizopita uliibuka mzozo miongoni mwa wabunge wa EAC jijini Arusha ambapo wabunge wa Uganda, Kenya na Rwanda walisababisha kikao cha Bunge kuvunjika ili kumshinikiza Spika aruhusu kujadiliwa kwa hoja ya vikao vya Bunge kufanyika kwa mzunguko katika nchi wanachama badala ya Tanzania pekee.
Wabunge wa Tanzania nao walifanya hivyo siku iliyofuata wakipinga hatua ya wabunge hao kutaka kumshinikiza Spika kukubali hoja hiyo kinyume na Kanuni za Bunge.
Kwa mwenendo huo sisi tunadhani kuna ajenda ya siri iliyofichwa chini ya zulia. EAC inachungulia kifo. Zinahitajika busara kuinusuru. Vinginevyo, historia ya EAC ya mwaka 1977 itajirudia.