Friday 30 August 2013

Tuitumie mitihani yetu ya maisha kama daraja

Posted  Alhamisi,Agosti29  2013  saa 22:2 PM
Kwa ufupi
Wapo vijana wengi nchini ambao wamekumbana na mitihani ya maisha ambayo kwa namna moja au nyingine imewajeruhi na hivyo wanaona kuwa huo ndiyo mwisho wa mafanikio katika ulimwengu huu.


Baada ya miaka miwili ya ndoa yake, Jennifer Tress kutoka Washington DC, Marekani alibaini kuwa mume wake ana uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi mwenzake.
Huo ulikuwa mwanzo wa filamu yenyewe, kwani alipomhoji kwa nini anamsaliti, alijibiwa ni kwa sababu yeye (Tress) si mrembo.
Tress aliumizwa na uzinzi wa mume wake, lakini zaidi hasa kwa kauli ya mume wake ya kumwambia ni mbaya kwa sura.
Hata hivyo, baada ya ndoa kuvunjika aliandika kitabu na kuzindua mtandao unaoitwa, ‘youre not pretty enough’ (wewe si mrembo kamili)ambao unawakutanisha wanawake wenye changamoto katika ndoa.
Mtandao huu na kitabu kwa sasa vinamwezesha kupata fedha kwa sababu ya kuwa na wanachama wengi, lakini si hivyo tu, bali Tress amekuwa maarufu na huitwa katika mabaraza mbalimbali ya wanawake kutoa ushuhuda.
Yawezekana hata wewe umeshawahi kupitia mtihani wa maisha kama wa Tress, nikuombe wewe usikate tamaa na kuona kuwa huo ni mwisho wa maisha, bali itumie changamoto hiyo kukuimarisha zaidi na kukupa mwanga wa mafanikio.
Wapo vijana wengi nchini ambao wamekumbana na mitihani ya maisha ambayo kwa namna moja au nyingine imewajeruhi na hivyo wanaona kuwa huo ndiyo mwisho wa mafanikio katika ulimwengu huu.
Hilo si kusudio la Mungu kwa mwanadamu. Maisha yanapokupa sababu 100 za kulia, yaonyeshe maisha kuwa una sababu 1,000 za kucheka.
Wapo wale waliowahi kupata ujauzito wakiwa shule, hivyo wakadhani kuwa huo ndiyo mwisho wa elimu au mwisho wa kuwa msichana mrembo.
Wapo wengine ambao wamepata ajali na kupoteza viungo vya miili yao jambo lililowafanya wakate tamaa ya maisha na kudhani kuwa hawataweza kuthaminika au kujipatia riziki katika dunia hii na wapo wenye historia mbaya ambazo wanashindwa kuzisahau na zinawafanya washindwe kusonga mbele.
Mwanasayansi, mgunduzi na mkandarasi, Alexander Graham Bell aliwahi kuandika katika moja ya vitabu vyake kuwa, mlango mmoja unapofungwa, mwingine hufunguliwa, lakini tatizo la mwanadamu ni kuwa huuangalia kwa muda mrefu na kwa kujutia, mlango uliofungwa kiasi cha kushindwa kuuona mlango ulio wazi.
Wengi wetu huongozwa zaidi katika mitazamo ya kibinadamu na kuona kuwa hakuna nafasi ya kufanya vyema tena duniani.


Kwa mfano, wapo wanaoamua kujitoa uhai kwa sababu tu, amefeli mtihani wa kidato cha nne au ameachwa na rafiki wa kiume au wa kike. Hapana shaka huku ni kukata tamaa kulikopita kiasi ambako humfanya mwanadamu hushindwa kukabiliana na tatizo lililopo mbele yake.
Hivyo, sivyo inavyotakiwa kutendwa na mtu yeyote katika maisha, siri ni moja kuyakanyaga, kuyatupa jalalani na kuyasahau matatizo kisha safisha njia mpya ya kuingia katika mafanikio. Kwa mfano, wapo ambao wamewahi kuishi katika mienendo mibaya mno wakati wa ujana wao, pengine walikuwa walevi, watumiaji wa dawa za kulevya, wazinzi au hata majambazi.
Historia zao zisiwe chanzo cha kushindwa kusonga mbele na kuyarudia waliyoyatenda bali ziwe elimu kwa wengine na elimu katika maisha binafsi.
Kama wewe ni mmoja wa watu wenye historia mbaya, usihofu, kwani wanazuoni wanatueleza kuwa, tofauti ya pekee iliyopo kati ya mwenye dhambi na ajiitaye mtakatifu duniani, ni kuwa kila mtakatifu ana historia na kila mwenye dhambi ana mustakabali.
Lucius Seneca, mwanafalsafa wa Kirumi anatoa mwongozo wake wa maisha na kusema kuwa changamoto katika maisha zinaimarisha ufahamu, kama ambavyo uchungu wa kuzaa unaleta maisha ya kiumbe duniani.
Mfano mzuri ni wa mwanahabari wa Mlimani Radio, Tuma Dandi ambaye licha ya kupata ajali iliyomfanya apooze sehemu kubwa ya mwili wake, hakukata tamaa, alisoma kwa bidii na kufanya kazi kwa kujituma na sasa ni mhariri na mwanahabari aliyepata tuzo kadhaa za umahiri.
Changamoto zisikukatishe tamaa, kama unakimbia na kukutana na ukuta, usigeuke nyuma na kurudi ulikotoka. Tafuta njia ya kuupanda, zunguka ukuta na utafute njia yeyote kuhakikisha unaukwea na kufanikiwa kufika upande wa pili.
Ewe Mtanzania mwenzangu, kumbuka kuwa unapolalamika kuwa huna viatu, basi kumbuka wapo wenzio ambao hawana miguu. Kimbia peku peku, tengeneza picha ya mafanikio katika ufahamu, igonge mhuri na hakikisha haifutiki…hakika utayafikia mafanikio hayo.
Ni vyema ukaugeuza udhaifu wowote, changamoto au historia mbaya katika maisha yako kuwa nguvu mbadala ya mafanikio yako. Kama wewe ni yatima, soma sana, jitume kwa bidii kwa sababu huna wa kumtegemea, hivyo elimu na bidii ya kazi, ndiyo nguzo yako.
Vilevile, kama wewe ni mlemavu, huo usiwe mwanzo wa kukata tamaa, bali tumia nafasi yeyote katika ufahamu na mwili wako kutengeneza njia ya kutokea.
0754-438084

source: Mwananchi