Monday 26 August 2013

‘Nyufa’ zajitokeza Bunge la Afrika Mashariki


 
Na Mussa Juma  (email the author)

Posted  Agosti24  2013  saa 20:45 PM
Kwa ufupi
Awali Bunge hilo, katika vikao vyake vya Arusha, vilikuwa vikifanyika katika Jengo la Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC) kwa kukodi.

Arusha. Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, (EALA), wameingia katika mpasuko, kutokana na baadhi ya wabunge hao kupinga kutumia ukumbi wa kisasa wa Bunge hilo uliopo Arusha kwa vikao vyote, na badala yake baadhi wanataka kuendelea na utaratibu wa kufanya vikao vya Bunge katika kila nchi wanachama.
Habari za uhakika toka ndani ya Wabunge wa Afrika ya Mashariki, walioanza kikao cha Bunge la jumuiya hiyo juzi jijini hapa, zimebainisha kuwa, licha ya Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo, kufikia uamuzi ya vikao vyote sasa kufanyika Arusha, lakini bado kuna wabunge wanapinga.
Kikao cha kamati ya uongozi kilichoongozwa na mwenyekiti wake ni Spika wa Bunge hilo, Dk Magreth Zziwa, kiliamua baada ya kukamilika jengo la Bunge, likiwa na ofisi kwa kila mbunge sasa vikao vyote vifanyike Arusha ili pia kupunguza gharama.
Awali Bunge hilo, katika vikao vyake vya Arusha, vilikuwa vikifanyika katika Jengo la Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC) kwa kukodi.
Katika hatua ya kuonyesha kushawishi wabunge kuanza kutumia jengo lao jipya kwa mikutano yote, Mbunge wa Bunge hilo wa Tanzania, ShyRose Bhanji aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutoa ardhi bure kwa ujenzi wa jengo la EAC lenye ukumbi wa kisasa wa Bunge.
Ofisa Habari za Bunge la Afrika ya Mashariki, Bobi Odiko, jana alikiri kuwapo mjadala wa kutaka kuendelea kuhamisha vikao vya Bunge au sasa kufanyika Arusha huku akisema anaamini wataafikiana.
“Ni kweli mijadala inaendelea na leo (jana) kulikuwa na kikao juu ya suala hili lakini naamani mwafaka utafikiwa”alisema Odiko

Source: Mwananchi