Thursday 29 August 2013

Mzee Moyo apinga Mansour kutimuliwa CCM wengine



 


Posted  Jumatano,Agosti28  2013  saa 21:28 PM
Kwa ufupi
  • Asema msimamo wa Mansour ndiyo alionao hata mwenyewe na kwamba, haki haikutendaka kutompa nafasi ya kujitetea.


Zanzibar. Wakati Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Zanzibar, Hassan Nassor Moyo, akisema uamuzi wa CCM kumfukuza uanachama Mwakilishi wa Jimbo la Kiembesamaki, Mansour Yussuf Himid, siyo sahihi, Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) Wilaya ya Dimani, Unguja umesema chama hicho kiwatazame vigogo wengine wanaokwenda kinyume cha maadili yake.
Halmashauri Kuu ya CCM ilimvua uanachama Mansour kwa kile kilichoelezwa kukisaliti chama, kwa kushindwa kusimamia malengo ya CCM na kutekeleza masharti ya uanachama, kushindwa kutekeleza wajibu wa mwanachama na kukiuka maadili ya viongozi wa CCM na kuikana ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2010-2015 na kuisaliti CCM.
UVCCM ilidai kuwa hatua hiyo isimkumbe peke yake, badala yake iwatizame wabunge, wawakilishi na viongozi wengine wanaokwenda kinyume na sera za chama hicho.
Taarifa ya umoja huo kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Katibu wa UVCCM Wilaya ya Dimani, Yussuf Suleiman, inadai umoja huo umepata faraja na imani kuona chama chao kinatetea nidhamu ili kukabiliana na vurugu zilizokuwa zikifanywa na mwakilishi huyo.
Pia, inadai umefika wakati wa uongozi wa chama hicho kuchukua hatua za maadili dhidi ya wawakilishi na wabunge ambao mchana ni CCM na usiku hugeuka maadui na wasaliti.
Moyo apinga
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema jana mjini hapa kwa simu kuwa Mansour ameonewa, kwa sababu hakupewa nafasi ya kujitetea kabla ya kuchukuliwa hatua ya kufukuzwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.
Moyo (pichani kulia) aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa miaka mingi, alisema hata yeye, moyo wake upo kwenye muundo wa Serikali ya Muungano wa Mkataba.
Watu waonaotaka Muungano wa Mkataba katika mapendekezo ya Katiba Mpya inayojadiliwa sasa wanataka ziwepo Serikali mbili za Tanganyika na Zanzibar zenye mamlaka kamili, baadaye kuwapo na Muungano wa mkataba baina ya Serikali hizo.
“Utashi wangu ulikuwa kwenye mkataba, lakini Kamati ya Katiba haikutupa kwa hiyo sasa kete yangu naitupa kwenye Serikali tatu,” alisema Moyo.
Alipoulizwa kuhusu madai kuwa atajivua uanachama wa CCM ikiwa Mansour atafukuzwa, Moyo alisema hakuwahi kusema hivyo bali alieleza ikiwa Mansour anafukuzwa na yeye anaweza kufikwa na hatua kama hiyo, kwani ana fikra sawa na Mansour.
“Sijasema nitajivua uanachama, ila nilieleza kuwa nami nitakuwa na hali kama hiyo ya Mansour kwani msimamo wangu si tofauti,” alisema Mzee Moyo.


CCM kina msimamo wa kutaka mfumo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar uendelee.
Hata hivyo asilimia kubwa ya wananchi wa Zanzibar waliotoa maoni yao kwa Kamati ya Katiba wanataka Muungano wa Mkataba na Serikali mbili za Tanganyika na Zanzibar, zenye mamlaka kamili na Kamati ya Katiba imetoa rasimu yenye kupendekeza Serikali tatu; Shirikisho, Zanzibar na Tanzania Bara.
Mansour agoma
“Naomba uniache tafadhali, nasikitika kuwa sitakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa sasa,” alisema.
Jumamosi iliyopita Mansour alizungumza na gazeti na kusema anasubiri uamuzi wa Halmashauri Kuu kujua hatma yake na kuahidi kuwa, angezungumza baada ya uamuzi huo, jambo ambalo ameshindwa kutekeza kwa kuendelea kuwa kimya.
Mara ya kwanza, tuhuma za Mansour zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 16, mwaka huu Ofisi za CCM Kisiwandui na wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumvua uanachama. Uamuzi wa kumvua uanachama Mansour uliwasilishwa katika kikao hicho chini ya Makamu Mwenyekiti wake, ambaye pia ni Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein. Hatua hiyo inaliacha wazi Jimbo la Kiembesamaki kwa ajili ya uchaguzi wa mwakilishi.

source : Mwananchi