Tuesday 27 August 2013

Mchakato kura ya maoni ya Katiba waanza


 


Posted  Jumatatu,Agosti26  2013  saa 22:3 PM
Kwa ufupi
Juni 3, mwaka huu, Jaji Warioba alizindua Rasimu ya Katiba baada ya mchakato huo na kuruhusu uundwaji wa Mabaraza ya Katiba kwa kutegemea makundi maalumu ambayo mchakato wake unamalizika Agosti 31, mwaka huu.


Dodoma. Historia inatarajia kuandikwa katika Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano unaoanza leo, mjini Dodoma wakati litakaposafisha njia kwa Watanzania kwa mara ya kwanza, kupiga kura ya maoni ya Katiba.
Bunge litajadili Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni 2013, ambao ndiyo utakaotoa njia kwa Watanzania kuamua Katiba Mpya baada ya Bunge la Katiba kumaliza kazi yake.
Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Tanzania Bara kupiga kura ya
maoni ya aina yoyote ile tangu Uhuru mwaka 1961 na ya pili kwa Zanzibar ambayo ilifanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 2010 kutoa nafasi ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Kuelekea mchakato huo wa Katiba Mpya, Bunge pia litajadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2013.
Hatua hiyo inatokana na safari ndefu ya mchakato wa ukusanyaji wa maoni ya wananchi iliyoanza Aprili 13, mwaka jana kwa Rais Jakaya Kikwete kuzindua Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba.
Juni 3, mwaka huu, Jaji Warioba alizindua Rasimu ya Katiba baada ya mchakato huo na kuruhusu uundwaji wa Mabaraza ya Katiba kwa kutegemea makundi maalumu ambayo mchakato wake unamalizika Agosti 31, mwaka huu.
Baada ya hatua hiyo, Bunge litapelekewa maboresho ya mapendekezo ya rasimu hiyo na kuyajadili ikiwamo kupitisha sheria ya mabadiliko hayo na baadaye kuweka muundo wa sheria na muundo wa kupigiwa kura hatua itakayofuata katika Bunge la Katiba baadaye Novemba, mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, hoja hizo mbili zimetengewa siku tano kuanzia Septemba 9 hadi 13, mwaka huu na mjadala wa marekebisho hayo unatarajiwa kuchukua nafasi hasa kwa wabunge wa pande mbili, CCM cha Chadema juu ya kutengeneza muundo.
Chadema, kimeshatoa baadhi ya mapendekezo yake katika muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kura ya Maoni ikiwamo kupinga Rais kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu wasiotokana na Bunge na Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

source: Mwananchi