Tuesday 27 August 2013

CCM yamvua uanachama kigogo


Na Habel Chidawali  (email the author)

Posted  Jumatatu,Agosti26  2013  saa 22:8 PM
Kwa ufupi
Kitendo cha kuungana na Mzee Moyo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad kupigia debe suala la Muungano wa Mkataba kati ya Tanganyika na Zanzibar kuliwakera makada wa CCM waliomchukulia kuwa anapingana na Katiba na Ilani ya CCM vilivyosimamia katika Serikali mbili.


Dodoma. Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (Nec), jana iliridhia kumvua uanachama, Mwakilishi wa Jimbo la Kiembe Samaki, Mkoa wa Mjini Magharibi, Mansour Yussuf Himid kutokana na kukiuka miiko ya chama hicho.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa Mansour ambaye hivi karibuni alikuwa waziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), amefukuzwa uanachama kutokana na kukiuka mambo matatu.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni kushindwa kutimiza malengo ya CCM na kutekeleza malengo ya uanachama, kushindwa kutekeleza wajibu wa uanachama na kukiuka maadili ya uongozi, kuikana na kuisaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015.
Kutokana na uamuzi huo, Nape alisema Mansour hatakuwa na nafasi ya kukata rufani mahali popote kwa kuwa uamuzi uliofikiwa jana ni wa kikao cha juu cha mwisho.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mansour alisema kwa sasa hawezi kuzungumza mengi kwani anahitaji muda wa kutafakari kutokana na uzito wa suala lenyewe.
“Ndugu yangu nashukuru sana kwa kunipigia simu. Ila ninahitaji muda wa kutulia kwanza. Nipe kama siku mbili au tatu hivi halafu nitaongea,” alisema Mansour, ambaye amekuwa Mwakilishi wa Kiembe Samaki tangu mwaka 2005.
Nec ilifikia uamuzi huo ikibariki mapendekezo yaliyotolewa na Kamati Kuu ya CCM upande wa Zanzibar iliyomvua uanachama kutokana na misimamo yake ya kisiasa na hasa suala la Muungano.
Mansour aliwahi kushika nyadhifa kadhaa ndani ya CCM ikiwamo ya ujumbe wa Halmashauri Kuu na Mweka Hazina wa chama hicho upande wa Zanzibar.
Kilichomponza
Kwa mara ya kwanza, tuhuma za Mansour zilifikishwa katika kikao cha Kamati ya Maadili ya CCM Zanzibar, kilichoketi Agosti 16, mwaka huu katika Ofisi za CCM Kisiwandui ambacho wajumbe wa kamati hiyo kwa kauli moja walitoka na azimio la kumfuta uanachama.
Suala hilo lilifikishwa Kamati Kuu ya CCM, Zanzibar Agosti 22, mwaka huu kupitia uamuzi huo na iliafiki. Kitendo cha Mansour kuingia kwenye Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar inayoongozwa na mwanasiasa mkongwe Hassan Nassor Moyo ambayo imekuwa ikipigania Muungano wa mkataba ilichochea tofauti yake na makada wenzake wa CCM Zanzibar.
Kitendo cha kuungana na Mzee Moyo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad kupigia debe suala la Muungano wa Mkataba kati ya Tanganyika na Zanzibar kuliwakera makada wa CCM waliomchukulia kuwa anapingana na Katiba na Ilani ya CCM vilivyosimamia katika Serikali mbili.

Nyadhifa SMZ
Mansour, ambaye amekuwa Naibu Waziri wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira kuanzia mwaka 2000-2005. Alipanda cheo na kuwa waziri kamili katika wizara hiyo kuanzia mwaka 2005 hadi 2010 alipohamishwa kuwa Waziri wa Kilimo kati ya 2010 na 2012 na Aprili, mwaka jana aliteuliwa kuwa waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar.
Hata hivyo, hakudumu muda mrefu katika wadhifa huo kwani alivuliwa wadhifa huo kutokana na kile kilichokuwa kimeelezwa tangu awali kwamba ni kutofautiana na chama hicho. Nyota yake iling’ara zaidi alipokuwa Wizara ya Nishati akiwa naibu na baadaye waziri kamili kwani alikuwa mmoja wa wanasiasa wa Zanzibar waliopinga waziwazi suala la mafuta kuingia kwenye masuala ya Muungano na hasa kwenye mijadala ya Baraza la Wawakilishi.
Bukoba ngoma nzito
Kwa upande wa sakata la mgogoro wa Bukoba, Nape alisema Kamati Kuu itaendelea kuwahoji wahusika hao leo baada ya kushindwa kukamilisha kazi hiyo jana.
Suala hilo linawapambanisha vigogo wa siasa wa Mkoa wa Kagera wakiongozwa na Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki na Meya, Dk Anatory Amani.
“Suala la Bukoba tutaendelea nalo kesho (leo) saa tano asubuhi baada ya kutokukamilisha kazi yake leo (jana), hivyo Kamati Kuu inatarajia kuendelea kushughulikia mgogoro huo kabla ya kuondoka mjini Dodoma,” alisema Nape.
Mbali na kutoa maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba, Halmashauri Kuu pia ilipitisha majina ya makatibu watatu wa CCM ngazi ya mikoa.
Waliopitishwa ni Mary Maziku, Romuli Njovu na Kassimu Mabrouk ambao watapangiwa mikoa. Pia ilipitisha uteuzi wa makatibu 25 wa wilaya wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM).

source: Mwananchi