Thursday 25 July 2013

WASOMI: Tanzania inahitaji miaka 240 kutokomeza umasikini

 Mwanachi, 2013.
Morogoro. Wasomi nchini wamesema Tanzania inashindwa kupiga hatua ya maendeleo kutokana na Serikali kuwa na sera na mipango mingi ambayo inashindwa kuitekeleza.
Walisema kabla ya kukamilika kwa mpango mmoja, unaanzishwa mwingine hali ambayo inafanya kila jambo kufanyika nusunusu.
Mkuu wa zamani wa Mkoa Rukwa, Daniel Ole Njolai, alisema Serikali iwe sikivu na itekeleze mipango yake ili kuwakomboa wananchi maskini, ambao asilimia 80 ni wakulima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano mkuu wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua), Dk Damian Gabagambi, alisema Tanzania inahitaji miaka 240 kuanzia sasa ili kutokomeza umaskini uliokithiri.
Dk Gabagambi alisema tatizo kubwa ni kutotekelezwa sera na mipango ya Serikali, huku akitolea mfano Mkurabita, Mkukuta na Kilimo Kwanza.
Alisema wakati mipango hiyo ikiwa kwenye utekelezaji, Serikali imekuja na mipango mingine mingi ambayo nayo itaguswa kidogo na kuanzishwa mingine ukiwamo, Mpango mkubwa wa kutoa matokeo sasa (Big results now).
“Tangu mwaka 1997 hadi 2011 umaskini umepungua kwa asilimia 2.1, maana yake ni kwamba tukitaka kupunguza umasikini mpaka asilimia 10, tutahitaji miaka 169 na ili tuutokomeze kabisa tunahitaji miaka 240,” alisema Dk Gabagambi.
Naye Profesa Amon Mattee kutoka Sua, aliwashauri wakulima na wafugaji kuzingatia sera katika masuala yote yanayohusu kilimo, kujitambua katika kukuza maslahi yao.
Profesa Mattee alisema wakulima wasisubiri kufanyiwa kila kitu, aliwataka kuwa kitu kimoja na kudai maslahi yao.
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadam (LHRC), Anord Sungusia, aliwashauri wakulima kuwa na rasimu ya katiba na kuisoma kwa kina na baadaye kuijadili, ili kuwasilisha mapendekezo yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.