Wednesday 24 July 2013

Wahimizwa kuhubiri amani,upendo


Na Goodluck Eliona, Mwananchi  (email the author)

Posted  Julai20  2013  saa 22:11 PM
Kwa ufupi
Ni viongozi wa dini zote nchini ili waumini wao waishi kwa kupendana na furaha, pamoja na kuhimiza mshikamano unaotishiwa na uvunjifu wa amani kila kukicha.


Dar es Salaam. Viongozi wa madhehebu ya dini wametakiwa kuhakikisha wanadumisha utulivu uliopo nchini kwa kuhubiri amani na upendo kwa watu wote.
Rai hiyo ilitolewa katika Parokia ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji Luhanga, Dar es Salaam jana na Msaidizi wa Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa wakati alipokuwa akiendesha misa ya upadrisho kwa Siriack Malasi na Shadrack Lyimo.
Nzigilwa alisema viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika jamii, hivyo wanapaswa kuilinda na kuidumisha amani iliyopo na kwamba jukumu walilonalo mapadri hao wapya ni kuhakikisha jamii wanayoizunguka inaishi katika mazingira ya utulivu na amani kama ndugu.
“Nendeni mkahubiri amani, furaha na upendo kwa watu wote hiyo ndiyo kazi yenu kubwa, tunahitaji kuwa na amani,” alisema Nzigela.
Akitoa neno la shukrani baada ya kupandishwa daraja la upadri, Padri Siriack Malasi alisema kuwa safari ya kufikia hatua hiyo haikuwa rahisi na kwamba wana kila sababu ya kuwashukuru watu wote waliowawezesha kufika katika daraja hilo.
“Neno tunaloweza kulisema ni asante sana, tumepita katika wakati mgumu na mara nyingine tulikuwa tunawasumbua kidogo. Hata kufika kwenu hapa ni mchango muhimu, kama wangefika mapadri na maaskofu bila nyinyi (waumini) ingekuwaje?” alihoji Malasi.
Misa hiyo ya upadrisho iliambatana na uzinduzi wa kitabu cha marehemu Jackson Mosha aliyekuwa Mjasuiti ambaye alifariki dunia mwaka 2009.

source: Mwananchi news paper