Monday 15 July 2013

Ushoga, uchangudoa maangamizo mengine Buguruni na Vingunguti

    
 
Na Nora Damian, Mwananchi  (email the author)

Posted  Julai13  2013  saa 12:24 PM
Kwa ufupi
Mlugu alisema baada ya kufika Dar es Salaam, vijana hao wamejikuta wakiingia kwenye biashara hizo kutokana na unyanyasaji na ujira mdogo.


Utafiti unaonyesha  vijana wanaojihusisha na vitendo hivyo wanatolewa vijijini
Dar es Salaam.  Asilimia 65 ya vijana kata za Buguruni na Vingunguti wapo hatarini kupata maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutokana na kujihusisha na biashara ya ushoga na uchangudoa.
Katika utafiti uliofanywa na Shirika la Ushauri kwa Familia (CAFLO) mwishoni mwa mwaka jana, uneonyesha idadi kubwa ya vijana hao ni wenye umri kuanzia miaka 12 na kuendelea.
Akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana na watu wanaoishi na VVU kutoka maeneo hayo juzi, Mwenyekiti wa shirika hilo, Mariam Mlugu, alisema idadi kubwa ya vijana hao ni wale waliochukuliwa kutoka mikoani kufanya kazi za ndani.
Mlugu alisema baada ya kufika Dar es Salaam, vijana hao wamejikuta wakiingia kwenye biashara hizo kutokana na unyanyasaji na ujira mdogo.
Alisema baada ya utafiti huo waliwasiliana na Kamati ya Ukimwi Manispaa ya Ilala ambayo ilikubali kuliwezesha shirika hilo kutoa mafunzo kwa vijana na wanaoishi na VVU, ili wabuni na kutafuta fursa mbalimbali kujiletea maendeleo.
Pia, Mlugu alisema baadhi ya  familia na jamii zimekuwa zikikosa fursa kufanya shughuli halali na kuamua kujiingiza kwenye kazi hatarishi, kama  biashara ya ngono na mapenzi ya jinsia moja kwa lengo la kujipatia kipato.
Awali, Mkurugenzi wa utawala wa shirika hilo, Dennis Mikongoti, alisema mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo watu wanaoishi na VVU na Ukimwi na ambao wapo hatarini kupata magonjwa hayo,  ili wapambane na umaskini wa kipato ambao ndiyo unachangia kwa kasi maambukizi hayo. Naye
Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Ilala, Malcela Msawanga, aliwaasa washiriki hao kutumia mafunzo hayo kuwaelimisha wenzao ambao hawakupata fursa hiyo.