Tuesday 23 July 2013

‘Tindikali’ aliyomwagiwa bosi HSC yachunguzwa



Na Bakari Kiango  (email the author)

Posted  Jumatatu,Julai22  2013  saa 21:23 PM
Kwa ufupi
Hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hili huku polisi wakiendelea na msako mkali wa kuwabaini wahusika


Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, limepeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali maji yanayodhaniwa kuwa ni tindikali aliyomwagiwa mmiliki wa maduka ya Home Shopping Center (HSC), Said Mohammed Saad kwa ajili ya uchunguzi.
Mmoja wa Ofisa wa Polisi, ambaye hakutaka kutaja jina lake aliliambia gazeti hili jana kuwa baada ya tukio hilo polisi wameamua kuyachukua maji hayo na kuyapeleka huko kwa uchunguzi ili kubaini ndani yake yalikuwa na nini.
Tukio hilo la kumwagiwa maji hayo lilitokea Julai 20 mwaka huu saa 1 usiku karibu na Kituo cha Polisi cha Osterbay wilayani Kinondoni, wakati Saad akizungumza na mmoja wa wafanyakazi wake katika duka lake jipya lililopo katika maeneo hayo.
“Majibu yatakayotoka kwa Mkemia Mkuu yatatusaidia katika upelelezi wetu katika jambo hili,” alisema Ofisa huyo na kuongeza kuwa.
“Hadi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na tukio hili huku polisi wakiendelea na msako mkali wa kuwabaini wahusika.”
Alidokeza kuwa kwa mujibu wa ndugu wa karibu wa Saad wanasema mgonjwa wao anaendelea vizuri na matibabu katika moja ya hospitali aliyolazwa, huku polisi wakimsubiri apate ahueni kwa ajili ya kumfanyia mahojiano juu ya tukio hilo.
Katika hatua nyingine, polisi kanda hiyo leo wanatarajia kufanya mkutano na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi kuhusu suala kulipuka kwa bomu katika mkutano wa Chadema.
Tukio hilo lilitokea Julai 22 mwaka huu maeneo ya Viwanja vya Sahara Mabibo wakati kitu kinachodhaniwa ni bomu kilichokuwa ndani ya gari la polisi kilirushwa katika mkutano huo.

Chanzo: Mwananchi news paper