Thursday 25 July 2013

Profesa Baregu aonya majungu mjadala wa rasimu ya katiba

   

 
Na Mussa Mwangoka, Sumbawanga.  (email the author)

Posted  Jumanne,Julai23  2013  saa 12:56 PM
Kwa ufupi
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Katiba la Wilaya ya Sumbawanga Prof. Baregu alionyesha dhairi kukerwa na kauli hiyo ya kusema “wasomi wanaipeleka nchi kusikojulikana” ambayo ilijitokeza mara kadhaa kwa watu waliokuwa wakichangia rasimu hiyo ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.


Rukwa. MJUMBE wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Prof. Mwesiga Baregu amewataka wajumbe wa mabaraza ya katiba kujenga hoja kuhusu muundo wa Serikali wanayoitaka badala ya kung’ang’ana wakiwalaumu wasomi kwa kudai wanaipeleka nchi kusikojulikana kutokana na wengi wao kuonyesha wanataka Serikali tatu.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Katiba la Wilaya ya Sumbawanga Prof. Baregu alionyesha dhairi kukerwa na kauli hiyo ya kusema “wasomi wanaipeleka nchi kusikojulikana” ambayo ilijitokeza mara kadhaa kwa watu waliokuwa wakichangia rasimu hiyo ya katiba iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Hoja za kusema wasomi mnatupeleka kusikojulikana siyo sahihi kama hamtaki serikali tatu jengeni hoja ya muundo wa serikali mnazotaka. Hii ni katiba ya Watanzania wote siyo wasomi pekee.......sisi tutazichukuwa hoja zenu na kwenda kuzifanyia kazi” alisema Prof. Baregu.
Awali diwani wa Kata ya Muze, Kalolo Ntilo alisema kuwa suala muungano wa Serikali tatu ambalo rasimu imependekeza hakubaliani nalo ila anataka kuwepo Serikali mbili za Tanzania bara na Zanzibar ambazo zitaunda muungano wa nchi hizo mbili huku wakiwatupia lawama wasomi kwa kudai wanataka kuwepo Serikali tatu ambazo athari zake ni kuvunjika kwa muungano miaka kadhaa ijayo.
Diwani huyo alisema suala la serikali tatu linahitaji mjadala wa kipekee utakajumuisha Watanzania wote hivyo kwa maoni yake haoni sababu ya katiba ijayo kuwa na muundo wa Serikali hizo ambazo zinapigiwa chepuo na baadhi ya wananchi wakiwamo wasomi.
Mkazi wa Kaengesa, Lazaro Muntama alisema kuwa ili kunusuru muungano kutovunjika ipo haja ya kuwepo kwa Serikali tatu yaani ya Tanganyika, Zanzibar na Muungano ambapo alipinga hoja za baadhi ya wajumbe zinazoeleza kuendesha serikali hizo ni gharama kubwa.
“imefika wakati sasa na sisi watu wa bara tunataka Serikali yetu ya Tanganyika ili tuwe na muundo wa Serikali tatu siyo mbili huku ni kujizudhuru haki yetu.