Friday 12 July 2013

Nassari apokelewa chini ya ulinzi mkali

 Na Waandishi Wetu, Mwananchi  (email the author)

Posted  Alhamisi,Julai11  2013  saa 15:7 PM
Kwa ufupi
Nassari ambaye jana alitarajiwa kupokewa na mamia ya wanachama wa chama hicho, baadaye angefanya mkutano wa hadhara jimboni kwake, aliwasili saa 6:00 Uwanja wa Ndege Arusha.


Arusha. Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, amewasili Arusha na kupokelewa na ulinzi mkali wa polisi, kuanzia uwanja wa ndege wa Arusha hadi ofisi yake ya ubunge Arumeru Mashariki.
Nassari ambaye jana alitarajiwa kupokewa na mamia ya wanachama wa chama hicho, baadaye angefanya mkutano wa hadhara jimboni kwake, aliwasili saa 6:00 Uwanja wa Ndege Arusha.
Hata hivyo, polisi ilitangaza kufuta mapokezi na mkutano wake, kwa maelezo kuwa ni kutekeleza uamuzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec kuzuia shughuli zozote za kisiasa Arusha hadi kukamilika uchaguzi wa madiwani Julai 14, mwaka huu.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Liberatus Sabas, alisema wamelazimika kuongeza ulinzi na kuzuia mapokezi hayo na mkutano, kwani vingekiuka maagizo ya Nec.
Akizungumza ofisi za Chadema Mkoa wa Arusha jana, Nassari alieleza kushangazwa na ulinzi mkali wa polisi.
“Ulinzi huu umeanzia Dar es Salaam Airport (uwanja wa ndege), nimeshuka Arusha hadi sasa polisi wanarandaranda nje ya ofisi hizi,” alisema Nassari.
Pia, mbunge huyo alieleza kushangazwa na polisi kuweka ulinzi ofisi yake, huku wananchi wenye shida wakishindwa kuzungumza naye kwa uhuru.
Alisema amerejea Arusha salama na sasa amepona yupo tayari kushiriki kama wakala wa uchaguzi mdogo wa Jumapili.
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi mdogo, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa, alisema chama kimewapanga wabunge wake kadhaa kuwa mawakala.
“Tumeunda vikosi na Godbless Lema (Mbunge Arusha Mjini) atakuwa anaongozwa kikosi cha QS1 hakuna matata,” alisema Golugwa.