Tuesday 16 July 2013

MH MBATIA AITOLEA UVIVU RED BRIGADE YA CHADEMA

 
 
MWENYEKITI wa Chama cha NCCR- Mageuzi James Mbatia, amekikosoa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kwa kitendo cha kutangaza kujihami kwa kuboresha kikosi chao cha ulinzi na usalama cha Red Brigade, kwamba kufanya hivyo ni kushindana na serikali.
Wakati Mbatia akisema hayo siku chache zilizopita Rais Jakaya Kikwete alitoa kauli yenye mwelekeo wa kukiponda chama hicho juu ya mpango wake huo akisema kuwa mpenda amani haundi kikosi cha mgambo.


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, katika kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho, Mbatia alisema ushindani wa kisiasa unatokana na hoja za msingi na si kushindana kwa vitendo.

“Kitendo cha Chadema kuunda kikosi chao ni sawa na kushindana na serikali kwani jeshi linatakiwa kudhibitiwa na serikali na si kila chama wala kabila, kwa sababu kufanya hivyo ni kupoteza amani ya nchi,”alisema Mbatia.

Alisema kuwa chama cha NCCR- Mageuzi, kitaendelea kushindana kisiasa kwa hoja kwa kutekeleza misingi mikuu ya itikadi ya chama.

Mbatia alisema hivi sasa wananchi wamejenga taswira mbaya kutokana na kitendo cha viongozi wa serikali kusubiri mpaka maafa yatokee ndio wakae meza moja na viongozi wa vyama vingine vya siasa.

Katika hilo alisema mwenendo wa siasa za miaka ya 47 na hivi sasa ni tofauti kwa kuwa kumekuwepo na viashiria vingi vya umwagaji wa damu za wananchi.

Alisema asilimia 83 ya Wantanzania wanaamini kuwa kazi ya usalama wa nchi ipo mikononi mwa Jeshi la Polisi, huku asilimia 11 wakiamini kwamba kulinda usalama wa nchi ni jukumu la kila mwananchi.

Pamoja na hilo alisema uchaguzi wa kata nne unaofanyika leo ni vyema amani ikazingatiwa ili kupunguza vifo vinavyoendelea kutokea.
 
Chanzo:Arusha One