Sunday 14 July 2013

Mengi alonga kushamiri kwa dawa za kulevya

  

“Huwezi kutenganisha rushwa kubwa na dawa za kulevya, hawa wasichana wetu waliokamatwa Afrika Kusini , lazima kuna mtu mkubwa aliye nyuma yao,siyo wao,” Reginald Mengi 
Na Minael Msuya na Benjamin Mwangoka, Mwananchi  (email the author)

Posted  Ijumaa,Julai12  2013  saa 10:41 AM
Kwa ufupi
 
Alisema, biashara ya dawa za kulevya inayoendelea  inatokana na tatizo la utoaji na upokeaji wa rushwa ambao unaongozwa na watu wakubwa, walioko katika mfumo halisi wa rushwa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema, biashara ya dawa za kulevya inashamiri kutokana na tatizo la rushwa nchini.
Mengi alibainisha hayo jana katika uzinduzi wa  ripoti ya mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini 2013, iliyoandaliwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
 Alisema, biashara ya dawa za kulevya inayoendelea  inatokana na tatizo la utoaji na upokeaji wa rushwa ambao unaongozwa na watu wakubwa, walioko katika mfumo halisi wa rushwa.
“Huwezi kutenganisha rushwa kubwa na dawa za kulevya, hawa wasichana wasanii wetu, waliokamatwa Afrika Kusini na dawa za kulevya na kile kiasi, lazima kuna mtu mkubwa aliye nyuma yao,siyo wao,” alisema Mengi.
  Mengi alisema,utashi wa Serikali katika kupambana na rushwa uko kisiasa ndiyo sababu hakuna utekelezaji na ikiendelea kuwakumbatia na kuwashikilia mkono watu hao nchi itadondoka.
    Alisema, taifa linatakiwa kuwatenga watoa rushwa na rushwa zao ili kuweza kuwa na taifa lenye nguvu kwa kuwa Serikali imeshindwa kupambana dhidi ya rushwa. kwa kuwa inahofia kukumbwa katika mfumo huo.
 Naye Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo nchini, Godfrey Simbeye alisema mazingira ya kufanyia biashara nchini ni magumu kutokana na kodi nyingi na sheria ngumu zilizowekwa.
Simbeye alisema, utafiti unaonyesha kuwa suala la utozaji wa kodi limekuwa changamoto kubwa katika biashara kutokana na kuwa na kodi nyingi zisizoeleweka.
“Vikwazo vikubwa vinavyoyakabili mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini ni kodi,  kumekuwa  na  kodi nyingi zinazotozwa na zisizoeleweka na sheria zilizowekwa zinaifanya biashara kuwa ngumu,” alisema.