Monday 15 July 2013

Mchungaji, wanakwaya wapigana kanisani

Na Moses Augustine, Sengerema

KATIKA hali isiyo ya kawaida, ugomvi mkubwa umetokea kwenye Kanisa la AICT, kati ya baadhi ya wanakwaya wa kanisa hilo linalofahamika kwa jina la “Bupandwa” na mchungaji wao Petro Masule. 
 
Tukio hilo la aina yake, limetokea kwenye Kijiji Bupandwa,Kata ya Bupandwa, Wilaya ya Sengerema, mkoani  Mwanza.
 Wanakwaya hao walisimamishwa kutoa huduma Kanisani kwa njia ya uimbaji kwa kosa la utovu wa nidhamu ambapo ugomvi huo, ulitokea Mei 12 mwaka huu, baada ya ibada.
Inadaiwakuwa , Mchungaji Masule hakutumia lugha nzuri baadayakuwaitawanakwaya hao “watenda dhambi ambao hawapaswi kuingia katika hekalu la Bwana”.
Kauli hiyo inadaiwa kuwakera wanakwaya hao ambao kwa mujibu wa mashuhuda wa
tukio hilo, walisema Mchungaji Masule aliyasema hayo katika mahubiri ya ibada ya kwanza.
Mchungaji huyo alidai kuwa, kutokana na makosa waliyotenda wanakwaya hao, wanapaswa kutubu ili waweze kuingia kanisani.
Baada ya ibada hiyo kumalizika, baadhi ya wanakwaya waliokuwa wamesimamishwa ambao walihudhuria misa hiyo, waliamua kuungana na kumfuata Mchungaji huyo akiwa na wazee wa kanisa wakihesabu sadaka.
Wanakwayahao walimuomba Mchungaji huyo awape vyombo vya kuimbia ambavyo walidai kuvinunua kwa fedha zao ili wakaazishe kanisa lao wakidai kukerwa na mahubiri yake.
Kutokana na matakwa ya wanakwaya hao, ilitokea vurugu kubwa ndani ya kanisa hilo kati yao na Mchungaji Masule, ambapo katika ugomvu huo, inadaiwa muumini mmoja aliumia sehemu mbalimbali za mwili wake.
Gazeti hili lilipomtafuta Mchungaji Masule, alikiri kuzipiga na wanakwaya ndani ya kanisa hilo ambao walikiuka maadili na matakwa ya kanisa kwa kutokufuata sheria na kanuni.
Kwa upande wake, Mtendaji wa kijiji hicho, Bw. Vincent Ngidingi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, kulaani kitendo kilichotokea kanisani hapo na kuwaasa waumini kufuata sheria za kanisa.

chanzo: Gazeti la Majira.