Friday 19 July 2013

Mbunge wa Bumbuli akataa kupokea mradi wa maji

Na Mwandishi Wetu  (email the author)

Posted  Alhamisi,Julai18  2013  saa 22:46 PM
Kwa ufupi
Ilipangwa kujenga tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 135,000, lakini mkandarasi aliamua kujenga tangi lenye uwezo wa kuhifadhi lita 90,000 ili kuuunganisha na tanki la zamani lenye uwezo huohuo lakini mkandarasi hakuunganisha matanki hayo jambo ambalo ni kosa’’ alisema..


Tanga. Katika hatua inayoashiria kuchoshwa na utekelezaji usioridhisha wa miradi, Mbunge wa Jimbo la Bumbuli, wilayani Lushoto, January Makamba amekataa kuupokea mradi wa maji uliojengwa katika Halmashauri Mpya ya Bumbuli kutokana na kile alichokieleza kuwa umejengwa chini ya kiwango.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Bumbuli, Makamba, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia alisema kuwa mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Sh400 milioni haukutekelezwa ipasavyo pamoja na kutengewa fedha nyingi na wahisani ambao ni Benki ya Dunia.
Mradi huo umepangiwa kuwanufaisha, wanakijiji katika vijiji vinne vya Bumbuli Mission, Bumbuli Kaya, Mboki na Kwamanolo na ulikuwa uanze kutoa huduma ya maji kuanzia Kijiji cha Kwamanolo.
“Ilipangwa kujenga tanki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 135,000, lakini mkandarasi aliamua kujenga tangi lenye uwezo wa kuhifadhi lita 90,000 ili kuuunganisha na tanki la zamani lenye uwezo huohuo lakini mkandarasi hakuunganisha matanki hayo jambo ambalo ni kosa’’ alisema..
Alisema fedha zilizotumika na thamani halisi ya mradi ni tofauti na kwamba ni vigumu kwake kuamini kwamba mradi huo utatekelezwa kama ulivyokusudiwa awali.
Alisema ni afadhali asipokee kwanza mradi huo ili taratibu zingine za kuchunguza zifanyike kama ni kweli mradi huo utasambaza maji ya kutosha.

chanzo: Mwananchi