Tuesday 23 July 2013

Mbunge mstaafu amtaka Kagame aombe radhi TZ

 
Na Sosthenes Nyoni, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumatatu,Julai22  2013  saa 10:15 AM
Kwa ufupi
Hivi karibuni Rais Kagame alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuna siku atamwadabisha Rais Kikwete na Tanzania kwa ujumla kutokana na ushauri alioutoa kwa Rais huyo wa kumtaka akae kwenye meza ya mazungumzo na vikundi vya waasi wa nchi hiyo vinavyoishi kwenye misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya  Kidemokrasi ya Congo.


Ni Frank Magoba aliyewahi kuwa mbunge Kigamboni kupitia CUF,  adai Kagame ametamka kauli mbaya
Dar es Salaam. Aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dar es Salaam kupitia Chama cha Wananchi (CUF),  Frank Magoba amemfyatukia Rais wa Rwanda, Paul Kagame, akimtaka aiombe radhi Tanzania, Rais Jakaya Kikwete kwa kumkebehi na kumdhalilisha kupitia vyombo vya habari.
Hivi karibuni Rais Kagame alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuna siku atamwadabisha Rais Kikwete na Tanzania kwa ujumla kutokana na ushauri alioutoa kwa Rais huyo wa kumtaka akae kwenye meza ya mazungumzo na vikundi vya waasi wa nchi hiyo vinavyoishi kwenye misitu ya mashariki mwa Jamhuri ya  Kidemokrasi ya Congo.
Magoba alisema  kauli ya Kagame ni ya dharau na kebehi mbaya kwa Rais wa Tanzania  na kwamba inahatarisha kuwapo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki  yenye umoja na mshikamano.
‘’Nikiwa mbunge mstaafu na mwanajeshi mstaafu napenda kuungana na Watanzania wengine kulaani kejeli na dharau kwa nchi yetu kwani tunatambua kuwa baadhi ya viongozi walishazoea kumwaga damu katika nchi zao kwa masilahi binafsi’’ alisema.
Akizungumza na vyombo vya habari jana alisisitiza kwamba kauli hiyo ni ya uchokozi wa hali ya juu na kwamba haina nia nzuri kwa Tanzania, Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.
“Watanzania tulitarajia Kagame atakanusha kwamba hakutoa kauli hiyo mwenyewe, lakini kwa kukaa kimya inamaanisha wazi kwamba aliitoa kwa nia maalumu’’ alisema na kusisitiza kwamba kama hakuitoa yeye basi aombe radhi. Magoba ambaye kwa sasa ni mwanachama wa CCM alimpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kukaa kimya na kutojibu lolote na kwamba  kauli ya Kagame siyo ya mtu mwenye hadhi  ya watu wanaojua demokrasia, ubinadamu na upendo kwa jamii.

source: Mwananchi news paper