Thursday 25 July 2013

Marekani yaitaka Rwanda iache kuwasaidia M23

Rais wa Rwanda Paul Kagame 
Na Mwandishi Wetu  (email the author)

Posted  Jumatano,Julai24  2013  saa 20:27 PM
Kwa ufupi
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani, Jen Psaki, alisema, Marekani inaitaka Rwanda iache mara moja kuwaunga mkono waasi wa M23 na kuondoa vikosi vyake Mashariki mwa DRC.

Marekani imeitaka Rwanda kuacha mara moja kuwasaidia wapiganaji wa kikundi cha Machi 23, (M23) walioko Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Serikali hiyo ya Marekani, ilisema jana katika taarifa yake kuwa kuna ushahidi kwamba maofisa wa Jeshi la Rwanda, wanawasaidia wapiganaji hao wanaoipinga Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kauli hiyo ya Marekani kwa Rwanda ni ya pili katika kipindi cha hivi karibuni. Mapema mwezi huu, Rais wa Marekani, Barack Obama akiwa nchini Tanzania kwa ziara yake ya kikazi, alisema amani ya Congo itajengwa na Wacongomani wenyewe.
Pia ni kauli ya kwanza kutolewa na Marekani baada ya mapigano ya hivi karibuni kati wapiganaji wa M23 na Vikosi vya Serikali katika eneo la karibu na mji wa Goma, ambao ndio mkubwa zaidi huko Mashariki mwa Congo na ni eneo tajiri kwa madini.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani, Jen Psaki, alisema, Marekani inaitaka Rwanda iache mara moja kuwaunga mkono waasi wa M23 na kuondoa vikosi vyake Mashariki mwa DRC.
Wito huo umekuja zikiwa zimesalia siku tatu kabla ya John Kerry, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kuwa mwenyekiti wa kikao maalumu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kitakachojadili eneo la Maziwa Makuu katika Kanda ya Afrika.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch, nalo liliikosoa Serikali ya Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 kwa muda mrefu.
Taarifa ya Human Rights Watch iliongeza kuwa, Rwanda bado inawaunga mkono waasi wa M23 wanaohatarisha usalama katika maeneo ya Mashariki mwa DRC.
Hii si mara ya kwanza kwa Rwanda kutuhumiwa kuliunga mkono kundi la M23, tuhuma ambazo imekuwa ikizikanusha mara kwa mara.
Msemaji wa Serikali ya DRC, Lambert Mende Omalanga alisema kuwa, ushahidi unaonyesha kuwa Kundi la M23 limefanya jinai kadhaa katika mji wa Kiwanja katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Source: Mwananchi news paper