Monday 22 July 2013

Kauli tata za Chikawe Uchaguzi Mkuu 2015

“Tunaweza kuwatumia wajumbe walewale wa Tume ya Katiba lakini safari hii tukawachukua wale wa Tanzania Bara pekee wakashiriki katika kuandaa Katiba hiyo.” Mathias Chikawe 
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumatatu,Julai22  2013  saa 8:24 AM
Kwa ufupi.
Julai 20, mwaka huu: “Uwepo wa Serikali tatu utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na Serikali tatu.”

HUKU Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiwa kimeweka bayana kwamba hakiungi mkono Serikali tatu kama Rasimu ya Katiba inavyoonyesha, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe ameibuka na kusema endapo Mabaraza ya Katiba yatawasilisha hoja za kuikubali, kuna uwezekano mkubwa wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 kukwama.
“Uwepo wa Serikali tatu utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na Serikali tatu.
“Kama tutafanya uchaguzi, utafanyika kwa taratibu zipi, ipi itakuwa mipaka ya marais wa Serikali tatu, makamu na mawaziri wakuu, mfumo wa Mahakama, Tume ya Uchaguzi, utendaji wa Bunge na wabunge, yako mengi, sasa mpaka hayo yaingie kwenye Katiba,” alisema Chikawe juzi Dar es Salaam.
Alisema lazima CCM isimamie suala hilo kwa kuwa kukubali Serikali tatu kutaua Muungano ambao sehemu kubwa unalindwa na chama hicho tawala.
“CCM wamejipanga kama baraza na kusimamia hili la Serikali mbili ambalo lengo ni kuulinda Muungano. Litakapokuja hili la Serikali tatu, lazima Muungano uparaganyike,” alisema.
Hata hivyo, kauli hiyo ya Waziri Chikawe inakinzana na ile aliyoitoa Juni 4, siku moja baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza hadharani Rasimu hiyo.
Waziri huyo alikaririwa na gazeti hili akisema upo uwezekazo wa Katiba Mpya ya Tanzania Bara ikapatikana kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 ikiwa mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano utakamilika kama inavyokusudiwa na rasimu hiyo kupitishwa na wananchi katika ngazi zote bila mabadiliko.
“Watu wasiwe na hofu. Sioni tatizo endapo rasimu itapita bila mabadiliko na kupata Katiba Mpya. Aprili mwakani mpaka Desemba inatosha kabisa kuandaa Katiba ya Tanzania Bara na tukaenda katika Uchaguzi Mkuu tukiwa na Katiba Mpya,”alikaririwa akisema na kuongeza:
“Tunaweza kuwatumia wajumbe walewale wa Tume ya Katiba lakini safari hii tukawachukua wale wa Tanzania Bara pekee wakashiriki katika kuandaa Katiba hiyo.”
Alisema kutokana na muda kuwa mfupi, Tume hiyo inaweza isifanye kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa wananchi kama ilivyofanya sasa na badala yake ikaandaa rasimu na kujadiliwa na wadau kisha kupelekwa katika mabaraza ya Katiba kabla ya kupata Katiba Mpya.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kukamilika Aprili mwakani.
Alisema kuanzia hapo, Serikali inaweza kuitumia tume ya sasa kutangaza rasimu ya kwanza ya Katiba ya Tanzania Bara kwa kurejea maoni iliyokusanya hivyo hatua ya kwanza ikawa ni kujadiliwa kwa rasimu hiyo kwenye mabaraza ya Katiba kwa miezi miwili na baadaye kupelekwa katika Bunge la Katiba jambo litakaloifanya ipatikane mapema.

Alisema kinachotakiwa sasa ni kujiandaa kwa Tanzania Bara kuwa na Katiba yake ambayo itatumika kwa ajili ya mambo mbalimbali, ukiwamo Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kuwatoa hofu Watanzania kwamba hakuna mpango wa kumwongezea muda wa uongozi, Rais Jakaya Kikwete kama ambavyo imekuwa ikielezwa kwani Serikali ina uhakika kwamba kila kitu kitafanyika katika muda uliopangwa.
Kauli hiyo ilikuwa ikirejea shaka ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba kuwa Serikali ina mpango wa kumwongezea Rais Kikwete muda wa kuongoza.
Juzi, Waziri Chikawe aliwaonya Wazanzibari akisema endapo mapendekezo ya Serikali Tatu yatapita, ni wazi kuwa wataumizwa na muundo wake kwa kuwa bado ni tegemezi kwa Tanzania Bara.
“Ukiangalia Wazanzibar wako milioni moja hivi na ukija Tanzania Bara wako milioni 44, halafu tuseme uwepo na mgawanyiko sawa wa mapato na matumizi kwa ajili ya Serikali ya Shirikisho, ni wazi hali itakuwa mbaya kwa Zanzibar.
Alisema Wazanzibari wanaoshabikia suala la Serikali tatu bila kufahamu madhara ama muundo wake watafikia hatua watataka Serikali mbili ziendelee.
Alisema kukubali kuwapa nafasi wanaotaka Serikali tatu ni kama demokrasia na ni wazi kuwa watatoa hoja zao hadi mwisho na watakapokuja kufanya upembuzi yakinifu, wataona kumbe wamepotoka.
Akizungumzia hoja hiyo, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema: Tuachieni muda… hayo mengine ni hisia tu. Ni kweli tunayajua lakini acheni tumalize hili kwanza (Mabaraza ya Katiba). Hii ndiyo hatua tuliyopo sasa.”
Amsifu Warioba kwa Serikali tatu
Lakini kwa upande mwingine, Chikawe alimsifu Jaji Warioba akisema kukubali kwake na kuisimamia hoja ya Serikali tatu ijadiliwe, kumeliepusha taifa kuingia kwenye machafuko ya kisiasa.
“Nampongeza sana Jaji Warioba kwa msimamo wake... Amesimamia Serikali tatu, ana maana yake. Juni 3, wakati akitangaza mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, Jaji Warioba amekuwa akisimamia suala la Serikali tatu na amekuwa akiipigania mara zote anapokuwa majukwaani, huku akisisitiza kuwa Muungano utaimarika.”
“Unajua watu hawakumwelewa Jaji Warioba, kama angekuja na suala la Serikali mbili, ni wazi ingekuwa mzozo mkubwa wa kisiasa, kungekuwa na kutokuelewana kuwa katumwa... Anasimamia chama chake na watu wangetumia nafasi kufanya vurugu kwa kisingizio cha kudai Serikali yao, lakini sasa hilo halipo,” alisema.

Source: Mwananchi news paper