Friday 12 July 2013

JK aponda mpango wa Chadema

          

Rais wa Tanzania, Jakaya KIkwete 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi  (email the author)

Posted  Alhamisi,Julai11  2013  saa 11:30 AM
Kwa ufupi
Ingawa Kikwete hakuitaja Chadema kwa jina, lakini chama hicho ndicho pekee kilichosusia kongamano la kutafakari amani kikidai kwamba Serikali haitendi haki.


Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete (pichani) amekiponda Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuanzisha kikundi cha mgambo akisema hatua hiyo imejidhihirisha kwamba chama hicho hakipendi amani.
Ingawa Kikwete hakuitaja Chadema kwa jina, lakini chama hicho ndicho pekee kilichosusia kongamano la kutafakari amani kikidai kwamba Serikali haitendi haki.
Kikwete alisema hayo jana wakati akifunga kongamano hilo lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Chadema ilisusia kongamano hilo ikisema kuwa amani haitafutwi kwa kufanya makongamano kama ilivyofanya TCD.
“Chama cha siasa kuanzisha kikundi cha wanamgambo kwa ajili ya kupiga watu ni kiashiria kwamba chama hicho hakitaki amani bali kinaridhishwa na vurugu,” alisema Kikwete na kuongeza kuwa wanaopenda amani humaliza tofauti zao kwa kuzungumza.
“Tusiiache nchi yetu ije kulindwa na majeshi ya Umoja wa Mataifa, tusije kufikia huko, tujitahidi kuondoa tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo,” alisema Kikwete.
Juzi Chadema walitangaza kwamba wataanzisha mafunzo kwa vijana wao kwa ajili ya kuwalinda ikidai kuwa dola imekuwa haisikilizi madai yao.
Alisema wanaosusa kongamano hilo wangeweza kufika wangeweza kutoa madukuduku yao kwa sababu viongozi wa Serikali na polisi walikuwapo lakini bado hawataki.
“Sasa hawa kweli wanapenda amani yetu wakati hawapendi kuja tuzungumze, wanataka watu wauane ama wapigane,” alisema kwa mshangao Kikwete.
Alisema Serikali na viongozi wake hawapendi vurugu na kwamba chama hicho kinafanya vurugu hizo ili kuwatoa katika ajenda za kuwaletea maendeleo Watanzania.
Hata hivyo aliwapongeza Chadema kwa kushiriki katika maandalizi ya kongamano hilo licha ya kususia kushiriki.