Monday 15 July 2013

Chadema yaitesa CCM uchaguzi wa udiwani Arusha

 

Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)wakiimarisha ulinzi kwenye Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kaloleni wakati wa uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata hiyo uliofanyika jana.Picha na Filbert Rweyemamu. 
Na Peter Saramba na Mussa Juma, Mwananchi  (email the author)

Posted  Jumatatu,Julai15  2013  saa 8:12 AM
Kwa ufupi
 
Yaibuka na ushindi wa kishindo katika kata zote nne za Arusha Mjini, wapiga kura  wengi washindwa kujitokeza

Arusha. Chadema kimethibitisha umwamba wake katika siasa za Jimbo la Arusha Mjini, baada ya kutetea kwa kishindo kata zake nne kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika jana.
Katika uchaguzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na ambao ulichukuliwa kama kipimo cha siasa za Arusha ambazo zimekuwa na mvutano mkubwa, Chadema kiliongoza katikia vituo vyote 136 vya kupigia kura Kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya Chadema kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles Mpanda (Kaloleni).
Matokeo
Katika matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Elerai, Obedi Meng’oriki mshindi alikuwa Jeremiah Mpinga wa Chadema aliyepata kura 2,047 dhidi ya 1,471 za Emmanuel Laizer wa CCM. Katika Kata hiyo kulikuwa na wagombea wengine ambao ni John Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na Boisafi Shirima (TLP;1).
Katika Kata ya Themi, Kinabo Edmund wa Chadema aliibuka na ushindi baada ya kupata kura kupata kura 674. Msimamizi wa Uchaguzi Kata hiyo, Ezeka Mboya alisema Kinabo alifuatiwa na Victor Mkolwe aliyepata kura 326 na Lobora Ndarpoi wa CUF alipata kura 307.
Kata ya Kaloleni, Msimamizi wa Uchaguzi, Anna Ledisa alimtangaza Kessi Lewi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 1,470 dhidi ya Emmanuel Mliari wa CCM aliyepata kura 330 na Abbas Mkindi wa CUF aliyepata kura 275 na Ngilishi Pauli wa Demokrasia Makini aliyeambulia kura mbili.
Kata ya Kimandolu, Msimamizi wa Uchaguzi, Suleiman Kilingo alimtangaza Mchungaji Rayson Ngowi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 2,761 na kumshinda Edna Saul wa CCM aliyepata kura 1,163. Kwa matokeo hayo, Chadema sasa kimefikisha madiwani 12 wakati CCM kimebakiwa na kumi na moja na TLP kina wawili.
Ushindi huo wa Chadema una athari kwa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kwani CCM kina wajumbe 14 tu kwenye Baraza la Madiwani, TLP wawili wakati Chadema sasa kimefikisha 15. Wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu pia ni madiwani.
Aidha, Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti kingine cha udiwani kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kinatarajiwa kuitisha uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alimwambia mwandishi wetu kuwa tume yake inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo hivi karibuni baada ya kata hiyo kutangazwa wazi na Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
Malaba alisema uchaguzi huo utaitishwa baada ya aliyekuwa Diwani wake, Alphonce Mawazo kujitoa CCM na kujiunga na Chadema hali inayokifanya chama tawala kuwa katika wakati mgumu kukitetea kiti hicho.

Wachache wajitokeza
Uchaguzi ulikuwa na idadi ndogo ya wapigakura kulinganisha na chaguzi zilizopita.
Elerai inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wapigakura 23,885 waliojitokeza ni 3,824 tu ikifuatiwa na Kimandolu yenye wapigakura 17,209 lakini waliopiga kura ni 3,967.
Kata ya Kaloleni ina wapigakura 12,674 hata hivyo, waliopiga kura ni 2,292. Themi yenye wapigakura wachache kuliko zote ikiwa na watu 6,387 lakini waliojitokeza kupiga kura ni 1,319 tu.
Licha ya idadi hiyo ndogo, baadhi ya wapigakura waliojitokeza walishindwa kutimiza dhamira yao baada ya kugundulika dosari kadhaa kwenye vitambulisho vyao na Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“NEC wamevuruga uchaguzi huu makusudi kwa kuchezea Daftari la Wapigakura kwa nia ya kukibeba CCM. Haiwezekani waliopiga kura Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 leo hii waambiwe majina yao hayamo kwenye daftari,” alilalamika mgombea udiwani Kata ya Kaloleni, Abbas Mkindi ‘Darweshi’.
Mkindi aliyewania kiti hicho kupitia CUF alitoa mfano wa mtoto wake, Omar Othman mwenye kitambulisho cha mpigakura namba 32479962 alichokitumia mwaka 2010 kuzuiwa kupiga kura baada ya jina lake kukosekana kwenye Daftari hilo. Wapiga kura wengine, Godchan Msella mwenye kadi namba 32479396  na Richard Minja mwenye namba 32479311 alizuiwa kupiga kura baada ya kubainika kuwa namba iliyopo kwenye Daftari ni tofauti na ya kadi yake.
Kutokana na kuwapo kwa mkanganyiko huo, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Hamid Mohamoud Hamid alilazimika kuwaita wataalamu wa mfumo wa kompyuta (IT), katika Kituo cha Kupiga Kura cha Kaloleni kusaidia, kazi ambayo ilifanywa na timu iliyoongozwa na Seif Mtero.
Malaba alikiri uwezekano wa kutokea tofauti za tarakimu kwenye vitambulisho vya wapigakura na Daftari la Kudumu la Wapigakura huku akishauri wasimamizi na mawakala wa vyama kutumia busara kuruhusu wananchi wenye vitambulisho na maelezo sahihi kupiga kura.
“Tofauti ya tarakimu kwenye kadi ya mpigakura na Daftari la Mpiga Kura ni kosa la NEC, hivyo siyo sahihi kuwahukumu wapiga kura kwa kuwanyima haki yao ya kuchagua viongozi wawapendao,” alisema Malaba.
Amani yatawala
Ukiacha dosari na idadi ndogo ya wapiga kura, uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na utulivu mkubwa tofauti na hofu iliyokuwapo awali kwamba huenda vurugu zingeibuka kutokana na mvutano uliopo kati ya vyama vya CCM na Chadema.


Hata hivyo, kulikuwa na kamatakamata na baadhi ya waliotiwa mbaroni ni wale waliokutwa na vitambulisho feki vya kupiga kura.
Katika eneo la Shule za Msingi Kimandolu na Elerai, watu wawili walikamatwa kwa kukutwa na shahada feki za kura. Kimandolu msichana aliyejitambulisha kwa jina la Mariamu alikamatwa baada ya kwenda na kadi inayodaiwa kuwa feki.
Mpiga kura huyo alikamatwa na msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mtendaji wa Kata hiyo, Selemani Kikingo na kukabidhiwa kwa polisi.
Katika Kata ya Elerai, Zainabu Mohamed pia alikamatwa kwa tuhuma za kuwa na shahada yenye utata na baadaye kukabidhiwa polisi.
Katika maeneo hayo, pia vijana ambao waliokataa kuondoka karibu na vituo baada ya kupiga kura walikamatwa.
Msimamizi wa uchaguzi kwa upande wa CCM katika Kata  ya Kimandolu, Abraham Joseph alisema idadi kubwa ya waliojitokeza ilikuwa ni ya vijana.
“Kituo hiki kina wapiga kura takribani 12,000 lakini kwa hali ilivyo sidhani kama wanaweza kufika hata wapigakura 4,000,” alisema Joseph.
Katika Kata ya Themi hali ilikuwa shwari. Makada wa CCM, wakiongozwa na Katibu wa Mkoa, Mary Chatanda walikuwa wakizunguka katika vituo vyote vya kata hiyo.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana (Bavicha), John Heche na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari nao walikuwa wakizunguka katika vituo.

chanzo: mwananchi.co,tz