Wednesday 24 July 2013

Chadema: Hakuna kusubiri mjadala wa Serikali tatu

       
Makamu wa Rais,Dk Mohamed Bilal akizindua rasimu ya katiba mpya 



Posted  Jumatano,Julai24  2013  saa 7:55 AM
Kwa ufupi
Mnyika  asema mjadala wa Katiba ya Tanganyika unapaswa kuanza sasa sambamba na huu wa Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Butiku asema hakuna cha kuogopa kwani Zanzibar imeshaonyesha njia


Dar es Salaam/Moshi. Chadema kimepinga kauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuhusu hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kikisema mchakato wa sasa wa Mabaraza ya Katiba, usiwe kikwazo cha mjadala wa muundo wa Serikali Tatu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema Dar es Salaam jana kuwa hatima ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 utakaotokana na mchakato wa mabadiliko ya Katiba unaoendelea, siyo suala la kusubiri.
Akizungumza na mwandishi wetu juzi kuhusu kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chikawe kwamba endapo mapendekezo ya Serikali Tatu yatapitishwa, kuna hatihati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika, Jaji Warioba alisema: “Tuachieni muda… hayo mengine ni hisia tu. Ni kweli tunayajua lakini acheni tumalize hili kwanza ( la Mabaraza ya Katiba). Hii ndiyo hatua tuliyopo sasa.”
Lakini jana Mnyika alisema: “Hatuwezi kusubiri hadi Mabaraza ya Katiba yakamilishe mchakato kama alivyoeleza Jaji Warioba katika gazeti lenu la Mwananchi toleo la leo, (jana),” alisema Mnyika kwa simu.
Jaji Warioba alitaka suala la muundo wa Serikali Tatu utakavyokuwa lisiwe hoja kwa sasa kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba inachokifanya ni kukusanya maoni kupitia Mabaraza ya Katiba na kisha kuandaa rasimu itakayopelekwa bungeni kwa ajili ya majadiliano na kwamba mjadala huo utawachanganya wananchi endapo utaingizwa katika hatua hii ya ukusanyaji maoni.
Lakini Mnyika alisema: “Mijadala hii haiwezi kusubiri mpaka hatua ya Mabaraza ya Katiba, inapaswa kuanza wakati huu kupitia mabaraza yanayosimamiwa na Tume na Mabaraza yanayoendeshwa na makundi ya kijamii. “Pia, masuala hayo ya mpito pamoja na marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ni mambo ambayo yanapaswa  kutolewa ufafanuzi wa ziada na Serikali zaidi ya kauli ambayo Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe ameitoa kupitia gazeti la lenu la leo (jana).”
Alisema kimsingi bado kunahitajika mjadala wa masuala ya mpito kwa sababu kuna uwezekano kwamba Katiba Mpya, ya Muungano au ya Zanzibar na ya Tanganyika, isiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, endapo suala la Serikali tatu litapita.
Alisema kwa upande mwingine, rasimu ya Katiba iliyotolewa imeibua mjadala juu ya mkwamo wa kikatiba (constitutional stalemate), ambao ni muhimu upatiwe suluhisho akisema chama chake kinapendekeza mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika uanze mara moja ili uende sambamba na huu wa Katiba Mpya ya Muungano. Alisema ilikuwa vyema yote yakajadiliwa katika Bunge la Agosti 27, mwaka huu.
Waziri Chikawe alikaririwa na gazeti hili juzi akisema: “Uwepo wa Serikali tatu utafumua mfumo mzima wa utendaji ndani ya Serikali. Hatuwezi tena kufanya uchaguzi wa Rais na wabunge 2015, hatuwezi kufanya chochote nje ya Katiba ya Serikali Tatu kwa kuwa kinachofuata ni kuunda Katiba nyingine inayohusiana na Serikali tatu.
Waziri Chikawe afafanua
Juzi, Waziri Chikawe alitoa ufafanuzi juu ya utata wa hoja zake kwa kuipongeza Tume ya Jaji Warioba kwa kazi inayofanya huku akisema anaunga mkono msimamo wa CCM wa kutaka kuendelea na muundo wa Muungano wa Serikali mbili.
Alisema mchakato wa kuandika Katiba Mpya unapaswa kuangaliwa kwa jicho pana zaidi ya lile la Uchaguzi Mkuu wa 2015.
“Kuna mambo mawili hapa. Mosi ni msimamo wa chama changu cha Mapinduzi (CCM) kuhusu Rasimu ya Katiba na pili msimamo wa Serikali ambayo mimi ni Waziri tena mwenye dhamana ya Katiba,” alisema na kuongeza:
“Msimamo wa CCM ni Serikali mbili na wanachama wote nikiwamo mimi tunajua hivyo. Lakini kuna suala la Serikali ambayo ndiyo iliyoamua kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa kadri ya uelewa wangu, Serikali haijatoa msimamo na inaunga mkono kazi inayofanywa na Tume.”
Alisema mambo hayo mawili hayapaswi kuchanganywa na kuwa kila chombo (CCM na Serikali) kinaweza kutoa kauli au msimamo kadri kinavyoona inafaa.
Licha ya kusema kwamba jukumu la kisheria la kuandaa Uchaguzi Mkuu ni la Tume ya Taifa ya Uchaguzi, alisisitiza kuwa ili ufanyike mwaka 2015 chini ya muundo wa Serikali Tatu unaopendekezwa na Tume ya Warioba, basi itabidi yafanyike mabadiliko makubwa ya sheria mbalimbali kazi ambayo haiwezi kufanywa kwa kukurupuka.
Hata hivyo, alisema maoni yake hayana maana kuwa Uchaguzi Mkuu hauwezi kufanyika mwaka 2015, bali yanalenga kuonyesha kazi kubwa iliyopo mbele.
Butiku
Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph Butiku amesema baadhi ya viongozi wakuu serikalini hawataki tume itoe ufafanuzi kuhusu mapendekezo ya muundo wa Serikali tatu kwa kuwa unagusa vyeo vyao.
Aidha, amesema hakuna haja ya kuwa na hofu kwani tayari Zanzibar imekwishaanza kujitegemea ikiwa na bendera yake, wimbo wake wa taifa na sasa inaidai Serikali yake kamili.
Butiku alitoa kauli hiyo juzi wakati wa kikao cha Baraza la Katiba la Wilaya ya Moshi Vijijini, ambacho kilitawaliwa na mvutano mkubwa miongoni mwa wajumbe kuhusu suala la kuwapo kwa Serikali tatu, huku wajumbe ambao ni madiwani, viongozi na wafuasi wa CCM wakitaka Serikali mbili.
Alisema kwa hali ilivyo sasa, tayari Zanzibar ina Serikali yake yenye mihimili yote ya dola na tume ilichokipendekeza ni kuiondoa Serikali ya Tanzania Bara kwenye ‘tumbo’ la Muungano.
Butiku alisema sababu hasa ya Zanzibar kutaka kuwa na nchi yao ni hofu ya kumezwa na Tanzania Bara katika Muungano wa Serikali mbili na hofu hiyo bado haijakwisha na inazidi kukua.
Butiku aliyataja mambo ambayo Zanzibar iliyafanya kwa baraka za marais wa wakati huo licha ya kwenda kinyume cha Katiba kuwa ni pamoja na kuwa na bendera yao pamoja na wimbo wa taifa.

Alisema Baba wa Taifa, hayati Julius Nyerere alifariki akiwa na imani kuwa Serikali tatu zitavunja Muungano na alifanya hivyo kwa sababu alitaka kuwapo kwa nchi moja.
Butiku alisema hata Mwalimu Nyerere katika kitabu chake alichoandika baada ya Kundi la Wabunge la G55 kutaka Serikali ya Tanganyika, alizungumzia kuwa na Serikali moja au Shirikisho.
Nyongeza na Daniel Mjema, Mos
 
Source: Mwananchi news paper