Monday 15 July 2013

Chadema chazidi kushutumu Jeshi la Polisi

Chadai polisi kuvamia nyumbani kwa Mbowe


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa tuhuma nzito kwa Jeshi la Polisi, baada ya kudai askari wake kuvamia nyumba ya Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kwa nia ya kumkamata.

Tuhuma hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Ukombozi eneo la Manzese jijini Dar es Salaam jana.
Mkutano huo uliitishwa kwa ajili ya kutoa tamko kuhusu Rasimu ya Katiba Mpya kwa wanachama na wafuasi wa chama hicho.
Dk. Slaa alisema polisi wakiongozwa na mkuu wa upelelezi mkoa wa Kinondoni, walivamia nyumba ya kiongozi huyo juzi usiku majira ya saa 6.55 na kulazimisha kuingia ndani kwa ajili ya kumkamata.
Alisema kitendo hicho alichokiita kuwa ni kinyume na utaratibu, kilifanywa huku ikiwa imepita siku nne tangu Rais Jakaya Kikwete kuliagiza jeshi hilo kuacha tabia ya kuwaandama wapinzani.
"Tunataka maelezo kwanini polisi wavamie nyumba ya Mbowe katika muda huo ambao kisheria hawaruhusiwi kumkamata kutokana na hadhi yake," alisema Dk. Slaa.
Aidha, alilitaka jeshi hilo kuomba radhi kutokana na kitendo hicho alichokiita cha udhalilishaji kwa Mwenyekiti wao wa chama, Kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni na Mbunge wa Jimbo la Hai.
Aliwaambia wafuasi wa chama hicho kuwa vurugu zinazotokea sehemu mbalimbali nchini zinatokana na jeshi hilo kufanyakazi kwa upendeleo na bila kufuata taratibu za kazi.
"Polisi hawakuleta barua ya kumkamata au kutakiwa kwenda ofisini kwao, kibaya zaidi kutokana na wadhifa wake hastaili kukamatwa baada ya saa 12:00 jioni, kinachofanyika sasa ni ukandamizaji wa hali ya juu," alisema.
Akijibu tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alimtaka Dk. Slaa akasome sheria ya polisi vizuri kabla ya kutoa tuhuma hizo.
Alisema polisi wana mamlaka ya kukamata mtu wakati wowote na kwamba kumkamata au kutomkamata liko ndani ya jeshi la polisi, hivyo hawezi kutoa maelezo yoyote.
Awali, wakitoa tamko la chama hicho, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lisu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando walisema chama hicho kinaunga mkono Rasimu ya Katiba Mpya iliyotolewa na Jaji Joseph Warioba.
Walisema wanashangaa kwanini CCM inapinga baadhi ya mapendekezo yakiwamo ya kuundwa kwa serikali tatu na tunu ya Taifa, ikiwa vifungu hivyo vinataka kuiweka Tanzania katika hali bora na udhibiti wa maliasili.
Lisu alitahadharisha Watanzania wawe tayari kupiga kura ya kudai Uhuru endapo Serikali ya CCM itaendelea kutumia nguvu kuifanya nchi kuwa ya serikali mbili ambayo imeonekana kuparaganyika.

chanzo: Ippmedia.