Thursday 6 June 2013

Rasimu ya katiba mpya yavuruga mbio za wanasiasa kuwania Urais 2015

 
Dar es Salaam/Dodoma: Mapendekezo yaliyotolewa katika Rasimu ya Katiba Mpya na Tume ya Marekebisho ya Katiba yamewavuruga wanasiasa ambao tayari walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, Mwananchi limebaini.

Tangu juzi Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba alipotangaza rasimu hiyo, kumekuwa na wasiwasi mkubwa sasa kwamba mipango ya urais wa 2015 itavurugika ikiwa mapendekezo hayo yatapitishwa.
Tishio kubwa katika rasimu hiyo ni pendekezo la kuwapo kwa Serikali ya tatu hali ambayo inatafsiriwa na baadhi ya wanasiasa kwamba inaondoa nguvu ya Rais yeyote; awe wa Jamhuri ya Muungano, Zanzibar au Tanzania Bara.
Habari za kuaminika zilizopatikana kutoka ndani ya kambi za vyama vya CCM na Chadema zinaeleza kuwa wale waliokuwa wakifikiria kuwania nafasi hiyo wameingiwa na wasiwasi.
Kadhalika, suala la umri wa kuwania urais kubakia miaka 40 pia linaonekana kuwagusa waliowahi kutangaza kutaka nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi kabla ya mapendekezo ya tume.
Katika suala la urais, wanasiasa wenye nia hiyo wanauona uongozi wa Jamhuri ya Muungano kuwa ni kama hauna nguvu tena kutokana na kushughulikia mambo machache, lakini wakati huohuo wanauona urais wa Tanzania Bara kwamba hauna mamlaka kamili ya kuwawezesha watambuliwe nje ya nchi.
Tume ya Marekebisho ya Katiba imependekeza mambo saba tu yawemo chini ya Serikali ya Muungano kati ya 22 ya sasa. Yanayopendekezwa ni Ulinzi na Usalama, Katiba na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, mambo ya nje, sarafu na Benki Kuu, uraia na uhamiaji, usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Muungano.
Ndani ya CCM
Makundi mbalimbali yanayowania urais ndani ya CCM inaaminika hayajafurahishwa na mapendekezo ya rasimu ya kutaka Serikali tatu.
Kwa maneno mengine, wanaona kama Rais wa Muungano ameng’olewa baadhi ya meno na masuala mengi yatakuwa yanashughulikiwa na Serikali ya Tanzania Bara na ile ya Zanzibar.
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeliacha hewani suala la Tanganyika hasa baada ya kutoa mapendekezo ya Serikali tatu kwenye Rasimu ya Katiba.
Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), alisema hakuna mantiki ya kuunda Serikali tatu ikiwa Tume haikutoa mwongozo wa hali itakavyokuwa kwa Tanzania Bara, Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar.

“Ukiangalia kwa haraka, hivi Serikali ya Tanganyika itakuwaje? Bunge la Tanganyika litakuwa la namna gani na utaratibu gani utatumika kupata wabunge?” alisema Sitta kwenye Viwanja vya Bunge, Dodoma jana.
Pia, Sitta aliyewahi kujipambanua kuwa atawania urais 2015 na hata kutaja kundi la muungano wa marafiki zake, alisema Tume pia haikuweka wazi utawala utakavyokuwa ndani ya Serikali tatu.
“Hivi viongozi wa Tanzania Bara na Zanzibar na wao wataitwa marais! Wapi duniani imeshatokea nchi moja ikawa na marais watatu? Hii haijawahi kutokea, na Tume inatakiwa kuweka sawa katika uongozi hasa ngazi ya Rais wa kuongoza hapa,” alisema Sitta.
Alipinga mpango uliopendekezwa wa wabunge kuchaguliwa wawiliwawili akionya kuwa utasababisha matatizo kwa kuwa Tume haijaweka wazi njia za kuwapata.
MwanaCCM mwingine ambaye ni miongoni mwa watu wanaotajwatajwa kuwania urais 2015 alikaririwa akisema: “Hivi kweli Mzee Warioba kweli anataka kututengenezea Mikhail Gorbachev (Rais wa zamani wa Urusi) hapa Tanzania? Hatutakubali!” Alikuwa akimfananisha Rais ajaye, ambaye atatokana na rasimu hiyo na Rais wa zamani wa Urusi, Gorbachev, ambaye mwaka 1991 alipoteza mamlaka yake baada ya kutoa madaraka ya ndani kwa nchi 14 zilizokuwa zinaundwa Muungano na baadaye zikajitangazia uhuru jambo ambalo kiongozi huyo alishindwa kulizua.
Pia watu wa karibu na mgombea huyo wanaamini kuwa kukubaliana na pendekezo la Serikali tatu ni sawa na kuvunja Muungano.
“Tunatakiwa kwenda Serikali moja na siyo kurudi Serikali tatu ukizingatia sasa ni miaka 50 tangu Tanganyika na Zanzibar ziungane. Hatuungi mkono suala hili kwani haliutakii mema Muungano.”
Katika siku za karibuni, joto la kuwania urais wa Tanzania lilianza kupamba moto baada ya kuibuka habari kuwa suala la kuwania urais lilijadiliwa wakati Rais Kikwete alipokutana na wabunge wa CCM.
Habari za ndani kutoka katika mkutano huo zilieleza kuwa Rais Kikwete alishauri kuwa haikuwa dhambi kujipanga kuwania urais mwaka 2015 lakini alionya kufanya hivyo kusiathiri umoja wa CCM.
Mtu mwingine, ambaye yuko karibu na kati ya watu wanaotamani urais kupitia CCM, alisema: “Hii rasimu ngumu, ila tukiona mambo siyo mazuri kwenye Muungano tutajitosa kwenye uchaguzi wa Rais wa Tanzania Bara.”
Chadema

Rasimu pia imegusa harakati za kuwania urais kupitia Chadema hasa ikizingatiwa kwamba mmoja wa makada wake, Zitto Kabwe alishatangaza dhamira yake mapema.
Kama rasimu hiyo itapitishwa na kuwa Katiba, Zitto atajikuta anakwama kwani imependekezwa miaka ya kugombea urais ianzie 40.
“Ila watu wengi wanafikiri Zitto amekwama ila jamani kuna Katiba ya Tanzania Bara inaweza kuwa tofauti na umri kuwa chini zaidi,” alieleza mtu wa karibu na Zitto.
Bila shaka hali hiyo itakuwa heri kwa wale wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa ambaye alikuwa anatarajiwa kukabiliana na Zitto kuwania tiketi ya kugombea urais kupitia chama hicho.
Wabunge wapinga
Mbunge Peter Serukamba, Kigoma Mjini (CCM) ameonya kuwa kubadili muundo wa Serikali ni gharama kubwa na kuhoji kutakuwa na marais wangapi?
“Muundo mzima ni gharama na tutatumia hadi fedha za maendeleo ya wananchi kuendesha Serikali ya Katiba mpya. Mimi binafsi napingana na hili, nataka Serikali mbili,” alisema.
Kwa upande wake, Maua Daftari, Viti Maalumu (CCM) alisema mfumo wa Serikali tatu uliopendekezwa ukipita itakuwa hasara kubwa kwa Wazanzibari.
“Kwa mtazamo wangu, kwa Zanzibar bado sana kuweza kusimama kwa miguu yake na wakati huohuo kuchangia katika Serikali ya Muungano,” alisema Daftari, ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi kwenye Serikali ya Muungano.
Mbunge mwingine kutoka Zanzibar, Mariam Msabaha, Viti Maalumu, (Chadema), alisema chuki za watu na uroho wa madaraka kwa watu wachache unaweza kuwa ndiyo sababu ya kupendekezwa kwa mfumo huo.